31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Madaktari waeleza sababu majeruhi ajali lori la mafuta kuendelea kufariki

AVELINE KITOMARY NA NEEMA SIGALIYE (TUDACo)-DAR ES SALAAM

IDADI ya vifo vya ajali ya lori la mafuta iliyotokea Agosti 10 eneo la Msamvu mkoani Morogoro, imefika 100  baada ya majeruhi watatu waliokuwa wakitibiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kufariki dunia juzi, huku madaktari wakitoa sababu ya vifo hivyo kuendelea.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma MNH, Aminiel Aligaesha, alisema waliofariki dunia ni Mazoya Sahani, Khasim Marijani na Ramadhani Mgwila.

Alisema kutokana na vifo hivyo, majeruhi waliobaki hospitalini hapo ni 15 kati ya 47 waliopelekwa huku waliopoteza maisha ni 32.

“Majeruhi wa ajali ya moto waliofariki jana (juzi) ni watatu na mpaka sasa tumebakiwa na majeruhi 15 kati ya 47 walioletwa hapa Muhimbili ambapo kati ya hao 13 wapo katika vyumba vya uangalizi maalumu ICU na wawili wako katika wodi ya kawaida ya Sewahaji waliofariki mpaka sasa ni 32,” alisema Aligaesha.

MADAKTARI WAELEZA HALI ILIVYO

Kwa upande wao madaktari bingwa wa upasuaji kutoka katika hospitali hiyo, walisema majeruhi hao wanaendelea kupoteza maisha kutokana na madhara makubwa waliyopata hasa katika mfumo wa hewa.

Akitoa ufafanuzi huo, mmoja wa madaktari hao, Dk. Laurian Rwanyuma, alisema majeruhi waliopelekwa hospitalini hapo walikuwa tayari wengi wao wamepata madhara kwa asilimia 80 hadi 90.

Dk. Rwanyuma alisema majeruhi hao walioungua kwa ndani wameathiriwa na moshi wa moto kwenye mfumo wa hewa na figo hali iliyosababisha kupumua kwa msaada wa mashine.

“Majeruhi walioletwa hapa walikuwa wameungua kwa sehemu kubwa kuanzia asilimia 80 hadi 90 na wengi walikuwa wameungua kwa ndani kutokana kuathiriwa na moshi wa moto.

“ Walioungua ndani wameathirika mfumo wa hewa na figo kutokana na hewa chafu ya carbon monoxide iliyoingia kwenye mapafu yao na ndiyo maana wengi wamekuwa wakiwekwa ICU ili kupata hewa safi ya oxygen,” alisema Dk. Rwanyuma.

Daktari mwingine bingwa wa upasuaji, Edwin Mrema, alisema majeruhi hao waliungua sehemu kubwa ya ngozi zao hali iliyosababisha kukosa kinga za mwili na pia mwili kupoteza maji mengi.

“Ngozi ndiyo kinga ya kwanza ya mwili ambayo inalinda mwili usipate madhara ya vijidudu, na tukumbuke tu kuwa wagonjwa walioungua ngozi ikiwa wazi kinga ya mwili inapotea, hivyo kusababisha mwili kushambuliwa kirahisi.

“Tunaendelea kufanya upasuaji kwa majeruhi wa ajali ya moto, shida kubwa ni kwamba walipoungua ngozi walikosa kinga kwani ngozi inakinga mwili na pia wanapoteza maji mengi, ndiyo maana wanahitaji kuongezewa damu nyingi na vifaa vya kuwaongezea joto,” alisema Dk. Mrema.

UWEZO WA KUTIBU MAJERUHI

Hata hivyo, Aligaesha alisema Muhimbili ina wataalamu wa kutosha na vifaa kuwapatia huduma majeruhi hao, hivyo vifo vinavyotokea si kuwa hakuna huduma bora hospitalini hapo.

“Kuna mijadala inayoendelea katika mitandao ya kijamii kuwa kwanini majeruhi wanakufa, wengine wanasema hospitali haina uwezo wa kuwatibu, mimi ninachowaambia ni kuwa uwezo wa vifaa na wataalamu tunao.

“Na pia hospitali yetu inatoa matibabu bora na ya hali ya juu, kwahiyo ningeomba wananchi waendelee kuiamini Muhimbili, majeruhi walioletwa hapa wana hali mbaya, hata wangepekwa Ulaya bado wengine wangeendelea kupoteza maisha kutokana na madhara makubwa waliyopata,” alieleza Aligaesha.

Alisema hospiatali hiyo inaendelea kupambana kwa kadiri wawezavyo ili majeruhi waliobaki wapate nafuu na hatimaye kurudi katika hali yao ya awali.

“Wataalamu wetu wanaendelea kupambana ili majeruhi 15 waliobaki waweze kupata nafuu na kupona kabisa warudi katika hali yao ya awali kwa gharama yoyote ile,” alisema Aligaesha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles