31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Lowassa: Msiogope

Pg 1 lowassaNA MAREGESI PAUL, NJOMBE

MGOMBEA urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, amewataka Watanzania wasiogope kufanya mabadiliko ya uongozi kwa kuwa hata Biblia inasisitiza watu wasiogope.

Amesema ili mabadiliko hayo yafanikiwe, Watanzania wanatakiwa kujitokeza kwa wingi Oktoba 25, mwaka huu na kumpigia kura za ndiyo pamoja na wagombea ubunge na udiwani kupitia Ukawa.

Lowassa aliyasema hayo jana katika mji wa Makambako, mkoani Njombe alipokuwa akihutubia maelfu ya wakazi wa Jimbo la Makambako.

“Jamani wananchi wa Makambako, nawaambia nataka kura za kutosha kuniingiza Ikulu, nikiingia madarakani nchi itakuwa tulivu na hakuna atakayemwaga damu.

“Tukichukua nchi hii itakuwa tulivu, hatutaki kumwaga damu na kama ni damu kumwagika, watamwaga wao na wala siyo sisi.

“Kwahiyo, nasema ‘I am serious’, nataka kura za kutosha kwa sababu naambiwa wale wenzetu (CCM) ni mabingwa wa kuiba kura. Nataka watakapoiba, zibaki nyingine za kutuwezesha kushinda.

“Hata nyie mnaotaka kuhama hameni wala msiogope kufanya mabadiliko kwa sababu neno usiogope limeandikwa mara 365 katika Biblia… nawaambia msiogope kwa sababu hata mimi siogopi,” alisema Lowassa na kushangiliwa.

Akizungumzia baadhi ya kero zinazowakwaza Watanzania, Lowassa alisema kama atafanikiwa kuingia madarakani, Serikali yake itakuwa makini, kwa kuondoa michango yote ya elimu ya sekondari ili wazazi wapate nafasi ya kusomesha watoto wao.

“Kuna kero nyingi sana nimeambiwa ziko hapa Makambako, ambazo naamini ninaweza kuziondoa pindi tu nitakapoingia madarakani.

“Kwanza kabisa, nitaondoa kero ya maji iliyoko hapa Makambako kwa sababu najua namna ya kuitatua kwa kuwa nilikuwa Waziri wa Maji enzi za utawala wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa.

“Pili, hili tatizo la mashine za kukusanya kodi za EFD nitaliangalia kwa kina kwa sababu haiwezekani nchi ikawa ya kibabekibabe tu, yaani wafanyabiashara wanasema hivi na wewe hutaki kuwasikiliza.

“Chuo cha VETA kitajengwa hapa Makambako ili kiwasaidie vijana, matatizo yote ya walimu na wafanyakazi wote serikalini, nitayatatua kwa sababu uwezo ninao.

“Nitafuta pia michango yote shule za sekondari kwa sababu chini ya Serikali yangu, elimu itatolewa bure kwani haya yote yako kwenye ilani ya chama chetu.

“Kwa maana hiyo, nawaomba tena, ikifika Oktoba 25, mwaka huu, mjitokeze kwa wingi kunipigia kura mimi, wabunge wa Ukawa na madiwani wetu wote ili nikaunde Serikali yenye nguvu,” alisema.

Katika maelezo yake, Lowassa ambaye ni Waziri Mkuu wa zamani, alisema suala la umasikini kwa Watanzania ni la kujitakia kwa kuwa Tanzania ina rasilimali nyingi zinazoweza kuchangia kukuza uchumi wa Taifa.

Alizitaja baadhi ya rasilimali hizo ambazo alisema atazitumia kukuza uchumi, kuwa ni pamoja na dhababu, gesi na mazao kama chai na pamba.

“Kama Mwenyezi Mungu akinijalia, nitaendesha nchi hii kwa spidi ya ajabu, kwani hatuna sababu ya kuwa masikini.

“Nawahakikishia uchumi wa nchi hii utakua kwa kasi kwa sababu rasilimali zipo na kinachotufanya tuwe masikini ni kutojua vipaumbele vyetu,” alisema.

Juu ya migogoro ya muda mrefu kati ya wakulima na wafugaji, Lowassa alisema itatoweka kwa sababu haiingii akilini Watanzania waendelee kugombana katika nchi yao, na kwamba ardhi yote itapimwa na wananchi kumilikishwa ili waitumie kuinua maisha yao.

Baada ya kuhutubia mkutano huo, Lowassa alihutubia mkutano mwingine mkubwa wa hadhara katika mji wa Njombe na kuwaombea kura wabunge na madiwani wa Ukawa, huku akisisitiza wananchi wasiichague CCM.

 

SUMAYE

Awali akihutubia maelfu ya wananchi hao, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, alisema katika Serikali ya CCM hakuna waziri anayefaa kupewa madaraka kwa kuwa wameshindwa kuwaletea maendeleo Watanzania.

“Katika Serikali ya CCM, hakuna waziri hata mmoja mwenye sifa za kupewa madaraka kwa sababu wameiharibu nchi hii. Hakuna hata mmoja na ndiyo maana namshangaa sana Magufuli (mgombea urais wa CCM) anaposema akiingia madarakani, atakomesha rushwa wakati na yeye yuko kwenye Serikali iliyojaa rushwa.

“CCM ni shidaaa, nawaomba msiwape kura kwa sababu hawana tena uwezo wa kuboresha maisha yenu,” alisema Sumaye.

Katika maelezo yake, Sumaye alionyesha kushangazwa na baadhi ya maeneo nchini kukosa maji, ukiwamo mji wa Makambako.

“CCM sasa imeanza kusambaza nguzo za umeme katika maeneo yasiyokuwa na umeme ili wawadanganye wanawaletea umeme, lakini msiwape kura,” alisema.

Ili kuthibitisha jinsi CCM walivyopoteza mwelekeo, alimtolea mfano Katibu Mkuu wa chama hicho tawala, Abdulrahman Kinana ambaye amekuwa akisema baraza la mawaziri lina mawaziri mizigo.

Kutokana na hali hiyo, alisema kama angekuwa Kinana angelazimika kuihama CCM na kujiunga na Ukawa kwa kuwa ndio wenye nia ya dhati ya kuwaletea maendeleo Watanzania.

 

MGOMBEA UBUNGE

Naye mgombea ubunge katika Jimbo la Makambako, Mhema Oraph (Chadema), aliwaambia wananchi kwamba atakapoingia madarakani, atatatua kero ya maji, atafuta ushuru usiokuwa na maana, atasaidia upatikanaji wa umeme na pia atatatua migogoro ya ardhi iliyokithiri jimboni humo.

Wakati huo huo, aliyekuwa Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM, Mkoa wa Njombe, Ally Mwimike, alitangaza kukihama chama hicho na kujiunga na Ukawa.

Ingawa hakutaja chama alichojiunga nacho katika umoja huo, Mwimike alisema Watanzania wanatakiwa kufanya mabadiliko kwa kuwa CCM imetawaliwa na rushwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles