31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Maalim Seif: Nitafia kwenye siasa

Na LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM

GWIJI la siasa za upinzani, Maalim Seif Sharif Hamad amesema hawezi kuacha siasa hadi hapo atakapofariki dunia.

Maalim Seif ambaye kwa sasa ni  Mshauri Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, hapo kabla akiwahi kuwa Katibu Mkuu huyo wa zamani wa Chama cha Wananchi (CUF) kabla ya kukihama chama hicho kutokana na migogoro ya kiuongozi, alitoa kauli hiyo katika mahojiano na kipindi cha Kokani kilichorushwa na kituo cha televisheni cha ITV juzi.

Mwanasiasa huyo ambaye pia amewahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar alisema kuwa yeye na siasa wameoana na kwamba mtu anapomuoa mkewe ni lazima utafika wakati watazikana.

“Mimi na siasa tumeoana, kwa hiyo unapomuoa mke wako mnakuwa pamoja unafika umri mpaka mzikane, kwa hiyo mimi kwenye siasa mpaka Mwenyezi Mungu achukue dhamana yake,” alisema Maalim Seif.

Katika hatua nyingine mwanasiasa huyo alisema miongoni mwa mambo anayoyajutia ni pamoja na kushindwa kuwaambia wananchi waandamane baada ya Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi nchini mwaka 1995, ili kushinikiza kutangazwa matokeo halali ya uchaguzi anaodai kuwa CUF ilishinda.

“Moja kwanza ninalojutia ni uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi Zanzibar ambapo CUF ilishinda ikawa siku tatu matokeo hayajatangazwa bado nikaona kwamba watakuwa waungwana hawa watatangaza ukweli.

“Lakini kwa kweli ningewaambia watu waingie barabarani siku ile basi wangetutangaza tu. Hilo najutia,” alisema Maalim Seif.

Maalim Seif amerejea kauli yake ya siku zote kwamba anaamini alishinda kwa sababu hata Kituo cha Televisheni cha DTV kilingaza matokeo hayo.

“Na mimi nakwambia wakati ule Mwalimu (Baba wa Taifa  Mwalimu Julius Kambarage Nyerere)  alikuwa anamfanyia kampeni Mkapa (Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa) Morogoro katika kikao cha wazee aliwaambia kwamba Zanzibar Seif kashinda, lakini yalikuwa cooked baadaye,” alisema Maalim Seif.

Jambo jingine ambalo alieleza kulijutia na ambalo pia amepata kusema huko nyuma wakati mgogoro wa kiuongozi CUF ukiwa umepamba moto ni kumwamini Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, licha ya kuonywa na wazee waliowataka kuwa makini dhidi yake.

“Tulipata maonyo kutoka kwa wazee kwamba huyu mtu mwangalieni vizuri lakini mimi bado nikaendelea kumwamini, sasa katufikisha hapa,” alisema Maalim Seif.

URAIS TANZANIA

Kuhusu kuwa na mpango wa kugombea urais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani alisema kuwa hajawahi kuwa na wazo hilo na kwamba yeye moyo wake ni kuiongoza Zanzibar.

Alipoulizwa ikiwa atagombea urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani alisema hawezi kulizungumzia suala hilo kwa sasa kwa sababu linahitaji kujipima kama bado wananchi wanamkubali pamoja na kushauriana na viongozi wa chama chake.

Kuhusu kupungua kwa upinzani visiwani Zanzibar baada ya yeye kuondoka CUF alisema kuwa watu waache kutafuna maneno kwa sababu kwa sasa chama kikuu cha upinzani katika visiwa hivyo ni ACT Wazalendo.

Mwanasiasa huyo alisisitiza kuwa hawezi kurejea CUF kwa sababu hata imani ya kiislamu inasema mwanamke ukimwacha kwa talaka tatu hupaswi kumrudia.

MGOGORO WAKE NA LIPUMBA

Kuhusu ugomvi wake na Profesa Lipumba alidai kuwa wakikutaka wanasalimiana na kuzungumza na tayari amesamehe yaliyopita.

Akizungumzia  hatua yake ya kujitangaza kuwa mshindi wa urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 alisema kuwa hajawahi kujitangaza mshindi na kwamba alichokifanya ni kuwaeleza waandishi wa habari kura walizozipata na kuitaka Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imtangaze mshindi.

Kuhusu hama hama ya wapinzani, Maalim Seif alieleza kutofurahishwa na tabia hiyo kwa sababu inaharibu taswira ya upinzani na kuwafanya wasiaminike.

“Kipindi hiki cha awapo ya tano, huu uhamaji hasa wa watu waliokuwa na vyeo upande wa upinzani inaonekana kuna jambo hapa linafanyika, inawezekana watu wanaahidiwa kwamba utakuwa hivi, utakuwa hivi.

“Tumeona wako waliohama walikuwa wabunge na wamehama vyama vyao bila sababu yoyote lakini baadaye uchaguzi uliporudiwa wakaahidiwa kwamba watakuwa wagombea na kweli wakawa wagombea.

“Na kweli CCM ikahakikisha wanapita kwa hali yoyote ile kwa hiyo hili lipo kwamba kwa namna fulani ushawihi unafanyika hivi, hilo nimeliona wazi wazi. Hili la pesa siwezi kusema kwa sababu mimi sina ushahidi wa wazi lakini hili la kuahidiwa lipo.

“Kwa mimi binafsi ninaonewa kusema nina uchu wa madaraka, kwa sababu mimi ningekuwa na uchu wa madaraka nilipohama CUF kuja ACT-Wazalendo ningesisitiza kuwa niwe kiongozi wa chama au niwe Katibu Mkuu wa chama, lakini kama unavyosema mwenyewe sisikiki kabisa. Kwa hiyo hilo mimi wananionea tu sina hata siku moja uchu wa madaraka.

Maalim Seif alisema kuwa baada ya kuhamia ACT walimuuliza wampe nafasi gani ya uongozi alikataa na kuwaambia kuwa popote watakapoona anaweza kuchangia atakubaliana nao.

Kuhusu hali ya siasa nchini kwa sasa alisema si nzuri kwa sababu siasa inahitaji watu wawe huru na vyama vya siasa vifanye kazi yake na kwamba kwa sasa vyama vyote vya siasa haviwezi kufanya mikutano ya hadhara wala maandamano mambo ambayo huviwezesha kutangaza sera na kutafuta uungwaji mkono.

“Sasa ikiwa nafasi hiyo huna hiyo siasa unafanyaje, kwa hiyo kwa sasa hakuna siasa katika nchi kwa sababu wakati mwingine imefika pahala mpaka vikao vya ndani vinaingiliwa,” alisema Maalim Seif.

Kuhusu uamuzi Mahakama Kuu wa kumtambua Profesa Lipumba kama mwenyekiti halali wa CUF alisema kuwa walikuwa wamejitayarisha kwa uamuzi wa aina yoyote.

“Hatukupata mshangao na wala hakuna mtu hata mmoja aliyeanguka kwa sababu ya maamuzi yale kila mtu alikuwa kajitayarisha kabisa,” alisema Maalim Seif. 

Alisema kuwa walijitayarisha kwa sababu katika masuala ya sheria unaweza kuhisi una haki lakini Mahakama ikaamua vinginevyo na kwamba wao wanaheshimu uamuzi wa mahakama.

Akizungumzia uamuzi wa wabunge ambao ni rafiki zake kuendelea kusalia CUF hata baada ya yeye kukihama chama hicho alisema wao wanaamini katika uhuru wa mtu kuamua na kwamba baada ya kuhamia ACT kulikuwa na tatizo hilo lakini walizungumza na wabunge hao kuona kama wako tayari kuacha ubunge na kuwafuata wao au watasalia CUF.

Pamoja na hayo mwanasiasa huyo mkongwe alisema kuwa uamuzi wa kuhama CUF umemwathiri na kwamba akisema kuwa haujaathiriwa atakuwa amesema uongo.

“Mtu anaweza kuwa na mke wake ambaye anampenda kwelikweli lakini Mwenyezi Mungu akamhitaji unavumilia, unakubali. 

“Kwa hiyo  acha chama hata mtu anaweza kuwa na mke wake ambaye wanaheshimiana wameishi kwa muda mrefu au mke ana mume wake wameishi maisha marefu lakini Mwenyezi Mungu akamchukua mmoja atasikitika lakini atabaki anavumilia na ataendela na maisha,” alisema Maalim Seif.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles