22.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Madai ya Sumaye kuhusu Chadema yaipa nguvu zaidi CCM

Na HASSAN DAUDI

GUMZO kwa kipindi chote cha wiki hii ni uamuzi wa mwanasiasa mkongwe nchini na Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, kuondoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Sumaye, ambaye hatua yake hii imewashitua wengi, kama ilivyokuwa wakati anaondoka Chama cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2015, amesema si tu Chadema, bali atakuwa nje ya siasa kwa ujumla.

Hivyo, sasa mbunge huyo wa zamani wa Hanang, akiliongoza jimbo hilo kwa miaka 22 (1983-2005), atakuwa huru kukisaidia chama chochote, ikiwamo Chadema, iwapo watahitaji msaada wake wa mawazo.

Hiyo ni kwa mujibu wa Sumaye katika mkutano wake na waandishi wa habari, akitangaza hatua yake hiyo Jumatano ya wiki hii.

Hata hivyo, ukifuatilia mazungumzo yake, utaweza kupata mambo mawili kutoka katika hotuba ya msomi huyo wa Shahada ya Uzamili ya Utawala wa Umma aliyotunukiwa katika Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani. 

Mosi, ni kwamba bado Chadema hawajaweza kuwathibitishia wananchi kwamba wanastahili nafasi ya kuchukua dola, kwa maana ya kuipiku CCM.

Pili, hotuba ya Sumaye mbele ya waandishi wa habari, licha ya kwamba inaweza kuonekana kicheko kwa makada wa CCM, binafsi naitazama kwa jicho la tatu, nikiamini ni somo kubwa kwa chama hicho.

Kwa sababu hotuba hiyo si tu ni chungu kwa Chadema, bali pia kwa CCM, ambao huenda sasa wanasherehekea, tena wakiwakebehi wapinzani wao hao kisiasa.

Nikianza kwa Chadema, naamini ni wakati mwafaka kwa viongozi wao kukiri kuna tatizo ndani yao na hatua za kulitokomeza zianze mara moja.

Kile alichokisema Sumaye, kwamba alihama CCM kusaka demokrasia na kwa bahati mbaya hajaikuta upinzani, si kauli inayopaswa kuchukuliwa kwa urahisi na Chadema.

Sina shaka kuwa wanafahamu Sumaye si kada wa kwanza wa Chadema kuibua shutuma dhidi ya mfumo wa kidikteta ndani ya chama chao.

Wapo wengi waliohama chama hicho, akiwamo aliyekuwa Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara, wakitaja sababu kuwa ni nguvu kubwa ya kundi la Freeman Mbowe.

Kwamba, kama aliyokiri kukutana nayo Sumaye, ni utamaduni wa muda mrefu ndani ya Chadema kwa mwanachama yeyote anayekinzana na mawazo ya kikundi hicho cha Mbowe kuishi kwa tabu kama hataamua kukimbia chama.

“Nongwa ilikuja baada ya kuamua kuchukua fomu ya kugombea kiti cha taifa,” anasema Sumaye na kuongeza: “Baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu ambao walifanya mipango ya mimi kuletewa fomu za Kanda (Pwani) na kuwa mgombea pekee, waligeuka na kuhakikisha kuwa kura za hapana ndiyo zinashinda. Wajumbe karibia wote walipigiwa simu na baadhi yao kufichwa hotelini kwa kazi hiyo.”

Tukirejea katika historia, inaelezwa kwamba ni kwa mazingira hayo, aliyekuwa kada maarufu ndani ya chama hicho, Zito Kabwe, aliondoka na kwenda kuanzisha ACT-Wazalendo kwa sababu ya tabia zisizowafurahisha wengi ndani ya chama hicho.

Sina utafiti unaoweza kuthibitisha kwa asilimia 100, lakini hiyo hainizuii kuamini kelele za aina hiyo zina nafasi kubwa ya kuwatia shaka wananchi wanaotaka kuunga mkono upinzani, hasa Chadema.

Hii inawafanya waamini hakuna jitihada za kweli za upinzani kuingia madarakani, badala yake wanasiasa wa upande huo wako kwa masilahi yao na si wananchi kama ambavyo wamekuwa wakijinasibu.  

Kwa upande mwingine, hiyo inathibitisha moja kwa moja kile kilichojengeka miongoni mwa wengi huko mitaani, kwamba upinzani ni kivuli cha wachache kujinufaisha na ruzuku na si nia ya dhati ya kuwa mbadala wa mawazo chanya yanayokosekana chama tawala.

Ni kwa maana hiyo basi, si dhambi kubashiri kuwa itachukua muda mfupi tu kuwaona Watanzania wachache waliobaki na ndoto ya kuuona upinzani ukiingia madarakani nao wakiungana na wengi kuamini wanaota ndoto za mchana.

Kama ambavyo tumeshuhudia katika mataifa jirani, ni kibarua kizito kwa upinzani kushinda vita dhidi ya vyama tawala, nikitolea mfano CCM, ambavyo silaha yake kubwa ni uzoefu, ushawishi kutokana na historia na rasilimali fedha.

Hivyo, mapambano ya kidemokrasia dhidi ya vyama vya aina hii yanahitaji upinzani makini, usiogubikwa na matukio ya aina hii tunayoyaona na kuyasikia ndani ya Chadema.

Tunaweza kukubaliana kwamba ni ngumu kuwaaminisha wananchi watakuwa sahihi kukipa madaraka chama ambacho viongozi wake wameonesha uroho wa madaraka na udhaifu wa kumaliza migogoro yao wenyewe hata kabla ya kushika dola.

Nikija kwa CCM, ukweli usio na shaka ni kwamba Sumaye kuondoka Chadema ni moja kati ya kete za ushindi kwao.

Kwanza, wapinzani wao wamepoteza mmoja kati ya wanasiasa wenye weledi na uzoefu mkubwa, achilia mbali mtaji wa ushawishi alionao.

Hakuna kiongozi, mwanachama au mpenzi wa CCM aliyesahau namna Sumaye kwa kushirikiana na Edward Lowassa walivyokuwa silaha muhimu ya upinzani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, ikifikia hatua ya CCM kuonekana kuwa kwenye hatari ya kuachia madaraka.

Pili, faida kubwa kwa CCM ni udhaifu aliouibua Sumaye wakati anajitoa Chadema, akilia kufanyiwa figisu katika uchaguzi wa nafasi ya Mwenyekiti Kanda ya Pwani kwa kuwa tu alitaka kuwania nafasi ya Mbowe (Mwenyekiti Taifa).

CCM wamekuwa wakisema mara kadhaa juu ya udikteta wa Mbowe ndani ya Chadema hivyo, unaweza kusema Sumaye amewasaidia kuwathibitishia Watanzania kuwa madai hayo ni ya kweli.

Lakini sasa, binafsi nilishitushwa kidogo na kauli ya Sumaye, nikiamini chama tawala hicho nacho hakina budi kujitathamini na kuona kama aina ya siasa za upinzani zilizopo zina faida kwake.

Namnukuu: “Kujiunga kwenye upinzani si jambo rahisi na inahitaji moyo. Inahitaji moyo, hasa kwa mtu aliyekuwa na nafasi kubwa katika taifa.

“Baada ya kujiunga huko, japo nilieleza sana kwamba ni kwa nia njema, nilianza kwa kupata matatizo kutoka serikalini.

“Kwa mfano, mashamba yangu yalichukuliwa, hata baadhi ya huduma zangu na haki zangu zilianza kuwa tofauti na za wastaafu wenzangu…”

Kwa madai hayo ya Sumaye, unaweza kuyatafsiri kuwa ni pigo kubwa kwa CCM, kwa mantiki kwamba ili chama kilichoko madarakani kiwe imara, kinahitaji upinzani wenye uwanja mpana, jambo ambalo kwa mujibu wa Sumaye halipatikani katika demokrasia ya vyama vingi nchini.

Ikiwa Sumaye anakiri familia yake ilianza kuona mateso ya yeye kuwa upinzani, inahitaji uelewa wa kawaida tu kubaini CCM inapoteza faida ya kujiimarisha kutokana na upande wa pili kutopata uwanja sawa katika demokrasia ya vyama vingi nchini.

Ni kwa mazingira hayo, si rahisi kwa CCM kupata tathmini sahihi juu ya ubora na udhaifu wa mbinu na rasilimali watu katika uwanja wa demokrasia.

Aidha, ni kama ninavyoiona ngumu kwa chama hicho kupata kipimo sahihi cha ushawishi wake kwa wananchi, licha ya kwamba kitakuwa kikiibuka kidedea kila uchwao kupitia boksi la kura katika chaguzi zinazofanyika.

Ndiyo, madai ya Sumaye kupitia mateso kwa kipindi alichokuwa upinzani yanaweza kuibua shaka kuwa kuna ombwe juu ya viongozi wa upinzani wanaojiunga na CCM kwa madai ya kuunga mkono juhudi za Rais Dk. John Magufuli.

Huenda ikawa ni mbaya kwa CCM kwa kuwa huenda hao wanaowapokea kutoka upinzani ni wale waliokumbana na majanga aliyoyataja Sumaye hivyo, wameona waache kukosoa na kujisalimisha.

Chadema kuishutumu CCM

Kikiwa ni chama kikuu cha upinzani nchini, Chadema imekuwa mstari wa mbele kutuma mashambulizi kwa chama tawala CCM na serikali yake.

Moja ya mashambulizi hayo ni kwamba CCM na serikali yake wanabana demokrasia na uhuru wa kujieleza na kuhoji ndani ya nchi.

Lakini kumbe mambo ni tofauti, wapinzani wa Mbowe ndani ya Chedema na baadhi nje ya chama hicho wamekuwa wakimshutumu kiongozi huyo kwa kuminya demokrasia ndani ya chama.

Mbowe yupo kwenye usukani wa Chadema kwa miaka 15, huku akimudu kuhimili vishindo vya upinzani na kuchaguliwa kwa kishindo.

Katika uchaguzi uliopita wa chama mwaka 2014, alikuwa akiwania nafasi hiyo na Gambaranyera Mongateo, ambaye hakuwa maarufu katika siasa za Chadema kama ilivyo kwa Sumaye na Cecil Mwambe wa hivi sasa.

Mbowe alishinda kwa asilimia 97.3 kutokana na kura 789 alizopata dhidi ya Mongateo aliyepata kura 20 tu.

Awali ushindani wa kuwania uenyekiti wa chama hicho ulizaa mgogoro mkubwa baina ya mbowe na mwanasiasa mwegine maarufu wa upinzani nchini, Zitto Kabwe.

Mwishowe Zitto alitimuliwa Chadema na kwenda kukiongoza chama cha ACT-Wazalendo ambacho, kwa kiasi kikubwa kilianzishwa na wanachama wa zamani wa Chadema waliokuwa wakimuunga mkono Zitto.

Dk. Vicencia Shule wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), anasema: “Mzazi bora ni yule anayemuona mtoto wake akikua. Hivyo ndivyo inavyokuwa kwenye uongozi, mkuu wa kazi aliye bora ni yule ambaye anatengeneza wenye uwezo zaidi yake wengi kwa wakati.

“Mimi ni muumini wa kuweka nukta. Kila kitu lazima kifikie mwisho na kingine kianze. Kwa mfano, ni vizuri kuweka nukta na kuanza sentesi mpya kuliko kuwa na sentesi ndefu haina kituo wala mwisho hadi inapoteza maana.”

Nguvu ya Mbowe ni ipi?

Watetezi wa Mbowe wanasema hawana wasiwasi na kiongozi huyo kwa sababu ameleta mafanikio makubwa ndani ya chama hicho tangu alipokikuta kikiwa na wabunge wasiozidi watano hadi kufikisha takribani 50.

Vilevile kiongozi huyo ameweza kufanya chama chake kujizolea kura milioni sita katika uchaguzi mkuu nafasi ya urais ambapo kete yake ya kumpigania Edward Lowassa kuwa mgombea wa vyama vya upinzani ilizaa matunda kwa wingi wa wabunge na wawakilishi kwenye halmashauri mbalimbali nchini.

Kiongozi mmoja mwandamizi kutoka chama tawala cha CCM na serikali ya awamu ya tano, anasema: “Namfahamu Mbowe, nimekuwa ndani ya chama hicho.

Zipo kasoro, lakini watu wanatakiwa kumtazama ngwe hii anafanya nini.

Binafsi nimeona kwa jicho la tatu, kumchukua Tundu Lissu kuwa mgombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti ni ishara kuwa Mbowe anajiandaa kung’atuka madarakani.

Tatizo hatujui ni lini atang’atuka na mikakati yake ni ipi mara atakapoondoka. Lissu ameingizwa kwa mkakati maalumu wa mwenyekiti wa sasa na huenda atashinda kwenye uchaguzi wa nafasi hiyo.”

Mtanzania Profesa Joseph Mbele kutoka Chuo cha Mtakatifu Olaf, Minessota nchini Marekani anamchambua Freeman Mbowe kama kiongozi wa mfano ambaye anapaswa kuigwa na jabali lisilotikisika kisiasa nchini Tanzania.

Anasema: “Mbowe hatingishiki na umaarufu wa wenzake, akina Tundu Lissu, Peter Msigwa, Godbless Lema, au Halima Mdee. Wote wako naye, naye yuko nao.

Hiyo ndio tabia ya mtu anayejiamini. Kutokana na akili yake hiyo na busara zitokanazo, Mbowe amefanikiwa kuijenga Chadema mwaka hadi mwaka, hadi leo kimekuwa ni chama kikuu cha upinzani, chenye kuongoza majimbo na miji mikubwa.

Ingekuwa kuna fursa na uhuru sawa kwa kila chama kufanya shughuli zake kama inavyoelekezwa na katiba na sheria, nina hakika Chadema ingekuwa mbali zaidi.”

Nani anafaa kumrithi Mbowe?

Jovinson Kagirwa, mwanasheria na mchambuzi wa siasa na utawala bora nchini, anasema: “Mwenyekiti anayefaa katika hatua hii ndani ya Chadema ni John Heche au Tundu Lissu.

Nje ya wanasiasa hawa wawili, ni afadhali chama kikae na kaimu mwenyekiti. Katika nyakati hizi mtaji sio fedha, bali mtaji hapa ni kufufua mioyo ya wanachama na wafuasi wao, kitu ambacho kinaogopwa na wapinzani wa upinzani kwa sasa ni mioyo ya Watanzania kufufuka na kuanza kudai madai yao.”

Kwa sababu tumeshaingia kwenye ‘mob democracy’, vyama vya upinzani vinahitaji kiongozi mwanaharakati kama tulivyoona maoni ya mwanasiasa mkongwe na mwenyekiti wa TLP, Augustine Lyatonga Mrema kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, ambapo alisema kuwa harakati ndio siasa za sasa.” 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles