24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

LISHE DUNI YAHATARISHA MAISHA YA WATOTO MTWARA


Na FLORENCE SANAWA,MTWARA



Mkoa wa Mtwara unakadiliwa kuwa na watoto zaidi ya 120,283 wenye upungufu wa damu unatokana na udumavu.

Wengi wa watoto hao wana uzito pungufu unaosababishwa na ukondefu ambao pia chanzo chake ni lishe duni.

Akizungumza juzi katika kikao cha tathmini ya lishe, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa alisema zipo tafiti mbalimbali zimefanywa na kuonyesha kuwa asilimia 47 ya wanawake wenye umri wa kuzaa hawana lishe nzuri.

Alisema lishe duni imekuwa na athari nyingi kwa wanawake hasa wajawazito ambao huwa katika hatari zaidi ya kupata watoto njiti pindi wanapojifungua, kuharibika kwa mimba, mtoto kufa akiwa mchanga na wengine hufia tumboni.

“Hapa lazima tujipange ili kuondokana na hili tatizo la lishe kwa kuweka mikakati na kuwa na takwimu halisi zitakazosaidia kupunguza tatizo hilo la utapia mlo miongoni mwa jamii.

“Hii ni changmoto kubwa, lazima tushirikiane ili kuweza kuondokana nayo, watoto 120,283 ni wengi sana, tunapoteza nguvu kazi ya taifa,” alisema Byakanwa.

Naye Ofisa Lishe Mkoa wa Mtwara, Herieth Joseph alisema bado kuna changamoto kubwa ya mama wajawazito kutumia dawa za kuongeza damu.

“Ili kuepusha vifo kwa akina mama, lazima tutoe elimu kwa jamii kuondokana na imani potofu juu ya kuongezewa damu hasa wakati wa kujifungua pale wanapotumia damu nyingi, wakisha elimishwa itasadia wao kuanza kutumia dawa hizo ili kuondokana na hili suala la kuongezewa damu,” alisema Joseph

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dk. Wedson Sichalwe alisema serikali inapaswa kutoa maelekezo kwa halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya elimu kwa akina mama wajawazito.

“Hivi sasa halmashauri zimekuwa hazitengi fedha kwa ajili ya utekelezaji wa afya za lishe kwa kila mtoto, lakini pia wanawake wajawazito wanachelewa kuhudhuria kliniki pindi wanapojitambua kuwa ni wajawazito,” alisema Sichalwe.

Hivi karibuni, akikabidhi mradi wa kuboresha huduma za afya, uliotekelezwa na Shirika lislilo la Kiserikali la Agakhan Foundation katika Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, mkurugenzi wa shirika hilo, Biko Evaristy alisema utapiamlo unaathiri hali ya afya na mazingira kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 5.

“Udumavu siyo mzuri, unapokomaa katika jamii husababisha uwezo wa kufikiri kuwa mdogo hivyo watu kuanza kurithishana na kuwa na mawazo sawa ndio maana katika mradi huu udumavu tuliupa kipaumbele.

“Hivi sasa inakadiliwa kuwa zaidi ya watoto milioni 180 duniani, wenye umri chini ya miaka mitano wamedumaa kiakili na kimwili kwa kusosa lishe bora.

“Mtoto mwenye udumavu huwa na seli ndogo zisizo hilimili kulinda mwili kupokea magonjwa kulingana na uzito wenyewe wa tatizo ingawa jamii haijalipa kipaumbele hili tatizo, unachangia kupata magonjwa mbalimbali utotoni,”  alisema Biko.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles