LISSU: NYALANDU KARIBU CHADEMA

0
53

Na MWANDISHI WETU

SIKU moja baada ya aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu, kujivua uanachama wa CCM na nyadhifa zote ndani ya chama hicho, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amemkaribisha ndani ya Chadema.

 

Lissu ambaye alipigwa risasi na watu wasiojulikana mjini Dodoma, Septemba 7 mwaka huu, alitoa kauli hiyo jana akiwa katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya anakotibiwa.

 

Akizungumza kwa sauti ya kukwaruza akiwa kitandani, Lissu alisema bado Watanzania wanahitaji kufanya uamuzi mgumu kwa kuikataa CCM kupitia uchaguzi wa madiwani unaotarajiwa kufanyika Novemba 26.

 

“Nimepokea kwa faraja kubwa taarifa ya kujiuzulu kwa Lazaro Nyalandu, ambaye alikuwa jimbo la jirani kwangu Singida Kaskazini, kutoka CCM na maombi yake ya kujiunga na Chadema.

 

“Nyalandu ameitumikia CCM kama Mbunge wa Singida Kaskazini kwa karibu miaka 20, lakini pamoja na muda wote huo, bado ana mawazo ya ujana, bado ni kijana katika fikra zake, ndiyo maana akapata ujasiri na uthubutu wa kuchukua hatua hii kubwa, ambayo watu wengi wasiopenda kuwa CCM wanashindwa kuchukua, naomba nimpongeze kwa hili,” alisema Lissu.

 

Pamoja na mambo mengine, Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), aliwataka Watanzania kuwapigia kura wagombea wa udiwani kutoka Chadema na vyama vingine vya Ukawa.

 

“Naongea nikiwa katika kitanda cha Hospitali ya Nairobi ambapo kama mnavyofahamu, naendelea na matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na wale ambao wamezoea kututesa.

 

“Ndugu zangu nina ujumbe leo, unaohusu uchaguzi wa marudio wa madiwani, kuna kata 40 zinagombaniwa.

 

“Kuwapa kura CCM ni sawa kuendelea kuhangaika wakati watu wachache wananufaika. Kwahiyo, ndugu zangu naomba tufanye maamuzi magumu katika uchaguzi huu katika hizi kata 40… Ni kuikataa CCM na kukubali kupiga kura kwa ajili ya wagombea watakaowekwa na Chadema pamoja vyama vingine vya Ukawa.

 

“Ujumbe huu ni ‘special’ kwa ajili ya wananchi wa Kata ya Siuyu, nawasalimu nyote nikiwa katika Hospitali ya Nairobi, ambako naendelea na matibabu baada ya kupigwa risasi…

 

“Ujumbe wangu leo kwenu, naomba sana mfahamu hili kwamba nguvu zilezile zilizotumika kumfunga Mahami (aliyekuwa Diwani wa Siuyu Mahami Gerald) na baadaye kumzuia asiendelee na kazi ya udiwani, kazi ambayo mmempa ninyi kwa ushindi mkubwa 2015, ni nguvu hizo hizo ambazo zimenifungulia mashtaka mara nyingi.

 

“…Naomba wananchi wa Siuyu mchukue hatua bila woga, wala kusitasita, nchi huwa haikombolewi na waoga, bali inakombolewa na wajasiri.

 

“Naombeni wananchi wa Siuyu mimi ninawafahamu, tumeshinda mara mbili pamoja kwa sababu mmekuwa wajasiri sana, katika uchaguzi huu wa diwani ambaye tumenyang’anywa bila sababu, aliondolewa madarakani bila sababu kwenye hili waonyesheni watu Siuyu wakoje.

 

“Naomba siku ya uchaguzi kila mzee, kila mama, kila baba, kaka, dada ajitokeze kuhakikisha Mahami Gerald anabaki kuwa diwani wa Siuyu.

 

“Badala ya mimi kuja kuzungumza nanyi moja kwa moja, nazungumzia kitandani, naomba tuwape fundisho watesi wetu na vilevile tuwape Watanzania fundisho kuwa Siuyu huwa hatuchezewi.

 

“Nawashukuruni, nawatakia kila la kheri, Mwenyezi Mungu atawalinda na atawapa ushindi wa nguvu,” alisema Lissu.

 

Mbali na hilo katika ujumbe wake huo wa sauti wa dakika 7, pia alizungumzia bomoabomoa inayoendelea katika baadhi ya maeneo nchini.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here