23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

LISSU ‘ALIMISS’ BUNGE, CHADEMA, TLS

Na Mwandishi Wetu               |       


Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, amesema amelikumbuka Bunge, chama chake (Chama cha Demokrasia na Maendeleo-Chadema), Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) na Watanzania kwa ujumla.

Kwa mujibu wa waraka wake alioundika ikiwa leo ametimiza mwaka mmoja tangu ajeruhiwe kwa risasi na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake jijini Dodoma, Septemba 7, mwaka jana.

Katika waraka huo kwa Watanzania, Lissu amesema mwaka mmoja umekuwa mrefu na mgumu sana kwangu kwake kwa sababu ya majeraha ya mwili na pia amei-miss Tanzania na Watanzania.

“Nime-miss sana Bunge, licha ya matatizo yote ya Bunge la Spika Ndugai. Nimewa-miss sana watu wangu wa Jimbo la Singida Mashariki na mikutano yetu ya hadhara, kazi zangu za chama, viongozi wenzangu, wanachama wetu na wafuasi wetu katika mamilioni yao.

“Nime-miss sana mapambano ya utetezi wa haki za watu wetu ndani na nje ya Mahakama, Mawakili wa Tanzania Bara (TLS) walionipa heshima ya kuwaongoza katika kipindi kigumu sana katika historia ya TLS,” amesema Lissu.

Amesema katika huo mwaka mmoja wa kukaa nje ya nchi, wa kutokuonana moja kwa moja na watu wake, familia, ndugu, jamaa, majirani na marafiki zake, kufuatilia mapambano ya kudai haki na demokrasia mitandaoni badala ya kuwa mshiriki kwenye uwanja wa mapambano, sasa ameelewa maana hasa ya kuwa ‘uhamishoni.’

Aidha, Lissu amemzungumzia dereva wake ambaye alidaiwa kutoroshwa kwa madai ya kushiriki njama za kumjeruhi akisema dereva huyo amekuwa mwaminifu kwake tangu akiwa na miaka 19, hawezi kushiriki njama hizo.

Hata hivyo, Lissu pia amehoji kuhusu ulipofikia uchunguzi wa polisi kuhusu tukio la kujerushiwa kwake na kuongeza kuwa hadi sasa hakuna mtu yeyote anayeshukiwa kumshambulia.

“Hakuna yeyote anayetuhumiwa, hakuna yeyote aliyehojiwa na wapelelezi wa polisi kama shahidi. Hata waathirika wa shambulio lenyewe, mimi na dereva wangu, hatujahojiwa,” amesema Lissu huku akiwatoa hofu Watanzania kwamba atarejea salama wakati wowote.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Uenezi ya Chadema, Hemed Ally, ambaye alikuwapo kipindi chote ambacho Lissu alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Nairobi, amesema aliyopitia Lissu ni mapito yanayompambanua katika mapambano ya ukombozi.

“Kaka yangu, Lissu unafahamu njia yetu, maisha yetu, upendo na udugu wetu tumshukuru Mungu kwa haya mapito.

“Naamini kesho yetu ya vita hii ni neema na ndoto ya Watanzania na ndiyo maana Mungu amekupitisha. Endelea kuugua pole na nyumbani Watanzania wanakusubiri kwa hamu isiyo kifani,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles