27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Maalim Seif: Kuna vitisho Zanzibar

Pg 1Na Agatha Charles

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar (SUK), Maalim Seif Sharif Hamad, amesema hali ya kisiasa visiwani humo si shwari, kutokana na wananchi kuishi maisha ya wasiwasi wa kushambuliwa na mazombi.

Amesema baada ya kutangazwa kwa uchaguzi mkuu wa marudio, wananchi wa Zanzibar na hasa wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF), wanadharauliwa, wanapigwa na kuvunjiwa maduka yao.

Kauli hiyo imetolewa jana na Maalim Seif, alipokutana na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ofisini kwake, Mikocheni, Dar es Salaam, ili kujadili juu ya hali ya nchi pamoja na kushauriana namna ya kusaidiana.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano wake na Lowassa, Maalim Seif alisema yapo madai kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imewataka wafanyakazi wa umma kupeleka vitambulisho vyao ili viingizwe kwenye kumbukumbu kwa lengo la kuwabaini ambao hawatapiga kura ya marudio hapo Machi 20.

Akiwa sambamba na Lowassa mbele ya waandishi wa habari, alisema Serikali ya Zanzibar inawatisha wananchi ili wawe waoga na hivyo wapige kura kwa lazima, hasa watumishi wa umma.

“Serikali ya Zanzibar inafanya vitisho, imeagiza watumishi wa serikali wapeleke vitambulisho vya makazi na vya kura ili viwekewe kumbukumbu ili tarehe 20 vijue nani kapiga na nani hajapiga. Si mara ya kwanza, huko nyuma iliwahi kutokea na wafanyakazi wa umma ambao hawakupiga kura walifukuzwa,” alisema Maalim Seif.

Alisema walitarajia kuwa baada ya kutangaza kujitoa katika kinyang’anyiro hicho, CCM wangeendelea na mambo yao ili kupata ushindi wa asilimia 99 au hata 100 ili kuunda serikali waitakayo.

Jambo jingine ambalo Maalim Seif alisema linatokea Zanzibar ni kile alichokiita hujuma kutoka katika kikundi cha watu wanaovaa soksi kufunika nyuso zao kupiga watu pamoja na kupora katika maeneo mbalimbali ambayo yana wafuasi wengi wa CUF.

“Kuna kikundi cha watu wanavaa soksi na kupiga watu, Michenzani walivunja vitu, kuna sehemu inaitwa Msumbiji ambayo kuna CUF wengi wakavunja maduka na mabao, Jang’ombe wakavunja vitu wakapiga watu, Polisi wapo lakini hawachukui hatua, wanajidai kushangaa,” alisema Maalim Seif.

Alisema iwapo matukio hayo yangekuwa yakifanywa na wafuasi wa CUF, vyombo vya Dola vingeshughulika.

“Ni jambo la kusikitisha kuona dola inashiriki kutisha watu, tulishasema sana kuwa hatushiriki uchaguzi, ‘why watu- harass’,” alisema Maalim Seif.

Alisema kutokana na hali hiyo, aliwahi kuwaarifu Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, ambao walimjibu kuwa hawana taarifa za watu kupigwa.

Alisema hayo yanatokea akiwa bado ana nafasi ya kumfikia kwa urahisi Rais na Makamu wake ili hatua zichukuliwe, vinginevyo hali ingekuwa mbaya.

“Mimi ni Makamu wa Kwanza in bracket (mabano) kwa kuwa muda ulishaisha, nilijaribu kuongea na vyombo vya dola Polisi, kuna mmoja niliwahi kumwita akajibu niandike kupitia kwa Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, hilo haliwezekani, protocol (itifaki) haiko hivyo,” alisem Maalim Seif.

Aliwataka wafuasi wa chama hicho kutokubali kuchokozeka kwa kuwa kuna sababu inatafutwa, hivyo wawe wavumilivu.

Maalim Seif alisema miezi michache nyuma kuna mabomu yalitegwa katika maeneo tofauti ya Mkunazini na Michenzani, lakini alishangaa Polisi kufika haraka kabla ya hayajalipuka na kuyategua.

Alisema anashangazwa na hali hiyo, huku kukiwa na ukimya wa waliohusika kuyatega mabomu hayo kutokana na maeneo hayo kuwa na kamera zinazorekodi kila kitu.

“Kuna kamera za ‘billion’s of money’ na zina uwezo mkubwa, sasa mabomu yanategwa chini ya kamera na watu hawajulikani,” alisema Maalim Seif.

Nafasi ya mazungumzo

Maalim Seif alisema bado kuna nafasi ya mazungumzo baina yao na upande wa Serikali ili mgogoro wa Zanzibar umalizike kwa amani.

Akijibu swali la waandishi wa habari kuhusu kutafuta suluhu kwa kushirikisha viongozi kutoka nje, Maalim Seif alisema hilo litafanikiwa iwapo CCM kitasitisha uchaguzi.

“Ndani ya Zanzibar tumekwama, najua watu wanapanua wigo kwamba tuingize watu kutoka Bara, sidhani kama kuna mazungumzo ikiwa wenzetu wanaendelea na uchaguzi. Sisi tupo tayari kufanya mazungumzo ikiwa wataacha uchaguzi,” alisema Maalim Seif.

Alisema upande wa CUF na hasa yeye mwenyewe hawana ajenda ya kulipiza kisasi, hivyo hajui kinachosababisha hofu kwa CCM kumkabidhi madaraka.

Alisema baraza linajengwa na vyama viwili, kwamba hata uchaguzi uliopita CCM kilipata viti 27 na CUF viti 27, hivyo wangekuwa sawa sawa.

Akijibu kuhusu karatasi za kupigia kura kuwa huenda zikawa na majina ya wagombea wa chama chao, Maalim alisema tayari walishaithibitishia Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kuwa hawatashiriki kwa kuiandikia barua.

Alisema mwisho wa uthibitisho ulikuwa jana na CUF kiliandika tangu Jumanne ya wiki hii kikithibitisha kuwa hakishiriki kuanzia ngazi ya diwani, ubunge na urais, hata kama walikuwa wameshinda.

Naye Waziri Mkuu wa zamani, Lowassa alisema kuna utaratibu wa kuachiana baada ya miaka mitano kwa mtu anayeshinda, lakini anashangaa kwa nini hawamruhusu Maalim.

Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar ulifutwa mwaka jana na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha, kutokana na madai ya kuwepo kasoro nyingi, ikiwemo baadhi ya wagombea kujitangazia matokeo.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles