27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

MADAI YA RUSHWA, VITISHO VYATAWALA UCHAGUZI UVCCM NYAMAGANA

Na PETER FABIAN-MWANZA

UCHAGUZI wa marudio wa Jumuiya ya Vijana wa CCM (UVCCM) Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, unadaiwa kutawaliwa na vitendo vya rushwa, vitisho, matusi na ulinzi mkali wa mgambo wa Jiji la Mwanza na kusababisha baadhi ya wajumbe kuandamana hadi ofisi za CCM mkoa kupinga matokeo ya mshindi.

Hali hiyo ilianza kujitokeza wakati wajumbe walipokuwa wakiingia katika ukumbi wa mikutano baada ya mgambo wa Jiji la Mwanza kumwagwa kulinda eneo hilo na kutumika kuwazuia baadhi ya wajumbe kuingia ukumbini na katika uchaguzi huo mgombea aliyeshinda Philipo Magori, aliyepata kura 163 na kumshinda mgombea mwenza Yusufu Ludimo, aliyepata kura 135, akionekana kubebwa waziwazi na viongozi wa wilaya.

Uchaguzi huo ulifanyika juzi baada ya  awali kufanyika Septemba 23, mwaka huu ambapo baadhi ya vijana na wajumbe wa mkutano mkuu wa UVCCM Wilaya ya Nyamagana kutoa malalamiko kwa Katibu wa Wilaya hiyo, Mariam Amir, kuwa mshindi amepatikana kutokana na mbinu ya kuchakachuliwa matokeo zilizofanywa kwa matakwa ya Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, Stanslaus Mabula (CCM), Katibu wa CCM Wilaya, Clemence Mkondya, Katibu wa UVCCM, viongozi wa Chama, Jumuiya ya Wazazi, UVCCM na Serikali ya wilaya hiyo.

Katika uchaguzi wa awali, Yusufu Ludimo, alipata kura 167,  Philipo Magori 109 na mgombea wa tatu, Hasan Mambosasa akaambulia 33 huku wajumbe 24 wa Kata ya Mahina wakizuiwa kupiga kura.

Akizungumza na MTANZANIA ofisini kwake jana, Katibu wa UVCCM Mkoa wa Mwanza, Mariam Amir, alisema kweli alipokea malalamiko ya vijana hao na kudai uchaguzi wa UVCCM Nyamagana umegubikwa na rushwa, vitisho vya watendaji na viongozi ambao wamekuwa wakipanga safu za watu wanaowataka kwa masilahi yao binafsi.

Kwa mujibu wa madai na maelezo ya wajumbe hao kwa Amir, Septemba 25, mwaka huu kabla ya uchaguzi wa marudio, Magori alinunua ng’ombe ambaye Khim aliwaeleza baadhi yao wakati akimfanyia kampeni kuwa ni kwa ajili kitoweo cha sherehe baada ya kutangazwa mshindi.

“Wajumbe 24 wa Kata ya Mahina waliozuiliwa kupiga kura ni wajumbe halali, nashangaa kwanini walizuiwa. Mkoa tulitoa wasimamizi wawili, Eva Makune (Katibu Msaidizi wa UVCCM mkoa) na Abel Mahenge Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji, tutaitisha vikao kupitia malalamiko hayo,” alisema Amir.

Amir aliwaomba vijana wa Nyamagana kuwa na uvumilivu wakati vikao vikipitia malalamiko yaliyowasilishwa na kwamba taarifa zitatolewa baada ya vikao hivyo kutoa maamuzi.

Wakizungumza na MTANZANIA kwa niaba ya wenzake siku moja kabla ya uchaguzi wa marudio, Mfungo Deus,  alisema rushwa ilikuwa ikitolewa waziwazi kama kampeni ya kumwezesha Magori kushinda nafasi huku  akimtuhumu Mwenyekiti wa UVCCM wa wilaya hiyo aliyemaliza muda wake, Hussein Khim, kuwapigia simu baadhi ya wajumbe kuwashawishi wampigie kura mgombea huyo.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Bado kuna rushwa CCM. Mbona mkuu ni CCM na anafanya kazi kubwa. Mkishikwa kwenye video mnakana. Lakini hapa wenyewe kwa wenyewe mnashikana uchai. Tujueje sasa. Hakuna sheria? au sheria zimekuwa kwa vyama vya upinzani tu?

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles