27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Maafa zaidi ya corona barani Afrika

NAIROBI, KENYA

SERIKALI ya Kenya imesema kuwa itatuma ndege ya Kenya Airways nchini China kesho Jumatano kwa ajili ya kuchukua vifaa vya kupambana na ugonjwa wa Covid-19, wakati maambukizi nchini humo yakiwa yamefikia zaidi ya 142.

Waziri wa Usafirishaji wa Kenya, James Macharia alithibitisha habari hiyo na kusema kuwa, vifaa hivyo vitatumika kuzuia njia za kuenea kwa maambukizi ya corona.

Waziri Macharia alitoa taarifa hiyo wakati akitangaza kuongezwa muda wa marufuku ya ndege za kigeni kuingia nchini Kenya kwa muda wa siku 30 nyingine.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ndege za mizigo tu na zile za kuhamisha raia wa kigeni ndizo zitakazoendelea kufanya kazi.

Huku hayo yakiripotiwa, Kenya imethibitisha kuwa na wagonjwa wapya 16 wa corona, baada ya kuwafanyia vipimo watu 530. Hadi sasa Kenya imefikisha idadi ya watu 142 wenye maambukizi ya Covid-19.

Juzi, Wizara ya Afya ya Kenya ilitangaza kuwa katika kesi mpya 16 za maambukizi ya corona nchini humo, miongoni mwao ni raia wa Kenya ni 15 na mmoja ni raia wa Nigeria.

Taarifa hiyo ya wizara ilieleza kuwa raia 11 kati ya hao wana historia ya kusafiri nje ya nchi na watano kati yao wameambukizwa wakiwa ndani ya Kenya.

Watu 12 ni kutoka mji mkuu wa Kenya, Nairobi, wengine watatu wanaishi Mombasa na mmoja ni kutoka Kilifi. Waliokutwa na maambukizi mapya ni wennye umri kati ya miaka 22 na 66, wanaume ni tisa na wanawake saba.

Vile vile Wizara ya Afya ya Kenya ilisema kuwa inatengeneza barakoa (maski) ambazo zitasambazwa kwa wananchi hivi karibuni.

Pia ilisema watu watakaokufa kwa corona watazikwa ndani ya masaa 24. Watu wa karibu wa familia wasiozidi 15 ndio wataruhusiwa kuhudhuria mazishi hayo yatakayosimamiwa na Serikali.

WAPINZANI UGANDA WAILAUMU SERIKALI

Nchini Uganda, wapinzani wameilaumu Serikali ya Rais Yoweri Museveni kwa kushindwa kudhibiti maambukizi ya corona nchini humo kama ambavyo wamesisitiza kuwa chakula kinachotolewa na Serikali kuwasaidia waathirika wa corona hakitoshi.

Televisheni ya France 24 iliripoti habari hiyo na kumnukuu Waziri Mkuu wa Uganda, Ruhakana Rugunda akijibu malalamiko hayo ya wapinzani akisema, hatua hiyo ya Serikali ni kwa ajili ya kuwasaidia  watu wenye shida zaidi tu si kwa ajili ya kila muathiriwa wa corona.

Ugawaji chakula ili kukabiliana na madhara ya kiuchumi na kijamii ya waathiriwa wa corona ulianza wiki mbili zilizopita nchini Uganda. Ulifanyika katika mji mkuu Kampala na maeneo mengine ya Uganda kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa corona. Hata hivyo wapinzani wanasema chakula kinachotolewa ni kidogo sana na hakikidhi haja.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa zamani aliyeongoza serikali ya mpito nchini Libya, Mahmoud Jibril,  amefariki dunia kwa ugonjwa wa Covid-19 yaani corona.

Ilielezwa jana kuwa kuwa Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Libya aliyeongoza mapinduzi yaliyong’oa madarakani Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011 alilazwa katika hospitali moja mjini Cairo, Misri baada ya kupata mshtuko wa moyo na siku tatu baadaye, aligundulika kuwa na ugonjwa wa Covid-19 na kuwekwa karantini.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Ganzouri iliyopo mjini Cairo, Hisham Wagdy, alisema Jibril alifikishwa hospitalini hapo Machi 21, 2020 na alithibitishwa kuwa na corona siku chache baadaye.

Habari hiyo imethibitishwa pia na msaidizi wa Mahmoud Jabril katika chama chake, yaani Fawzi Ammar ambaye alisema kuwa, Jibril alifariki dunia katika hospitali moja binafsi mjini Cairo, Misri alikokuwa anatibiwa tangu mwezi uliopita.

JOHNSON BADO YUKO HOSPITALINI

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson pia ameendelea kuwepo hospitali usiku mzima wa kuamkia jana baada ya kufikishwa hapo juzi kufanyiwa uchunguzi kutokana na dalili za virusi vya corona ambazo hazijaisha, siku 10 baada ya kutambulika kuwa na virusi hivyo.

Kiongozi huyo alitangaza Machi 27 kwamba alipimwa na kupatikana na virusi hivyo na amejitenga katika nyumba yake iliyoko Downing Street tokea wakati huo.

Usiku wa juzi alipelekwa hospitali kwa uchunguzi zaidi kutokana na ushauri wa daktari wake aliyesema wanafanya hivyo kutokana na tahadhari tu.

Lakini Waziri wa Nyumba wa Uingereza, Robert Jenrick alisema ni matarajio yao kwamba kutokana na vipimo alivyofanyiwa atarudi na kuendelea na majukumu yake hivi karibuni.

Jenrick alisema waziri mkuu huyo ataendelea na majukumu yake ya kuliongoza Taifa la Uingereza hata akiwa hospitalini.

MATUMAINI YAANZA KUONEKANA ULAYA

 

Taarifa zilielea jana kuwa mataifa ya Ulaya yaliyoathirika zaidi na virusi vya corona yameanza kuona dalili ndogo za matumaini katika mapambano dhidi ya virusi hivyo kufikia jana, ila Marekani inajiandaa kwa hali mbaya zaidi.

 

Haya yanakuja wakati ambapo idadi ya vifo Marekani inaelekea kufikia watu 10,000.

 

Virusi vya corona vimeuathiri karibu ulimwengu mzima na kuwapelekea karibu nusu ya watu duniani kusalia majumbani na kupelekea vifo vya karibu watu 70,000.

 

Malkia Elizabeth II wa Uingereza, juzi alitoa hotuba yake ya nne ya dharura katika uongozi wake wa miaka 68 ambapo aliwataka Waingereza na nchi za Jumuiya ya Madola kusalia kuwa kitu kimoja.

 

Ila kulikuwa na sababu ya kutabasamu katika baadhi ya sehemu Ulaya kwani Italia iliripoti visa vichache zaidi vya vifo katika kipindi cha wiki mbili na Hispania ikashuhudia visa vyake vya waliofariki vikishuka kwa siku ya tatu mfululizo, huku Ufaransa ikiwa na idadi ndogo ya waliokufa katika kipindi cha wiki moja.

GUTERRES ATOA WITO

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres amezitaka Serikali kuwajumuisha wanawake katika juhudi zao za kupambana na janga la virusi vya corona.

Visa vya dhuluma dhidi ya wanawake vimeongezeka kote duniani wakati Serikali tofauti zimeweka marufuku ya kutotoka nje kwa ajili ya kuudhibiti kuenea kwa virusi hivyo.

Akizungumza katika ujumbe alioutoa kwa njia ya video, Guterres alizitaka Serikali kuwaweka wanawake katika mipango yao ya kukabiliana na virusi hivyo.

Kwa mujibu na tume ya kitaifa ya wanawake nchini India katika wiki ya kwanza ya marufuku ya kutotoka nje, nchi hiyo iliripoti mara mbili ya visa vya unyanyasaji wa wanawake ambavyo kawaida inaandikisha.

Na uongozi nchini Ufaransa unasema visa nchini humo viliongezeka kwa theluthi moja huku Australia ikiripoti asilimia 75 ya watu waliokuwa wanatafuta njia za kuwasaidia waathirika wa dhuluma za kinyumbani kwenye mtandao wa intaneti.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles