25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Mabalozi watano wawapa neno wafanyabiashara

RENATHA KIPAKA -BUKOBA

MABALOZI watano wameeleza fursa za kiuchumi zinazopatikana katika nchi wanazoiwakilisha Tanzania ili kuwasaidia wafanyabiashara mkoani Kagera kuzichangamkia.

Hayo yamebainishwa wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Kagera inayofanyika mjini Bukoba kwa kushirikisha viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.

Mabalozi hao na nchi wanazowakilisha kwenye mabano ni Ernest Mangu (Rwanda), Luteni Jenerali Paulo Meela (DRC), Dk. Azizi Mlima (Uganda), Dk. Pindi Chana (Kenya) na  Dk. Edmund Kitokezi (Burundi).

Balozi wa kwanza kuzungumzia fursa hiyo, alikuwa Mangu ambaye alisema Rwanda ina fursa ya soko la mchele, makopa, ndizi na mahindi ambayo wananchi wake wanayatumia kama chakula cha mifugo.

Alisema kutokana na ufinyu wa ardhi nchini Rwanda, Watanzania waishio Mkoa wa Kagera wanatakiwa kuzitumia fursa hizo kwa kuuza biashara zao.

“Ndugu zangu tutumie fursa zilizopo Rwanda ili kutafuta fedha na kuwa na soko la bidhaa nilizozitaja, kuna soko kubwa la dagaa kutoka Ziwa Victoria, samaki ambavyo vyote kwetu vipo,” alisema Mangu.

Balozi Meela alisema wafanyabiashara wanapaswa kuchangamki fursa ya kupeleka bidhaa za viwandani kama chumvi, simenti na vifaa vya ujenzi nchini DRC ambavyo huko ni changamoto kuvipata.

“Nitumie nafasi hii kuwaomba wafanyabiashara kujenga tabia ya kutoka kutembea mkaone fursa zilizopo katika miji ya Kivu na Goma ili kujifunza jinsi watu wanavyofanya biashara na kupata mawazo mapya,” alisema Meela.

Balozi Chana alisema ili kufanikiwa katika biashara, mfanyabiashara anatakiwa kutumia mitandao ambayo inaweza kusaidia kupata taarifa ya bei ya bidhaa na wateja.

“Wafanyabiashara wa Kagera ili mfanye biashara katika masoko ya mipakani ambayo ni ya kimataifa, mnatakiwa kufuata taratibu za kuwa na vibali, sio kwenda tu, vinginevyo mtajikuta mnakwenda bora mmekwenda, tumieni mabalozi wa nchi husika ili msikwame,” alisema Chana.

Mapema, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti, alisema dhamira ya kuanziasha Wiki ya Kagera ni kuzitambua fursa zilizopo ambazo ni uvuvi, ufugaji, utalii, misitu, mipaka, viwanda na huduma za kijamii.

“Nina uhakika kupitia fursa zilizopo kwa mabalozi waliohudhuria hapa kutoka nchi tano, zitatambuliwa na wafanyabiashara waliopo Kagera ili kutafuta jinsi ya kuzifanyia kazi,” alisema Gaguti.

Wiki ya Kagera inatarajiwa kuzinduliwa rasmi leo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa viwanja vya Gymkhana, Manispaa ya Bukoba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles