27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Lishe duni, elimu vyatajwa chanzo udumavu Iringa

Na MWANDISHI WETU-IRINGA

LISHE duni kutokana na wananchi kutokuwa na elimu ya ulaji wa vyakula vya kutosha na vyenye mchanganyiko wa viini lishe, ndiyo sababu kubwa ya Iringa kuwa moja ya mikoa inayoongoza kwa watoto kuwa na utapiamlo na udumavu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Ofisa Lishe wa Mkoa wa Iringa, Neema Mtekwa alisema kuwa jamii imekuwa ikishindwa kutumia lishe yenye virutubishi hali inayosababisha kwa kiasi kikubwa kuwa na utapiamlo na udumavu licha ya Mkoa wa Iringa kuwa moja ya mikoa inayoongoza kwa uzalishaji.

Neema alisema kuwa kwa mujibu wa utafiti uliofanyika mwaka juzi kuhusu hali ya lishe nchini, Mkoa wa Iringa una watoto 15,000 chini ya miaka mitano wenye udumavu, sawa na asilimia 47 huku kitaifa ikiwa na asilimia 31.8.

“Watoto wenye ukondefu ni 8,473 sawa na asilimia 3.7 huku kitaifa ni asilimia 3.8 na hali ya kuzaliwa na uzito pungufu ni asilimia 6.2 sawa na watoto 4,842 na kitaifa mkoa una asilimia 6.3,” alisema Neema.

Aliongeza kuwa uzito pungufu ni asilimia 18.4 sawa na watoto 29,696 huku kitaifa mkoa ukiwa na asilimia 14.7 na uzito uliozidi ni watoto 4,842 sawa na asilimia 3 huku kitaifa ni asilimia 2.8.

Neema alisema kuwa sababu kubwa inazosababisha hali hiyo ni kutowekeza muda wa kuwa na watoto kuwalisha ipasavyo ikiwepo kuwapa pombe kwa baadhi ya maeneo, lishe duni kutokana na wananchi kutokuwa na elimu ya ulaji wa chakula cha kutosha na chenye mchanganyiko wa viini lishe.

Aliongeza kuwa visababishi vingine ni watoto wa miezi 6 hadi 23 wanaopewa kiwango cha chakula kinachokubalika ni asilimia 12 tu huku watoto hao wanaopewa mlo wenye mchanganyiko wa vyakula tofautitofauti zikiwemo mbogamboga, matunda na vyakula vya jamii ya kunde na nyama ni asilimia 25.

Neema alisema kuwa kutokana na changamoto hiyo, Mkoa wa Iringa umeweka mikakati mbalimbali katika kuweza kupambana na hali ya utapiamlo na udumavu kwa watoto wenye chini ya miaka mitano ikiwemo kutoa elimu ya nadharia na vitendo kwa jamii kuhakikisha kwamba ulaji wa kiwango cha juu cha virutubishi unafanyika na kuzingatia unyonyeshaji katika siku 1,000 za mtoto unafuatwa.

“Katika kupambana na hali hiyo, mkoa umekuwa ukishirikiana na sekta mtambuka na wadau mbalimbali katika kutoa elimu juu ya lishe bora licha ya changamoto ya uhaba wa maofisa lishe, lakini kupitia watoa huduma za afya jinsi gani ya kutoa ushauri wanasaidia kwa kiasi kikubwa kutoa elimu hiyo,” alisema Neema.

Alisema kuwa mkakati mwingine ni kuhakikisha halmashauri zote za mkoa zinatenga fedha za utekelezaji wa afua mbalimbali za lishe kama kununua vyakula dawa, kutoa elimu za lishe, kupanga mipango ya lishe, kufanya siku za afya na lishe ya kijiji na mitaa, hivyo mkoa unasimamia na halmashauri kutekeleza hayo.

Wakizungumza kuhusu changamoto hiyo, baadhi ya wadau wanaozalisha unga wenye viini lishe mkoani hapa walisema kuwa mkakati mojawapo ni kuzalisha unga wenye viini lishe kwa matumizi ya kila siku kwa jamii.

Mmoja wa wadau hao, Mkurugenzi wa kiwanda cha kuzalisha unga wa sembe wenye viini lishe cha AMP Super Sembe, Alfred Mpanga alisema kuwa walipewa mkakati wa kuzalisha unga wenye viini lishe kutoka kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza kwa lengo la kupambana na udumavu na utapiamlo.

Mpanga alisema kuwa kutokana na hilo, unga unaozalishwa kwenye kiwanda hicho lazima uwe na viini lishe ambavyo vinasaidia kwa kiasi kikubwa kuweza kupambana na udumavu na utapiamlo hali ambayo kwa kiasi kikubwa imesaidia jamii kubadilika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles