28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Maajabu uchaguzi Serikali za Mitaa

Pg 1....

Na Waandishi Wetu, Dar na Mwanza

HAYA ni maajabu. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya wapiga katika kituo cha Shule ya Msingi Mwenge, Kinondoni jijini Dar es Salaam kufika kituoni na kukuta majina yao yakionyesha tayari wamepiga kura.
Hali hiyo, ilisababisha kuibuka vurugu kubwa ambazo zilisababisha upigaji kura katika uchaguzi huo wa marudio, kusitishwa kwa muda.
Msimamizi wa uchaguzi katika kituo hicho, Nasoro Kichuma alisema uchaguzi huo ulianza vizuri, lakini kadrii muda ulivyozidi kwenda wapiga kura wengi walishangazwa namna majina yao yalivyotumiwa na watu wasiofahamika.
“Ni jambo la kushangaza kuona mtu anafika kituoni kupiga kura halafu anakuta jina lake limetumiwa, yaani inaonesha tayari amekwishapiga kura … hali hii inazidisha wananchi kuwa na hasira na kushindwa kutumia haki yao ya msingi ya kidemokrasia kuchagua viongozi wanaowataka,”alisema Kichuma.
Mbali ya tukio hilo, hali ilikuwa mbaya zaidi katika vituo vya Ali Maua, Kata ya Kijitonyama na Kituo cha Mnyamani Buguruni, ambako eneo hilo liligeuka uwanja wa masumbwi kati ya wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF).
Watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa CCM, walipigana ngumi kavu kavu na vijana wanaodaiwa kutoka CUF kwa kile kilichodaiwa kuwa wapiga kura wengi waliofika kituoni hapo ni mamluki.
Msimamizi wa uchaguzi Kituo cha Mnyamani-Burguruni, Jumanne Muhanji alisema tangu kufunguliwa kwa kituo hicho asubuhi wafuasi walikuwa wakilumbana.
Alisema baada ya hali kuwa mbaya zaidi, polisi walilazimika kuingilia katika kutuliza hali hiyo.

KITUO CHA ALI MAUA
Katika kituo hicho, vurugu zilitawala baada ya watu 30 wanaodhaniwa kuwa mamluki wa CCM kufika kwa ajili ya kupiga kura.
Msimamizi msaidizi wa kituo hicho, Abdalah Mkenge alisema uchaguzi ulianza vizuri asubuhi kwa kuweka utaratibu mpya wa namba tofauti na uchaguzi uliopita wa kusoma majina.
Alisema licha ya kutumika utaratibu huo, bado changamoto ya mamluki ilijitokeza kwani wengi wao walidaiwa kufika kituoni hapo wakiwa katika gari aina ya Noah, kitendo kilichoamsha hasira kutoka kwa wafuasi wa CUF.
Hali hiyo, ilitulizwa baada ya polisi waliokuwa na silaha na mabomu ya machozi kufika.
Hali ya usalama katika kituo cha vingunguti ilionekana kuwa tulivu, baada ya polisi wengi kuonekana eneo hilo.
Hali ya kutoaminiana kwa wapiga kura ilitawala, huku wengi wakishindwa kuona majina yao kwenye ubao wa matangazo.
Katika kituo cha Misewe, uchaguzi uliendelea vizuri huku wapiga kura wakionekana kuwa watulivu.
Msimamizi wa uchaguzi msaidizi,Rose Masondole alisema kuwapo wapiga kura bado mpaka mchana walikuwa wamepokea kesi tisa.
Katika kituo cha Mbuyuni, alisema wagombea wa nafasi ya mwenyekiti walifika kituo hapo wakiwa na madaftari ya wapigakura
Msimamizi wa uchaguzi kwenye kituo hicho,Ibrahim Mabewa alisema kitendo hicho kilisababisha mvurugano mkubwa.
Katika kituo cha Kinondoni Mjini, wananchi walilazimika kupigia kura katika eneo la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).
Hali hiyo, ilitokana na kituo chao cha awali kuhamishwa baada ya kutokea vurugu zilizo daiwa kusababishwa na mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa CCM.

MWANZA

Taarifa kutoka mkoani Mwanza, zinasema uchaguzi wa Mtaa wa Ibungilo ‘B’ Kata ya Nyamanoro uliotarajiwa kufanyika jana ulikumbwa na miujiza.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, Justine Lukaza na Ofisa Mtendaji wa kata ya Nyamanoro wakiwa na askari polisi walibandika matokeo ya uchaguzi uliofanyika Desemba 14, mwaka huu.
Matokeo hayo yanaonyesha mgombea wa CCM, Christopher Mugeta kuwa mshindi kwa kupata kura 448 dhidi ya Ramadhan Said wa Chadema ambaye alipata kura 321 kati ya kura 769 zilizopigwa.
Kutokana na hatua hiyo, Mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia (Chadema) naye amemsimika Said kuwa ndiye mwenyekiti wa mtaa huo akipinga matokeo hayo kwa vile walikubaliana uchaguzi kurudiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kiwia alisema wameamua kumsimika Said baada ya viongozi wa kata ya Nyamanoro na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kukiuka makubaliano waliyofikia wiki iliyopta.
“Mara nyingi tunapopigania haki zetu tumekuwa tukionekana watu wenye vurugu, angalia kitendo cha kubandika matokeo ya Desemba 14, mwaka huu ambayo yalivurugika baada ya kura kuzidi na kumlazimu mtendaji wa kata kuahirisha uchaguzi huo hadi Desemba 21, mwaka huu..kitendo hiki kinaonyesha utumiaji wa nguvu, tutakipinga kwa nguvu zote,” alisema.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela, Lukaza alikanusha kuwapo kwa dosari katika uchaguzi wa Desemba 14.
Alisema matokeo ya uchaguzi huo yaliahirishwa kutangazwa kutokana na wafuasi wa CCM kufanyiwa vurugu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles