27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Maalim Seif kuweka rekodi ya kugombea urais 2020 ACT?

NA MARKUS MPANGALA

UAMUZI wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa muda mrefu wa Chama cha Wananchi  (CUF) Maalim Seif Sharrif Hamad, kuhamia chama kingine cha upinzani umeibua mjadala mkubwa nchini kote na kudhihirisha kuwa mwanasiasa huyo bado ni lulu kutokana na kuzoa wafuasi na wanachama wa chama chake cha zamani na kujiunga nao ACT-Wazalendo.

Maalim Seif amechukua uamuzi huo baada ya kuwa kwenye mgogoro wa uongozi na kisiasa dhidi ya Profesa Ibrahim Lipumba, na kutengeneza makundi mawili yaliyokuwa yakikinzana. 

Matokeo ya awali ya mgogoro wa CUF yalishuhudiwa  baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, chini ya Jaji Dk. Benhajj Masoud, Februari 18, mwaka huu kutengua uteuzi wa wajumbe wa bodi ya wadhamini wa Chama cha Wananchi (CUF) wa kambi ya Profesa Ibrahim Lipumba.

Wakati hatua hiyo ya mahakama ikivunja sehemu ya nguvu za kambi ya Profesa Lipumba, bado uliendelea na kuzidi kukidhoofisha chama chenyewe. Chama hicho pia kimekimbiwa na baadhi ya makada na viongozi wake, ambao wamekwenda kutafuta fursa za kisiasa ndani ya chama tawala CCM.

Miongoni mwa waliokihama chama hicho ni Julius Mtatiro (aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF kambi ya Maalim Seif Sharif Hamad), Maulid Mtulia (aliyekuwa mbunge wa chama hicho katika Jimbo la Kinondoni), Abdallah Mtolea (aliyekuwa Mbunge wake wa chama hicho katika jimbo la Temeke), na Zuberi Kuchauka (aliyekuwa Mbunge wa chama hicho katika Jimbo la Liwale mkoani Lindi).

Athari nyingine ya mgogoro huo ni wabunge 8 wa viti maalumu wa CUF na madiwani wawili wamepoteza nafasi zao kutokana na msuguano baina ya kambi hizo mbili zinazohasimiana. 

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa na diwani wa zamani wa chama tawala, kwa sharti la kutotajwa jina lake amesema, “Ni jambo rahisi kubaini kuwa chama cha ACT-Wazalendo kina fursa ya kuwa chama kikuu cha upinzani mwaka 2020. Hiki chama kinaweza kupata mtaji wa wabunge 18 wote kutoka majimbo ya visiwani Pemba na wengine wanne kutoka ngome za Maalim Seif. Kabla ya uchaguzi haujafanyika tayari ACT-Wazalendo kina wabunge 22 kutoka Zanzibar na wawakilishi katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar. 

“Historia inasema wazi kabisa, CCM haijawahi kupata mbunge katika majimbo ya Pemba tangu kurudishwa kwa mfumo wa siasa za vyama vingi mwaka 1992. Upinzani utapata anguko kubwa la wabunge wa majimbo Tanzania Bara. Hivyo kuifanya ACT ya Zitto Kabwe na Maalim Seif kuwa na mtaji wa majimbo ya Pemba. Sioni dalili za Chadema kufikisha majimbo 15 kwa Tanzania Bara katika uchaguzi ujao hivyo kuifanya ACT kuwa na uhakika wa nafasi za wabunge wengi bungeni,”

Maalim Seif ana nguvu kisiasa na ushawishi mkubwa katika pande hizo, ndiyo maana baadhi ya wanasiasa wanaendelea kumpigania na kuonyesha imani kubwa waliyonayo kwake. Mathalani, vyombo vya habari vimeripoti kuwa wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) jijini Tanga, kutoka Kata 27 na matawi 96, wamemfuata Maalim Seif.

Nguvu za Maalim Seif kisiasa visiwani zilichochea mabadiliko ya kikatiba ili kujenga mshikamano kati ya chama tawala na wapinzani, ambapo kulitengenezwa nafasi ya makamu wa kwanza wa rais (ambaye anatakiwa kutoka chama cha upinzani). 

Ingawa nafasi hiyo hivi sasa iko wazi, baada ya mgogoro wa kisiasa ulioibuka pindi CUF iliposusia kurudiwa kwa uchaguzi baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.

Katika chaguzi mbalimbali za mwaka 1995, 2000, 2005, 2010 na 2015 zinaonyesha kuwa kiongozi huyo ni hazina ndani ya chama hicho, hasa pale anavyojizolea kura kila uchaguzi.

Vilevile nguvu ya Maalim Seif inaonekana kwenye uongozi ndani ya chama kipya cha ACT -Wazalendo jinsi ambavyo viongozi waandamizi wanavyomfuata, huku maelfu ya wafuasi wake wakiungana kwenye chama hicho. 

Ushawishi wa Maalim Seif ulikolezwa zaidi tangu mwaka 1992 uliporejeshwa mfumo wa vyama vingi. Wanasiasa walioungana na Maalim Seif kwenye chama kipya cha ACT-Wazalendo ni pamoja na Chiku Aflah Abwao, Mansoor Yusuf Himid, Thomas Msasa, Nassor Mazrui, Sakina Dewji, Venance Msebo, Juma Duni Haji.

MAALIM SEIF KUKABIDHIWA JAHAZI LA URAIS 2020?

Jina la Maalim Seif Sharrif Hamad lina rekodi ya kipekee katika uchaguzi mkuu. Kiongozi huyo amegombea urais wa Zanzibar katika chaguzi za mwaka 1995, 2000, 2005, 2010 na 2015.

Maalim Seif ni mwanasiasa aliyegombea urais wa Zanzibar mara nyingi zaidi kuliko mwingine yeyote nchini. Hadi sasa amegombea urais wa Zanzibar mara 5, na iwapo mwaka 2020 kama atapitishwa itakuwa ni mara ya 6.

Safari ya Maalim Seif kugombea urais ilianza mwaka 1995 alipopambana na mgombea wa CCM, Salmin Amour. Kwa mujibu wa Tume ya uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) matokeo ya urais mwaka 1995, Salmin Amour alishinda kwa asilimia 50.24 dhidi ya 49.76 alizopata Maalim Seif. Hata hivyo, CUF ilitangaza kutoutambua ushindi huo.

Mwaka 2000, Seif aliingia ulingoni kupambana na Amani Abeid Karume, mtoto wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Karume. Kwa mara nyingine, matokeo ya ZEC yalionyesha Seif aliangushwa baada ya kujikusanyia asilimia 32.96 ya kura dhidi ya asilimia 67.04 alizopata Amani Karume. Uchaguzi wa mwaka 2000.

Hata hivyo, kumekuwa na malalamiko katika chaguzi hizo, baadhi ya waangalizi walisema haukukidhi vigezo vya kidemokrasia kutokana na wagombea kutoka vyama vya upinzani kutishwa na vyombo vya dola.

Waangalizi kutoka Jumuiya ya Madola walisema uchaguzi huo ulitawaliwa kwa kile walichokiita ‘uchafu mwingi’.

Vidonda vya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 vilijitokeza zaidi mwaka 2001, ambapo baadhi ya wafuasi wa CUF walipoteza maisha baada ya kushambuliwa na vyombo vya dola. Maandamano ya Januari 27, 2001, yalichangia kusainiwa kwa makubaliano ya pili ya amani baina ya pande mbili za CUF na CCM ili kuleta utulivu visiwani Zanzibar.

Uchaguzi wa mwaka 2005, CUF walimteua Maalim Seif kupambana tena na Amani Abeid Karume wa CCM. Uchaguzi huo ulipokamilika, ZEC ilimtangaza Amani Abeid Karume kuwa mshindi baada ya kujikusanyia asilimia 53.18, huku Seif Hamad akijipatia asilimia 46.07 ya kura zote.

Hata hivyo waangalizi wa kimataifa kwa mara nyingine, walisema kuwa uchaguzi huo haukuwa huru na haki. Taarifa ya waangalizi wa Jumuiya ya Madola walisema palikuwa na kasoro nyingi na uhaba wa uhuru miongoni mwa wapigakura na wagombea. CUF ilipinga matokeo hayo.

Maalim Seif alirudi tena kwenye kinyang’anyiro cha mwaka 2010 akiwakilisha CUF dhidi ya Dk. Ali Mohammed Shein wa CCM. Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, 2010, ZEC ilimtangaza Dk. Shein kuwa mshindi wa kiti cha urais wa Zanzibar kwa kupata asilimia 50.1 dhidi ya 49.1 za Maalim Seif.

Kutokana na makubaliano ya vyama hivyo kumaliza mgogoro wa muda mrefu visiwani humo, Maalim Seif alitakiwa kuwa sehemu ya Serikali, aliteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, huku Balozi Seif Ali Iddi akiwa Makamu wa Pili wa Rais.

Matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 yalifutwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na Mwenyekiti wake Jecha Salum Jecha. ZEC ilitangaza pia uchaguzi wa marudio utafanywa Machi 20, mwaka uliofuata.

Licha ya kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi huo, Maalim Seif aliitisha mkutano wa waandishi wa habari Oktoba, 2015 na kusema kuwa yeye ndiye mshindi wa kiti cha urais Zanzibar na alikataa kushiriki uchaguzi wowote wa marudio.

Huu ni ushahidi wa wazi kuwa Maalim Seif anazo nguvu za kisiasa kuanzia visiwani Zanzibar ambavyo vitamwezesha kukiuza chama chake kipya alichohamia ACT-Wazalendo.

Ndiyo maana, kila uchaguzi unapowadia, matokeo rasmi yanayonyesha imani ya wafuasi na wanachama wanamuunga mkono Maalim Seif. Wanaonekana kuamini kuwa kiongozi huyo kuwa na uwezo wa kuongoza Zanzibar. Kwa hiyo matumaini na mategemeo hayo ndiyo chanzo cha Maalim Seif kuwa jabali la kisiasa visiwani Zanzibar hadi leo, jambo ambalo ni faida kwa ACT-Wazalendo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles