26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Lukuvi atumbua watatu

>>Ni watumishi wa Sekta ya Ardhi, wanadaiwa kushirikiana na matapeli wa viwanja.

Na Mwandishi Wetu-ARUSHA

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amewasimamisha kazi watumishi watatu wa Sekta ya Ardhi katika Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa tuhuma za kushirikiana na matapeli wa viwanja katika jiji hilo.

Mbali na kuwasimamisha, ameagiza maofisa hao kutokanyaga katika eneo la ofisi za Jiji hadi hapo uchunguzi utakapofanyika na uamuzi dhidi ya tuhuma zao utakapotolewa.

Lukuvi alichukua uamuzi huo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika ofisi za Jiji la Arusha jana, msingi ukiwa ni uwepo wa tuhuma nyingi  za matapeli wa viwanja  wakishirikiana na baadhi ya maofisa wa ardhi wasiokuwa waaminifu kufanya utapeli kwa wamiliki halali.

Maofisa hao waliosimamishwa ni Elizabeth Mollel, Lassen Mjema na Zawadi Mtafikikolo.

Lukuvi pia aliagiza maofisa Ardhi wa Jiji la Arusha kuhakikisha matapeli wote wa viwanja wanaoshirikiana na watumishi hao wasipatiwe huduma katika masuala yoyote ya ardhi kutokana na  kuonekana kujihusisha na mipango ya utapeli wa viwanja kwa kushirikiana na baadhi ya watumishi wa Sekta ya Ardhi katika jiji la Arusha.

Katika ziara yake hiyo ya kushtukiza pamoja na kuelezwa na Ofisa Ardhi Mteule wa Jiji la Arusha, Dicley Nyato, uwepo wa watumishi wawili, Lassen na Zawadi, huku Elizabeth akiwa katika likizo ya uzazi, watumishi hao walipotea ghafla ofisini bila taarifa mara baada ya kuelezwa wanahitajika kwa Waziri na hata pale walipopigiwa simu za mkononi hazikupatikana.

Kwa mujibu wa Lukuvi, watumishi hao wa Sekta ya Ardhi katika jiji la Arusha wamekuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na matapeli wa viwanja katika jiji hilo, jambo linalotia shaka utendaji wao wa kazi na kubainisha kuwa  maofisa hao wamekuwa na tabia ya kufuatilia kesi zilizopo katika Mabaraza ya Ardhi kwa nia ya kuwasaidia matapeli.

Kutokana na kadhia hiyo, Lukuvi aliagiza kuanzia sasa hati zote za wito wa Mahakama nchini kusainiwa na Ofisa Ardhi Mteule au Msajili wa Hati ama Kamishna Msaidizi wa Ardhi wa Kanda na Mwanasheria wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi lazima afahamishwe uwepo wa kesi husika.

“Kuanzia sasa ‘summons’ zote zipokelewe na Maofisa Ardhi Wateule, Makamishna au Wasajili wa Hati wa Kanda na watumishi wengine wasipokee wala kujihusisha,” alisema Lukuvi.

Lukuvi alisema matapeli wa viwanja wamekuwa wakifungua kesi katika Mabaraza ya Ardhi dhidi ya wamiliki halali na wakati mwingine hawawafahamu hata wamiliki,  lengo lao likiwa kuwakatisha tamaa pale kesi inapochukua muda mrefu, hasa ikizingatiwa baadhi hawana uwezo wa kuweka mawakili na hivyo kuwa na uwezekano mkubwa wa kupoteza haki zao.

Alisema, tabia hiyo haiwezi kuvumiliwa na kusisitiza kuwa mtandao wote wa matapeli wa viwanja katika jiji la Arusha ataukomesha kama alivyofanya katika jiji la Dar es Salaam ambalo huko nyuma lilishamiri sana kwa tabia hiyo.

 

Kwa upande wake Nyato, alimueleza Lukuvi kuwa wamekuwa wakisumbuliwa sana na matapeli wa viwanja katika jiji hilo na wakati mwingine huwashitaki, lengo likiwa kujipatia viwanja kwa njia ya udanganyifu na kuviuza.

Lukuvi alifanya ziara hiyo ya kushtukiza Arusha akitokea wilayani Babati Mkoa wa Manyara, ambako aliweza kutoa faraja iliyopotea kwa takribani miaka 50 kwa wananchi wa vijiji vya Singu na Endasago kwa kuamuru kubaki katika maeneo yao ambayo yalikumbwa na mgogoro kati ya wanakijiji na wamiliki wa mashamba ambao ni Kampuni za Agric Tanzania Ltd na  Endasago Co Ltd.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles