30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Maalim Seif ‘apiga hodi’ ACT Wazalendo

ANDREW MSECHU

-DAR ES SALAAM

KAMATI Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo, imekutana Dar es Salaam huku mjadala wa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ukitawala katika kikao hicho.

Hatua hiyo inatokana na kuwepo kwa taarifa za ndani ya chama hicho kukutana na kuweka mkakati wa namna ya kumshawishi Maalim Seif ili kujiunga nao.

Taarifa za ndani zinaeleza hatua ya kukutana kikao hicho inatokana na uamuzi wa Profesa Ibrahim Lipumba kuitisha mkutano wa uchaguzi huku taarifa za kung’olewa Maalim Seif ndani ya CUF zikitawala.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya ACT Wazalendo, kiliiambia MTANZANIA jana kuwa Maalim Seif au mwakilishi wake alialikwa kushiriki kikao hicho ili kujadili kwa pamoja namna bora ya hatima ya kiongozi huyo, hasa baada ya uchaguzi wa Lipumba ambaye amechaguliwa tena na hatima ya kesi zilizopo mahakamani.

“Ni kweli Maalim Seif amepewa taarifa za kikao hiki na amealikwa, lakini sijui kama atakuja yeye au mwakilishi wake.

“Lakini kubwa amekuwa akitakiwa na vyama viwili vya upinzani ikiwamo ACT ambapo kila kimoja kinajaribu kuweka ushawishi wake kwa kiongozi huyo aweze kujiunga nacho. Tunasubiri hatima yake na nini atakachoamua,” alisema mtoa taarifa huyo.

Akizungumza jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, alisema miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa na kikao hicho ni pamoja na suala la CUF.

“Ukweli ni kwamba tunafuatilia kwa karibu sana yanayoendelea ndani ya Chama cha CUF.

“CUF ni chama kamili chenye katiba yake ambayo ni lazima iheshimiwe. Pia kina vikao vyake vinavyokaa kwa mujibu wa katiba ambavyo lazima viheshimiwe, sisi tunahitaji kuona katiba inaheshimiwa na sheria za nchi pia zinaheshimiwa. Ila kishindo kikubwa kinakuja.

“Sisi ACT Wazalendo tupo na tunasimama upande wa haki, kwahiyo hatuwezi kukubaliana na upande unaokwenda kinyume na haki.

“Tunafuatilia yanayoendelea kwa mkutano uliomalizika wa Ibrahim Lipumba. Zaidi, tunasubiri uamuzi wa mahakama unaotarajiwa kutolewa Machi 18 ili kuweka wazi msimamo wetu,” alisema Shaibu.

Alisema pamoja na mambo yote yanayoendelea ndani ya CUF ambayo kwa sasa imegawanyika katika pande mbili, yaani CUF Maalim na CUF Lipumba, Kamati Kuu ya chama hicho itakayomaliza kikao chake leo, itajadili kwa kina suala hilo na kutoa rasmi mwelekeo wake.

Akizungumzia agenda nyingine za kikao hicho cha Kamati Kuu, Shaibu alisema zipo za kitaifa na za kichama, kwamba wataangalia mweneneo wa nchi kisiasa na kiuchumi katika robo ya kwanza ya mwaka huu na pia kuangalia viporo walivyovuka navyo mwaka jana.

MTANZANIA ilipomtafuta Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma upande wa Maalim Seif, Mbarala Maharagande alijibu kwa ufupi ‘si kweli’.

Naye Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma, upande wa Maalim Seif, Salim Bimani, alisema hana taarifa za mwaliko huo wala kutumwa mwakilishi.

“Mimi sina taarifa yoyote na tunapozungumza hapa sasa hivi Maalim Seif yuko hapa ofisini,” alisema Bimani.

Chama cha CUF kimekuwa katika mvutano wa pande mbili, wa kwanza ukiwa wa Mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Lipumba na wa pili wa katibu anayetambuliwa na vikao halali vya chama hicho, Maalim Seif.

Mvutano huo ulianza baada ya Profesa Lipumba ambaye alitangaza kujiuzulu uenyekiti Julai 2015 ikiwa ni hatua ya kupinga uteuzi wa aliyekuwa mgombea urais wa Chadema kupitia Ukawa, Edward Lowassa, kisha kurejea katika chama chake mwaka mmoja baadaye akidai kuwa yeye bado ni mwenyekiti halali.

Jana Profesa Lipumba alisema kwa muda mrefu amemvumilia Maalim Seif, lakini sasa imefika mwisho.

Juzi na jana wajumbe wa mkutano mkuu walikuwa wanaendelea na uchaguzi wa wajumbe wa Baraza Kuu kwa kanda na leo katibu mpya anatarajiwa kutangazwa huku aliyekuwa Mbunge wa Gando, Khalifa Suleiman Khalifa, Mussa Haji Kombo na Haroub Mohammed Shamisi majina yao yakitajwa huenda mmoja wao akabeba mikoba ya Maalim Seif.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles