27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MABADILIKO YA SHERIA KUWABANA ZAIDI WAUZA UNGA, TLS


ESTHER MBUSSI NA RAMADHAN HASSAN

DODOOMA

SERIKALI imewasilisha bungeni Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali unaopendekeza kufanyiwa marekebisho kwa sheria 13 ikiwamo Sheria ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), inayokusudia kumpatia Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) fursa ya kuangalia kama kanuni husika zimezingatia masharti ya sheria za nchi.

Pia katika marekebisho hayo, Sheria ya Kabidhi Wasii Mkuu wa Serikali, Kifungu cha 4, kinampoka Waziri wa Katiba na Sheria mamlaka ya kumteua Kabidhi Wasii Mkuu wa Serikali, badala yake imeweka masharti uteuzi huo ufanywe na Rais.

Akiwasilisha muswada huo bungeni jana, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, alisema madhumuni ya muswada huo ni kuimarisha utendaji wa taasisi za Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuondoa mwingiliano wa majukumu ya kitaasisi.

Alisema madhumuni mengine ni kuhuisha miundo ya baadhi ya taasisi ikiwamo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuleta tija na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi za Serikali lakini pia ili kuendana na mabadiliko ya sheria yaliyotokea katika sekta hiyo.

SHERIA YA TLS

Akizungumzia Sheria ya TLS, Profesa Kabudi, alisema katika marekebisho ya sheria hiyo pia vimewekwa vigezo vitakavyotumika kuwapata Wajumbe wa Baraza na taratibu za kufuatwa wakati wa utungaji wa kanuni zinazosimamia chama hicho.

“Sehemu ya 14 ya muswada wa marekebisho ya Sheria ya TLS, Sura ya 307, imeweka masharti ya kumtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuzipitisha kanuni zinazotungwa na Baraza la chama hicho kabla ya kuchapishwa katika Gazeti la Serikali,” alisema.

SHERIA YA MAKOSA YA JINAI, DAWA ZA KULEVYA

Katika sheria hiyo, Profesa Kabudi, alisema inapendekezwa Kifungu cha 57, Sura ya 20 ya Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, kuongeza masharti yatakayowezesha wapelelezi na wachunguzi kufanya mahojiano kwa kutumia vifaa vya sauti au vya kidijitali na Jaji Mkuu atatunga kanuni kwa ajili ya utekelezaji bora wa masharti hayo.

“Kifungu cha 188 cha Sheria ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya ya mwaka 2015, kinarekebishwa kwa lengo la kuainisha masharti yanayotoa ulinzi kwa mashahidi wanaoitwa kutoa ushahidi wao mahakamani, iwapo Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), atafungua maombi kwa ajili hiyo.

“Ulinzi unaotajwa kwa sasa katika sheria hiyo ya sasa unahusu kutotaja majina yao katika magazeti.

“Muswada unapendekeza pia kufanya marekebisho ya kifungu cha 205 cha sheria hiyo kwa kuongeza kifungu kipya cha 205A, kinachoainisha masharti kuhusu kupokelewa taarifa za wataalamu kama ushahidi mahakamani,” alisema.

Profesa Kabudi alisema katika sehemu ya tano ya muswada huo, inapendekezwa kurekebishwa kwa tafsiri ya maneno ‘Katibu Mkuu’ kwa kumwondoa Naibu Mwanasheria Mkuu kwa kuwa katika muundo wa awali alikuwa Katibu wa Wizara lakini kwa sasa Naibu Mwanasheria ni msaidizi wa AG.

“Sehemu ya Sita ya Muswada inapendekeza kurekebisha Sheria ya Ukomo Sura ya 89, kifungu cha 44, kinampatia waziri mwenye dhamana mamlaka ya kuongeza ukomo wa muda wa kufungua shauri mahakamani.

“Muswada unapendekeza kifungu hicho kirekebishwe kwa kuongeza masharti ambayo yatamwezesha waziri kutunga kanuni kwa ajili ya utekelezaji bora wa mamlaka ya kuongeza muda wa kufungua mashauri ya madai nje ya muda.

“Pia muswada unapendekeza kurekebisha kifungu cha 11 kwa kuweka utaratibu mbadala wa kuchukua maelezo ya shahidi kwa njia ya kiapo bila kulazimika maelezo hayo kuchukuliwa mbele ya mahakimu kama inavyoelekezwa katika kifungu cha 11 (2) cha sasa,” alisema.

Profesa Kabudi alisema, Serikali pia inapendekeza kuongeza vifungu vipya vya 38A, 38B na 38C, kwa lengo la kupokea maelezo na uthibitisho wa nyaraka za viapo ambapo kwa sasa sheria haina masharti kuhusu namna ya kupokea maelezo na ushahidi wa nyaraka na maelezo hayo yanaweza kutumika kama ushahidi katika mazingira ambayo shahidi aliye nje ya nchi hawezi kuja Tanzania kutoa ushahidi.

KAMBI YA UPINZANI

Akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mbunge wa Malindi, Ally Saleh (CUF), alisema Serikali imekuwa ikikiuka utaratibu wa utungwaji wa sheria kwa kuanza kutoa matamko na maelekezo na kisha unafuata utaratibu wa kisheria.

Alisema Serikali hutakiwa kufanya kazi zake kwa mujibu wa sheria, ibara ya 63 (3) (d) ya Katiba, inalipa Bunge mamlaka ya kutunga sheria na alihoji kama Serikali inatoa maelekezo kupitia kwa Rais au mawaziri na baada ya hapo kuleta muswada wa sheria kuhalalisha uamuzi na maelekezo ni ishara kuwa inapuuza mamlaka na hadhi ya Bunge.

“Mwaka 2016 akiwa katika mkutano mkuu wa CCM, Rais John Magufuli, alitangaza na kuelekeza Serikali kuhamia Makao Makuu Dodoma bila uwepo wa sheria.

“Pamoja na Kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba ya Bunge kuhoji jambo hilo, AG alitoa kauli kuwa jambo hilo linatakiwa kufanyiwa kazi na Ofisi ya Waziri Mkuu huku akijua yeye ni AG bila kujali wizara na idara,” alisema.

Akizungumzia marekebisho ya Sheria ya TLS, Saleh, alisema sheria hiyo inawanyima haki watumishi wa umma, madiwani, wabunge na viongozi wa vyama vya siasa kuwa wajumbe wa Baraza la Uongozi wa chama hicho.

Alisema ni jambo la kusikitisha kuwa Serikali inatunga sheria kwa kumlenga mtu au taasisi na haitungwi kwa malengo mahususi ya kuwasaidia wananchi.

MAONI YA KAMATI

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Katiba na Sheria, Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Damas Ndumbaro (CCM), alisema kamati imeshauriana na kukubaliana na Seriklai kuyafanyia kazi kwa wakati mwafaka maoni ya kuhuisha sheria ya TLS.

“Sheria ya TLS imeanza kutumika nchini tangu Januari Mosi, 1955 na tangu wakati huo haijafanyiwa maboresho ya msingi kuhusu malengo, muundo na mfumo wa uendeshaji wake hali inayosababisha changamoto zinazoonekana sasa kwa chama hicho kushindwa kuendana na zama zilizopo,” alisema Dk. Ndumbaro.

MUSWADA WASHINDWA KUPITA

Hata hivyo, muswada huo ulishindwa kupita kutokana na akidi ya wabunge kutotimia hatua iliyomlazimu Mwenyekiti wa Bunge, Najma Murtaza Giga, kuahirisha shughuli hiyo hadi keshokutwa (Jumatatu).

Hatua hiyo ilikuja wakati Bunge lilipoketi kama kamati ili kupitia vifungu vya muswada huo na marekebisho yake na kisha kuupitisha ndipo Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee, aliomba utaratibu kwa Najma kuhusu akidi ya wabunge kabla ya muswada kupigiwa kura.

Mdee alisema kwa kutumia kanuni ya 88 (10) 77 (3) kuhusiana na akidi ya vikao vya Bunge kwamba wanaenda kufanya uamuzi wa kupitisha muswada huo kifungu kwa kifungu na hatimaye kupitisha sheria lakini idadi ya wabunge wanaotakiwa kuipitisha ni wachache.

“Mwenyekiti kwa kutumia kanuni ya 88 (10), lakini vilevile na kanuni ya 77 kama ambavyo unaona, sasa hivi tunaingia katika kamati ya Bunge na tunaelekea kufanya uamuzi wa kupitisha kifungu kwa kifungu na hatimaye kupitisha sheria hii kwa ajili ya mabadiliko haya ya sheria mbalimbali.

“Sasa ndiyo kama vile unavyoona hapa, sihitaji kutumia nguvu nyingi kukushawishi, hili Bunge lina wabunge 393 na nusu ya akidi ni 193.

“Ka makadirio ya chini lakini tunaoenda kufanya uamuzi tupo 67, tumeshajihesabu, kwa hiyo kwa sababu kanuni inaturuhusu kupiga kura kwa kengele basi tupige kengele, tusubiri kama watu wapo nje basi waje na ikishindikana itabidi tuahirishe shughuli hii kwa leo (jana),” alisema Mdee.

Najma alisema suala hilo litatolewa uamuzi wakati wa kupiga kura na aliendelea kusoma vifungu vya sheria hiyo na kumaliza, hata hivyo, Mdee alisimama tena kumkumbusha suala la akidi kutotimia.

“Sasa nilikuwa naomba kiti chako kwa kutumia kanuni ya 77 utoe maelekezo kengele ipigwe kwa dakika tatu ili waliokuwa nje waje, lakini pia utoe maelekezo kwa makatibu wa Bunge watuhesabu ili kwa kumbukumbu za  Bunge tujulikane wangapi kisha maelekezo ya kanuni yafuate,” alisema.

MANYANYA ATAKA WAKATWE POSHO

Baada ya Mdee kusema hayo, Naibu Waziri  wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Manyanya, alitaka wabunge walioondoka katika mkutano huo wakatwe posho za siku hiyo.

“Kwanza leo siku ya ibada kuna wengine wameenda kusali vile vile inawezekana kuna wale wanaokuwa ni wazembe wa kuhudhuria bungeni kwa hiyo endapo utaridhia kwamba itahesabika ikaonekana hatutaweza kutosha, ukiwatoa wale ambao wamekwenda msikitini na walioomba udhuru basi wote wakatwe posho ya siku ya leo (jana),” alisema.

Najma aliamuru kupigwa kwa kengele ili kuita wabunge walioko nje na kusubiri kwa muda wa dakika tatu lakini walijitokeza wachache lakini hata hivyo hawakutimia.

Kutokana na hali hiyo, Giga alisimama  kuahirisha shughuli za bunge hadi Jumatatu.

“Dakika tatu zimeisha lakini naona kama wametimia au vipi? Wabunge kwa vile kazi zote kwa siku hii ya leo (jana) tumezimaliza imebaki kulihoji bunge naahirisha shughuli zote za Bunge hadi saa tatu asubuhi,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles