24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Maalim Seif amfungia milango Dk. Shein

cc*Asema hana muda wa kukutana naye

* Baraza Kuu la CUF latoa maazimio 13

 

NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amesema hayuko tayari tena kukutana na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein kwa ajili ya mazungumzo ya kutafuta mwafaka.

Kauli hiyo aliitoa jana mjini Unguja, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kutangazwa kwa maazimio 13 ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho, kilichokutana kuanzia Aprili 2, mwaka huu.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kujua kama atakwenda Ikulu pindi akiitwa na Dk. Shein kwa ajili ya mazungumzo ya kutafuta mwafaka, Maalim Seif aliweka wazi kwamba hana haja ya kufanya hivyo kwani tangu awali kiongozi huyo hakuwa na nia njema na suala la Zanzibar.

“Siko tayari kukutana na Shein, kama nani na nazungumza nini nikikutana na Dk. Shein Ikulu? Labda kama nitakutana naye kwa njia nyingine sawa za kibinaadamu, lakini hatuko tayari tena kuzungumza na Shein,” alisisitiza Maalim Seif.

Alisema haoni uwezekano wa Serikali ya Dk. Shein kuendelea kuwapo madarakani hadi ifikapo 2020 na hilo linatokana na msukumo wa nchi wafadhili kusita kutoa misaada katika baadhi ya miradi waliyoahidi kwa Tanzania.

“Uwezekano wa Serikali hii kuendelea hadi 2020 siuoni kutokana na presha hii  ya jumuiya za Kimataifa,” alisema Maalim Seif.

 

MATIBABU YAKE

Akizungumzia mjadala wa malipo ya matibabu yake ya hivi  karibuni kufanywa na Serikali alipokwenda nchini India kutibiwa na baadaye kulazwa katika Hospitali ya Hindu Mandal jijini Dar es Salaam, Maalim Seif alisema anazo stahiki zote kulipiwa matibabu na Serikali ya Zanzibar kwa vile ni Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Alisema wakati anajiandaa kwenda nchini India kwa matibabu, alimwandikia barua Rais wa Zanzibar, Dk. Shein kumpa taarifa ya safari yake hiyo na kuongeza akiwa kwenye matibabu alishangazwa kusikia Serikali imebeba mzigo wa matibabu yake.

“Nilipokwenda India kutibiwa, chama kilitaka kubeba mzigo wa matibabu yangu, lakini kwa vile ile Serikali ya Kitaifa ilikuwa bado ipo, nikaamwandikia Dk. Shein kumpa taarifa ya safari yangu.

“Kesho yake nikaenda kutibiwa, sijui ikawaje wakasema nitatibiwa na Serikali, nikaambiwa nalipiwa matibabu, lakini nina stahiki zangu, hata gari ninayotumia ni ya Serikali,” alisema Maalim Seif.

 

UKARIBU WAKE NA VIONGOZI

Maalim Seif pia aliwatoa wasiwasi wanachama na wafuasi wa chama chake kuhusu ukaribu wa viongozi wa Serikali walioonyesha alipokuwa mgonjwa.

Alisema kuwa hafikirii kama Wazanzibari watakuwa na wasiwasi na ukaribu wake na viongozi wa Serikali kwani ulikuwa ni wakati ule wa mazungumzo ya kutafuta mwafaka baada ya kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015 na si vinginevyo.

Maalim Seif aliongeza kuwa hata alipokuwa mgonjwa viongozi hao walikwenda kumjulia hali na kumtakia apone haraka na kusisitiza katika hali halisi asingeweza kulikwepa jambo hilo.

“Kama ukaribu ni wakati ule tulipokuwa na mazungumzo yakavunjika, sina uhusiano nao tena. Nilipoumwa viongozi kadhaa walijitokeza na sidhani kama huo ndio ukaribu, kiongozi anapiga simu niko njiani nakuja kukuangalia na akifika tunazungumza hali ya afya yangu na kunitakia heri. Ni ile hali ya ubinadamu.

“Tutake tusitake mimi ni kiongozi, nikiumwa, nikifiwa ni jambo la kawaida tunafanya kila siku, tukiacha hizi siasa siuoni ukaribu na viongozi wa Serikali,” alisema Maalim Seif.

 

USHAURI WA MADAKTARI

Maalim Seif pia alizungumzia ushauri wa madaktari wake, akikiri kuwa wamemtaka atumie muda mwingi kupumzika na kusema anaendelea kuufuata.

Kwa mujibu wa Maalim, madaktari wamesisitiza apumzike sana, lakini hawakumshauri kupumzika kitandani katika muda wote.

“Ni kweli madaktari wamesisitiza nipumzike sana, hawakusema nilale wakati wote, wamenipa masharti nisikae kitako, nitembee na nisimame, hata vikao hivi vya juzi nilikuwa nasimama au natembea,” alisisitiza Maalim Seif.

 

KUTOMTAMBUA DK. SHEIN

Akizungumzia hatua ya chama chake kutomtambua Dk. Shein na Serikali yake, Maalim Seif alisema hawakuzuka katika kufikia uamuzi huo na kusisitiza kuwa tangu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya Uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana walitangaza kutotambua hatua hiyo.

“Tangu alipofuta Jecha uchaguzi tukasema haukuwa halali, tulisema waziwazi hatutambui uchaguzi wa marudio wa Machi 20 na wananchi waliitikia.

“Kama Rais katokana na mchakato huo huo ambao hatuutambui kwa kuwa ni haramu, hatuitambui na Serikali yake,” alisema Maalim Seif.

 

MAAZIMO YA BARAZA KUU

Awali Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa CUF, Dk. Twaha Taslima, alisoma maazimio 13 yaliyofikiwa na Baraza Kuu la Uongozi wa chama hicho, ambapo miongoni mwao ni kuwataka wananchi kutumia njia za amani, kikatiba na kisheria zilizowahi kutumika katika nchi nyingine duniani kuwakataa watawala wasio na ridhaa yao.

Pia baraza hilo limefurahishwa na hatua ya zaidi ya asilimia 80 ya wananchi kutojitokeza kushiriki uchaguzi wa marudio wa Machi 20, mwaka huu.

Pamoja na hali hiyo, baraza hilo limewapongeza wagombea wa nafasi zote kwa kutoshiriki uchaguzi huo licha ya ZEC kulazimisha na kusisitiza hatua hiyo imeonyesha kuwa viongozi hao hawajali nafasi na vyeo binafsi bali wanachotaka ni mabadiliko ya kweli kwa masilahi ya Wazanzibari.

Baraza hilo pia limesisitiza kuutambua Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana na matokeo yake yaliyoonyesha chaguo la Wazanzibari ni CUF na Maalim Seif ndiyo chaguo la kuiongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Kutokana na hali hiyo, Baraza Kuu la Uongozi limezishukuru jumuiya za kimataifa na taasisi za kitaifa na kimataifa na nchi rafiki za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zilizokataa kuleta waangalizi wa uchaguzi wa marudio.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles