23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Maandamano yashika kasi Pakistan

islamabad, palestina

SHULE zimefungwa nchini Pakistan, huku barabara zikiwa tupu wakati makundi ya itikadi kali yakiendelea na maandamano ya kupinga uamuzi wa kuachiwa mwanamke wa Kikristo aliyehukumiwa kifo kwa kukashifu dini.

Polisi imesema wafuasi wa mhubiri wa Kiislamu mwenye msimamo mkali walifunga mojawapo ya barabara kuu za kuingia mji mkuu Islamabad, wakiwalazimisha wasafiri kutumia njia nyingine mbadala, huku watu wengi wakiamua kusalia majumbani ili kuepuka maandamano hayo.

Maandamano hayo yalizuka juzi baada ya jopo la majaji watatu kuamuru kuachiwa huru Asia Bibi, mwanamke wa Kikristo aliyehukumiwa kifo mwaka wa 2010. Uamuzi huo umesifiwa kuwa wa kihistoria na wanaharakati wa haki za binadamu.

Wafuasi wa vuguvugu la Tehreek-e-Labaik – TLP waliandamana katika miji yote na viongozi wake wakaapa kuendelea na maandamano yao.

Waziri Mkuu, Imran Khan, ametoa wito wa kuwepo utulivu na kuwaonya viongozi wa maandamano kupitia hotuba ya televisheni kwa taifa jana usiku, kutoishambulia serikali.

Serikali pia iliwapeleka wanajeshi katika miji mikubwa ili kuyalinda majengo ya serikali baada ya viongozi wa maandamano kuwataka majaji walioibatilisha hukumu dhidi ya Bibi wauawe.

Bibi alihukumiwa kifo na mahakama moja ya wilaya katika mkoa wa kati wa Punjab mwaka wa 2010, kwa madai ya kukashifu dini baada ya kuzuka mabishano na wanawake wawili wa Kiislamu walipokuwa wakifanya kazi shambani. Mahakama Kuu ya mji wa Lahore ikakubaliana na hukumu hiyo ya mwaka wa 2014 chini ya sheria tata za nchi hiyo kuhusu kukashifu dini.

Wakati huo huo, familia ya Bibi imesema mwanamke huyo wa Kikristo anapanga kuondoka nchini humo kwa kuhofia usalama wake. Bibi yuko mahali pasipojulikana, ambako mama huyo wa watoto watano aliye na umri wa miaka 54 anazuiliwa kwa sababu za kiusalama, akisubiri kuachiliwa huru rasmi.

Kaka yake, James Masih, ameliambia shirika la habari la AP kuwa dada yake ataondoka nchini humo hivi karibuni, lakini hakufichua nchi atakayohamia. Ufaransa na Uhispania zimejitolea kumpa hifadhi. Mume wake, Ashiq Masih, alikuwa amerejea kutoka Uingereza na watoto wao katikati ya mwezi Oktoba na anamsubiri ajiunge nao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles