27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

LIGI KUU BARA IKIRINDIMA LEO MIAMBA MITANO KUWANIA UONGOZI

Na MOHAMED KASSARA -DAR ES SALAAM

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, leo watashuka dimbani kusaka pointi tatu muhimu dhidi ya wapinzani wao Mtibwa Sugar, katika mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, Yanga itaingia uwanjani ikifahamu kwamba inahitaji ushindi ili kurefusha pengo la pointi kati yake na mpinzani wake mkuu, Simba ambayo kesho itaumana na Stand United, kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Yanga ipo nafasi ya sita katika msimamo, ikiwa na pointi nane, baada ya kucheza michezo minne, ikianza kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Lipuli FC, ikaichapa Njombe Mji bao 1-0, ikalazimisha sare ya bao 1-1 na Majimaji FC, kabla kuitungua bao 1-0 Ndanda FC, wiki iliyopita.

Kama itafanikiwa kuvuna pointi tatu leo, itafikisha pointi 11, ambazo zitaifanya iongoze ligi endapo Azam iliyoko nafasi ya pili ikiwa na pointi 10 itaivaa Singida United na kupoteza katika mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri uliopo Manispaa ya Dodoma na kusalia na pointi zake 10.

Yanga pia itakuwa ikiomba Prisons  inayolingana nayo pointi ichezee kichapo itakapoikabili Mbao FC katika mchezo utakaofanyika leo kwenye Uwanja wa Kirumba, Mwanza.

Yanga itataka kuendeleza ubabe wao baada ya kuibuka na ushindi wa bao 3-1 dhidi ya Mtibwa  katika mchezo uliozikutanisha timu hizo msimu uliopita kwenye uwanja huo.

Mtibwa kwa upande wake, itaingia uwanjani ikisaka ushindi kwa sababu kuu mbili, kuendelea kukalia kiti cha uongozi wa ligi hiyo, lakini pia kulipa kisasi cha kipigo ilichokipata msimu uliopita.

Wakata miwa hao wapo kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo wakiwa na pointi 10, baada ya kucheza michezo minne, wakishinda mitatu na kutoka sare moja.

Walizindua kampeni zao kwa kuichapa Stand United bao 1-0, ikailaza Mwadui  1-0, ikaitungua Mbao mabao 2-1, kabla ya kulazimisha sare ya bao 1-1 na Ruvu Shooting wiki iliyopita.

Kama itafanikiwa kuifunga Yanga leo itafikisha pointi 13, hivyo kujiweka katika mazingira mazuri ya kuendelea kushika uongozi kama Azam itavurunda kwenye mchezo wake na Singida.

Pigo kwa wapenzi wa Yanga ni kukosekana kwa kiungo wao mahiri, Papy Tshishimbi, anayetumikia adhabu ya kadi tatu za njano.

Kocha Mkuu wa Yanga, Mzambia George Lwandamina, aliliambia MTANZANIA jana kuwa ana matumaini ya kushinda mchezo huo baada ya kufanya maandalizi ya kina kwa ajili ya kuwakabili Mtibwa.

“Hatukuwa tukifunga mabao mengi katika michezo yetu iliyopita kutokana na kukosa umakini licha ya kwamba tulikuwa tunatengeneza nafasi nyingi, kwa wiki nzima nilikuwa nashughulikia tatizo hilo ambalo kwa kiasi kikubwa naamini nimelipatia ufumbuzi.

“Hata hivyo, katika mechi muhimu ni kupata ushindi bila kujali idadi ya mabao, nimewaambia wachezaji wangu hawatakiwi kumdharau mpinzani wetu yeyote kwa kuwa hii ni ligi na kila mmoja anaingia uwanjani akiwa na lengo moja kuu, kuvuna pointi tatu ili ajiweke katika nafasi nzuri kwenye msimamo,” alisema Lwandamina.

Hayo yakiwa ya Lwandamina, kocha mkuu wa Mtibwa, Zuberi Katwila, alisema wamekuja Dar es Salaam si kwa ajili ya kutalii bali  kuchukua pointi tatu na kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.

“Najua mchezo utakuwa mgumu, lakini naamini kikosi nilichonacho kinaweza kupambana na kupata ushindi katika mazingira yoyote iwe nyumbani au ugenini.

“Tutapambana kwa hali yoyote ili kuhakikisha tunapata pointi tatu muhimu na ninaamini nia, sababu na uwezo tunao,” alisema Katwila ambaye ni kiungo wa zamani wa Mtibwa.

Vumbi jingine la ligi hiyo litaonekana likitimka kwenye viwanja vingine vitano, Majimaji baada ya kuambulia kipigo kutoka kwa Njombe Mji katika mchezo wake uliopita, itajiuliza tena kwa kuikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Majimaji.

Majimaji inakamata nafasi ya 15 miongoni mwa timu 16 zinazoshiriki ligi hiyo ikiwa na pointi mbili, wakati Kagera inakamata mkia ikiwa na pointi moja.

Ndanda FC baada ya kujeruhiwa na Yanga kwa kulazwa bao 1-0 itakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Nangwanda, Mtwara kupepetana na  Lipuli, Njombe Mji itasafiri hadi Mlandizi, Pwani kuwavaa maafande wa Jeshi la Kujenga Taifa, timu ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mabatini.

Mbao FC baada ya kulazimisha sare mabao 2-2 dhidi ya Simba, itaikaribisha Prisons kwenye Uwanja wa Kirumba, Mwanza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles