27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Lukuvi: Tunawasaka wananchi waliokula njama na maofisa ardhi 183 kuiibia serikali

Ramadhan Hassan -Dodoma

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema baada ya kuwasimamisha kazi watumishi  183 wanaodaiwa kuingilia mfumo wa ukadiriaji wa kodi ya ardhi sasa ni zamu ya wananchi walioshirikiana nao kuiibia mapato Serikali. 

Akizungumza na Waandishi Habari jana katika ofisi za wizara hiyo eneo la Mtumba jijini hapa akiwa ameongozana na naibu wake,Angelina Mabula, Waziri Lukuvi alisema wananchi hao watakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Pia alisema anaunda timu ya wataalam kwa ajili ya kufanya uchunguzi itakayoongozwa na Taasisi ya Kuzuia na  Kupambana  na rushwa (Takukuru) kwa ajili ya kuwachunguza watumishi hao  183 .

“Nataka niwaambie wale wamiliki ambao wanafikiri madeni yao yamelipwa, nao hawapo salama wanafikiri madeni yamefutwa kwa utaratibu huu nao hawapo salama nao wamehusika katika kuiibia serikali.

“Umefanya makusudi kupatana na Afisa Ardhi kupunguziwa deni, halafu hukushtuka kwamba deni lako kubwa limefutwa huo ni wizi wa makusudi hapa tume ‘deal’ na watendaji lakini nataka niwaambie watu wote wanaofikiri ni wajanja huko katika viwanja vyao hawapo salama, tutawashughulikia,” alisema.

Akizungumzia jinsi walivyowabaini wizi huo na kuamua kuwasimamisha watumishi hao 183, Lukuvi alisema waliunda timu ambayo ilichunguza malipo ya kodi za pango la ardhi yanayofanywa kwa njia ya mfumo huo baada ya kupata shaka juu ya uendeshwaji wake.

 “Kuna mfumo wa Wizara ambao unaonesha wamiliki wote waliopewa hati na kumilikishwa kwa matumizi mbalimbali na sisi ndio tunatunza kumbukumbu,”.

Alisema kupitia mfumo huo kila wilaya wanaye mtu mmoja aliyepewa nywila (Password) ya kuingia katika mfumo na kuingiza kiwango cha umilikaji cha kodi ambayo inaonesha nani anatakiwa kulipa katika kila wilaya.

“Uchunguzi umefanywa kwa kipindi cha miezi sita na kubaini kwanza kuwapa ‘Invoice’ ndogo iliyowawezesha wenye viwanja vyao kulipa hela kidogo na tumelinganisha na mfumo wa hazina wa GePG ambao unapokea fedha,”.

 “Tumegundua kwenye mfumo wa wizara mwenye kiwanja A anadaiwa shilingi milioni 30  lakini kwenye mfumo wa wizara umefuta milioni 30 kana kwamba huyu mdaiwa amelipa fedha zote lakini mapokezi ya pili ya mfumo wa hazina yanaonesha huyu mtu amelipa milioni 3,” alisema Lukuvi.

 “Kwahiyo tumegundua kwamba kuna tofauti kati ya fedha halisi zilizopokelewa na kiwango cha fedha za data zilizofutwa kwenye mfumo wa kwetu wa ardhi.

“Sasa kwa sababu mfumo unaonesha ni nani kwa jina aliyeingia kwenye mfumo, hao 183 tumewagundua kwa ushahidi wa mfumo na walionekana wamefuta madeni,”alisema Waziri Lukuvi.

Alisema tayari jambo hilo limeanza kushughulikiwa na watumishi hao hawajaingia kazini tangu jana.

UCHUNGUZI

Kuhusu timu itakayoshirikiana na Takukuru, Lukuvi alimuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dorothy Mwanyika, kuteua wajumbe  kwa ajili ya kuanza kazi hiyo Jumanne ya Agosti 13 mwaka huu na kumaliza ndani ya siku 30 .

Ametaka timu hiyo kuhusisha wataalam kutoka katika vyombo vyote vya ulinzi na usalama, kitengo cha habari na mawasiliano (IT) kilichopo wizarani na kitengo cha malipo cha hazina cha mfumo wa GePG.

Alisema watumishi hao waliosimamishwa wanadaiwa kuchukua kiwango kinachoanzia Sh.100,000 na kuendelea.

Alitolea mfano kiwanja namba 1na 2 kitalu 1 cha Mbeya hoteli kilichopo katika jiji la Mbeya ambapo amedai kuwa mmiliki amefanya ujanja na ofisa ardhi kwa kupunguziwa kutoka mita za mraba zaidi ya 20,000 hadi mita za mraba 502 ambazo amekuwa akizilipia tangu mwaka 2002 hadi sasa.

Lukuvi alisema mteja huyo alipaswa kulipa zaidi ya Sh.milioni sita kwa mwaka lakini analipa Sh. 63,252 kwa mwaka.

Alisema Serikali inamdai  zaidi ya Sh.million 68 na kumwagiza Katibu Mkuu, Mwanyika  kumshughulikia mtumishi aliyefanya ujanja huo kwa kuwa bado yupo kazini.

UCHUNGUZI UANZIE 2016

Katika hatua nyingine Waziri Lukuvi ametaka uchunguzi wa timu itakayochunguza uanzie mwaka 2016 alipoingia wizara hiyo na kuanza kutumia mfumo huo.

“ Hawa 183 wamechunguzwa kwa kipindi cha miezi sita sasa wapitie tangu 2016 wakati tulipoanza kutumia mfumo, wachukuliwe hatua,wote ambao walionekana kujishuhulisha na mchezo huu ikiwa ni pamoja na kupelekwa mahakamani,”.

AWAKATAZA KUONANA NA MAAFISA ARDHI

Waziri Lukuvi alisema wananchi wengi wamekuwa wakiibiwa na maofisa ardhi kutokana na kuonana nao uso kwa uso hivyo ameshauri walipe kodi kwa njia ya simu.

“Mwananchi huhitaji kumfuata ofisa ardhi kukaa mezani na kufanya mazungumzo maana hivi sasa wizara imerahisisha huduma za malipo ikiwemo kwa njia ya simu na wakala wa benki hivyo wanaweza kulipa ankara bila wasiwasi na bila kwenda kumuona ofisa ardhi ofisini,”alisema.

MAPENGO KUJAZWA

Aidha ukuvi amemuagiza Kamishana wa Ardhi kujaza nafasi za watumishi 183  waliosimamishwa.

“Nataka niwatoe wasiwasi ingawa tumewaondoa tumejipanga huduma ziendelee kama kawaida Kamishana wa Ardhi ameliweka hili vizuri.

“Shughuli za Serikali hazitakwama tumeamua tufanye hili kwani watendaji wengi walikuwa wakisimamiwa na Tamisemi lakini sasa hivi wanasimamiwa na sisi ndio maana tumepata nguvu ya kuwasimamisha.Tumeamua tujisafishe mapema kwa kipindi kirefu kumekuwa na mchezo huo,”alisema

Katika hatua nyingine, Lukuvi alisema watumishi 183 waliosimamishwa kazi wataendelea kuchunguzwa na kama kuna baadhi wataonekana hawajahusika watarudishwa kazini.

“Kuna wengine wanalalamika Password zao ziliingiliwa sisi hatujali, lakini tume ipo itafanya uchuguzi na ambao hawajahusika watarejeshwa,”alisema Waziri Lukuvi.

HAKUNA UKOMO WA UMILIKI WA VIWANJA

Lukuvi pia alisema hakuna ukomo wa mtu kumiliki viwanja 

 “Ukipimiwa viwanja vyako vyote unatakiwa kupewa sio kuambiwa kwamba hiki kinaingia kwenye kupima sio kweli hakuna ukomo wa umiliki wa viwanja,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles