24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Lukuvi ambeza mpinzani wake

lukuviNA RAYMOND MINJA, IRINGA

MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Ismani kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), William Lukuvi, amembeza mpinzani wake anayegombea kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Patrick Sosopi, kuwa hawezi kuvaa viatu vyake.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa juzi wakati akiwahutubia wananchi wa vijiji vya Igingilanyi, Kising’a, Matembo na Ilambilole vilivyopo Isimani.

Alisema viatu vyake havimtoshi pia hana staha ya kuwashawishi wananchi kuwaletea maendeleo na badala yake anawabeza wagombea wa CCM kuwa kwa kipindi cha miaka 20 hakuna maendeleo yoyote yaliyofanywa na chama hicho.

“Mimi kiatu changu navaa namba nane, Sosopi anavaa namba moja hivi kweli ataweza kuwa mbunge wa jimbo hili, kiukweli niwaambie kama mnataka maendeleo ichagueni CCM kwa kuwa ndicho chama pekee kitakachowaletea maendeleo na sio kingine,” alisema Lukuvi.

Akiwa Kijiji cha Kinywang’anga, aliahidi kutafuta madaktari katika zahanati zilizopo jimbo hilo na dawa za kutosha ili kuendeleza huduma nzuri ya afya.

Alisema ameagiza gari la kubebea wagonjwa nchini Japani yenye gharama ya Sh milioni 120 kwa ajili ya zahanati ya Kijiji cha Kinywang’anga.

Alisema kwa sasa tayari ujenzi wa Zahanati ya Kisinga unaendelea na wanajenga wodi ya watoto, wodi ya wazazi na nyumba za kuishi watumishi ikiwa maendeleo yote yameletwa chini ya uongozi wa CCM.

Alisema kwa kipindi cha miaka mitano ijayo atahakikisha wananchi wake wanapata maji ya uhakika kutoka Mto Ruaha.

“Tayari fedha za kuvuta maji ya Mto Ruaha kutoka Iringa Mjini hadi Ismani tumeshapata, wataalamu tayari wapo na wamesema muda wowote kuanzia sasa kazi itaanza,” alisema Lukuvi.

Akiwa Kijiji cha Mkungugu alisema atapandisha kiwango cha elimu jimboni humo na kuweka haki sawa kwa wanawake na wanaume katika umiliki wa ardhi.

Kuhusu suala la umeme, alisema ni la muhimu kwa sababu kuna maeneo yaliyopo ndani hayana umeme hivyo atahakikisha analeta nguzo ili wananchi wapate nishati hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles