24.3 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

MABARAZA YA WATOTO; NGAO YA KUWAEPUSHA NA UKATILI 

Na ELIYA MBONEA-ARUSHA


WANAONEKANA kuwa ni watoto wenye furaha, wakicheza na kuimba kuisubiria kesho yao njema pindi watakapoanza kulitumikia taifa na familia zao. Lakini nje ya matarajio hayo si salama kwani vitendo vya ukatili, ubakaji, kazi ngumu, mimba na utekaji vimewazunguka.

Ni watoto takribani 300 wamekutana kupitia mabaraza ya watoto yaliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Meru, mkoani Arusha kubadilishana mitazamo na kupaza sauti kwa mambo yanayowahusu.

Watoto hawa kwa sasa wanakabiliwa na changamoto nyingi za vitendo vya ukatili kama kubakwa, ndoa za utotoni, kufanyishwa kazi ngumu na katika siku za hivi karibuni kumeibuka ukatili wa utekaji watoto kisha kuwaua.

Mbali ya kuwapo juhudi za wanaharakati wa masuala ya watoto, wazazi na Serikali kutetea haki za watoto, mlango mwingine wa mabaraza ya watoto sasa umeanza kutumiwa na watoto wenyewe kuwasilisha kilio chao.

Katika mkutano uliofanyika Halmashauri ya Wilaya Arumeru, mkoani Arusha, kupitia mabaraza yao wanawasilisha vilio tofauti wanavyokutana navyo, wanapokuwa shuleni, nyumbani hadi kwenye michezo.

Katibu wa Baraza la Watoto Wilaya ya Arumeru, Glady Kyungai katika mkutano uliojumuisha viongozi wa mabaraza kutoka kata 26 za Halmashauri ya Wilaya ya Meru, anasema wazazi wengi hawana uelewa kuhusu umuhimu wa mabaraza hayo.

Kyungai ambaye pia ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Sing’is anawaomba wazazi kutenga muda wa kujadiliana na watoto wao kuhusu masuala ya kitaaluma pindi wanapotoka shuleni.

“Watoto wengi wanakabiliwa na tatizo la kupewa ruhusa kutoka kwa wazazi wao ili washriki vikao na majadiliano yanayofanywa kwenye mabaraza ya watoto. Hili limeendelea kuwa tatizo kwani linawanyima uhuru na uelewa watoto wengine,” anasema.

Anazitaja changamoto nyingine zinazowakabili watoto katika maeneo tofauti kuwa ni pamoja na kutotambulika kwa wawakilishi wa watoto katika maeneo wanayoishi ikiwamo mitaa, vitongoji na vijijini.

Anataja changamoto nyingine kuwa ni kutoshirikishwa katika vikao vya maendeleo wanapoishi ambapo wameshindwa au kukosa nafasi ya kutoa maoni ikiwamo kushiriki katika vikao vya uamuzi vitakavyowawezesha kuelezea kero zao.

“Kushindwa kushiriki vikao hivyo kunatufanya tushindwe kuwasilisha kero zetu kama wenzetu kupata mimba wakiwa shule, mfano Shule ya Sekondari ya Sing’is watoto watatu wamepata mimba na kuacha masomo, wawili kidato cha tatu na mmoja cha nne.

“Lipo tatizo la walimu shuleni kuwatolea lugha chafu watoto, mfano kuwaita mabwege, taarifa na hata kuwaita mashetani ikiwamo kuwapiga makofi, haya yote tunaamini tukiyasema kwenye vikao vya maendeleo maeneo yetu yatasikika,” anasema Kyungai.

Palipo na changamoto hapa kosi mafanikio Kyungai anasema, mabaraza hayo wamefanikiwa kumshauri mtoto mwenzao aliyekuwa akiishi maisha ya kuteseka na kushindwa kusoma ambapo kwa sasa anaendelea na masomo vizuri.

“Kupitia mabaraza yetu tumefanikiwa kuitisha vikao mara kwa mara na kusikiliza kero wanazoleta watoto kisha tunamshirikisha ofisa mtendaji kwa ajili ya kuzitafutia ufumbuzi,” anasema Kyungai.

Anazitaja faida nyingine ya vikao hivyo kuwa ni kupunguza utoro kwa watoto wenzao ikiwamo kuwashauri walimu wapunguze adhabu kali ili kuwavutia watoto kuipenda shule.

Mratibu wa Dawati la Jinsia na Watoto Halmashauri ya Meru, Saumu Kweka anasema mkutano huo uliofadhiliwa na Shirika la Compassion Tanzania umewezesha watoto kukaa na kushirikishana baadhi ya changamoto zinazowazunguka.

Kweka ambaye ni Ofisa Maendeleo ya Jamii amelitaja jukumu la mabaraza ya watoto kuwa ni kutetea haki za watoto ikizingatiwa vitendo vya unyanyasaji na ukatili kwa watoto vimeendelea kuongezeka.

“Tumetumia fursa hii kuzungumza nao na kuwapa mbinu mkakati za kukabiliana na changamoto zinazowazunguka. Tumealika dawati la Polisi wametoa elimu na wadau wetu Compassion Tanzania nao wameleta watoto ili kushirikiana na hawa na kuona mabaraza yanavyofanya kazi.

Kweka anatoa wito kwa wazazi nchini kujaribu kutimiza majukumu yao kwa kuwa vyanzo vingi vya watoto wa mitaani vimetokana na wazazi kutotimiza wajibu wao kwa watoto.

“Ndoa zinavunjia watoto wanagawanyika na kujikuta wanakosa malezi muhimu, niwaombe wazazi watenge muda wa kuzungumza na watoto. Mtoto anaweza kufanyiwa ukatili na mzazi ukawa mwenye shughuli nyingi akajikuta anakosa muda wa kumuuliza kutokana na umbali alioutengeneza. Ukizungumza na mtoto ni rahisi kukushirikisha anayofanyiwa,” anasema Kweka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles