31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Lugola apiga marufuku watumishi kunyanyaswa

Na MWANDISHI WETU-DODOMA

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amewataka viongozi na watumishi mbalimbali wa wizara yake wafanye kazi kwa kushirikiana na kuacha tabia ya kunyanyasana wakati wanatekeleza majukumu yao ya kikazi.

Pamoja na hali hiyo, amesema kila mtumishi wa wizara yake ana umuhimu mkubwa kwa kufanikisha mafanikio ya wizara hiyo kwa kuwa watumishi hao wanafanya kazi kwa kutegemeana.

Akizungumza na watumishi wa makao makuu wa wizara hiyo jijini Dodoma jana, Lugola, alisema kikao hicho alikiitisha kwa lengo la kujuana na watumishi hao pamoja na kujua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi.

“Mambo muhimu ambayo yatatuletea mafanikio ndani ya wizara yetu ni kufanya kazi kwa bidii, kufanya kazi kwa kushirikiana na tukifanya hivyo hakika tutapendana na kuzidi kufanikiwa,” alisema Lugola.

Alisema hapendi kuona mtumishi yeyote ananyanyaswa kwa kutopewa haki zake au kucheleweshewa pasipokuwa na sababu za msingi ikiwemo malipo mbalimbali ya watumishi wanayodai na endapo yatatokea hayo watumishi hao wamletee kero zinazowakabili ofisini kwake na kwa kushirikiana na katibu mkuu wa wizara hiyo watazitatua.

“Utumishi wa umma naujua na pia nimepitia manyanyaso kadhaa mpaka leo nimefikia hapa kutokana na historia yangu, kwanini tusipendane? Kwanini tunyanyasane? Kwanini tusishirikiane?

“Ni tabia mbaya na inatakiwa kulaaniwa kwa baadhi ya wakuu wa idara na vitengo pamoja na wengineo ambao wana tabia ya kunyanyasa watumishi waliochini yao,” alisema Lugola.

Mkutano huo ambao ni wa kwanza kwa Waziri Lugola, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali, Jacob Kingu pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Ramadhan Kailima, kuzungumza na watumishi wa Wizara hiyo tangu walipoteuliwa miezi kadhaa iliyopita, walitaka kujuana zaidi na watumishi wa wizara hiyo pamoja na kujua changamoto zao zinazowakabili.

Kwa upande wake Katibu Mkuu, Meja Jenerali Kingu, aliwataka watumishi wa wizara yake kupendana na kutengeneza umoja wa kusaidiana katika matukio mbalimbali yakiwemo ya furaha na matatizo.

“Anzisheni umoja, mpendane, mshirikiane katika matukio mbalimbali, wekeni utamaduni wa kuchangiana, hii itasaidia sana kufanya kazi kwa umoja na kupata mafanikio zaidi,” alisema Meja Jenerali Kingu.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Ramadhan Kailima, alisema katika maisha yake anachukia unyanyasaji wa watumishi wa aina yoyote, hivyo hatakubaliana na kiongozi yeyote atakayemnyanyasa mtumishi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles