24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Maaskofu waungana na Ukawa

Tarcisius Ngalalekumtwa
Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Tarcisius Ngalalekumtwa

Na Raymond Minja, Iringa

BARAZA la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), limetoa tamko la kuwataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kujadili maoni yaliyoko kwenye Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Tarcisius Ngalalekumtwa, alisema wajumbe wa Bunge hilo wanatakiwa kujadili rasimu hiyo kwa kuwa imebeba maoni ya wananchi.

Tamko hilo la TEC linafanana na msimamo uliotolewa na wajumbe wanaotoka katika vyama vya upinzani wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), wanaotaka wajumbe wa Bunge hilo wajadili maoni yaliyoko kwenye rasimu na si vinginevyo.

Hata hivyo, msimamo huo unapingwa na wajumbe wengine wanaotoka CCM ambao wanataka mambo mengine yasiyokuwa katika rasimu hiyo yajadiliwe kwa masilahi ya taifa.

Katika mazungumzo yake jana kwa waandishi wa habari, Askofu Ngalalekumtwa alishangazwa na mwenendo wa Bunge la Katiba lililopita kwa kile alichosema kuwa wajumbe hawakuzingatia maoni ya rasimu.

“Bunge lililopita wajumbe walijadili maoni ya Katiba Mpya bila umoja kwa sababu walikuwa wakishambuliana kwa kauli kali, wakikashifiana bila kudhibitiwa na uongozi waliouchagua wenyewe.

“Mchakato huu wa Katiba umeliingiza taifa katika mgogoro mkubwa unaoashiria hatari mbeleni, kwa hiyo nawataka wayatendee haki maoni ya Watanzania walio wengi ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza hapo mbeleni.

“Kama Bunge litaendelea na malumbano yasiyokuwa na msingi kama Bunge lililopita, litaiingiza nchi katika matatizo na katika hili wananchi watawahukumu na kuwawajibisha kwa kukosa umakini katika jukumu walilokabidhiwa.

“Kwa moyo na sala na tafakari, tulifuatilia walivyojadiliana kuanzia mwezi Februari hadi Aprili 2014 na walijadiliana pasipo umoja kwani walishambuliana kwa kauli kali,” alisema.

Kutokana na hali hiyo alisema kwa sasa Watanzania hawataki kuendelea na Katiba ya mwaka 1977 kwani licha ya Katiba hiyo kuwa na kasoro, inaweza kuleta migogoro nchini.

“Watanzania wanahitaji Katiba inayoruhusu utawala wa sheria, haki sawa, manufaa na ustawi kwa wote na inayoheshimu utu wa kila mmoja huku ikizuia matumizi mabaya ya madaraka na ufisadi.

“Kwa sasa tunahitaji Katiba itakayowezesha ushiriki kamili wa watu katika maamuzi ya vipaumbele vya maendeleo yao na taifa.

“Tunataka Katiba shirikishi katika matumizi ya madaraka ili madaraka hayo yatumike kwa ajili ya kuwahudumia wote badala ya wachache,” alisema Askofu Ngalalekumtwa.

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

  1. Nadhani kuna waandishi wa habari walipotosha sana tamko la TEC la 01/07/2014, lililotolewa na Makamu wa Rais TEC mha. Niwemugizi. Haiwezekani kanisa libadili msimamo haraka hivi, kama kweli lilikuwa lipo kinyume na UKAWA.

  2. Waraka huu umetoa ujumbe tosha kwa chama tawala kinachojitahidi kupindisha maoni ya wananchi na kutetea misimamo yao isiyokuwa na maslahi kwa nchi na inayoashiria machafuko. Tafakari tu idadi ya wajumbe wa Katiba wengi ni kutoka CCM; Tafakari pia hotuba ya Raisi ya ufunguzi wa Bunge hilo; Usichoke tafakari pia Kanuni za upigaji kura jinsi zilivyolazimishwa ziwe za WAZI. Mwisho hebu chambua uwezo wa wajumbe hasa wa chama tawala katika uchambuzi wa mambo na utoaji wa hoja.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles