24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Liewig abwaga manyanga Stand Utd

babu-patrick-liewigNa ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM

KOCHA Mkuu wa Stand United, Patrick Liewig, amesitisha mkataba wa kuifundisha timu hiyo katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara, kutokana na kuchoshwa na mwenendo mbaya wa uongozi wa klabu hiyo.

Liewig raia wa Ufaransa aliyewahi kuifundisha Simba kabla ya kurejea kuinoa Stand tangu msimu uliopita kwa mkataba wa miaka miwili, amefikia uamuzi huo baada ya kukubaliana na uongozi katika kikao kilichofanyika jana.

Liewig ni kocha wa tatu kubwaga manyanga msimu huu baada ya Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ aliyeachana na Mwadui FC pamoja na Rogasian Kaijage aliyejiuzulu kuifundisha Toto Africans.

Akizungumza na MTANZANIA juzi, Liewig alisema haridhishwi na mambo yanayoendelea ndani ya uongozi wa klabu hiyo ambao pia umeshindwa kuwaheshimu wachezaji na benchi la ufundi.

“Mkataba wangu ulitakiwa kumalizika Juni mwakani, lakini kutokana na hali ilivyo ninalazimika kuondoka kwa sababu uongozi uliopo umeshindwa kuiongoza timu vizuri,” alisema.

Chanzo cha habari za uhakika kutoka ndani ya klabu hiyo, zinaeleza kuwa tayari kocha msaidizi, Athuman Bilal, amekabidhiwa majukumu ya kuifundisha timu hiyo ambapo kibarua chake kilianza rasmi katika mchezo wa jana dhidi ya Azam FC.

“Uongozi ulifikia mwafaka na kocha Liewig tangu jana jioni na tayari ameondoka kwenda jijini Dar es Salaam kusubiri safari ya kurejea kwao Ufaransa.

Hata hivyo, inadaiwa kuwa uongozi wa Stand umeshindwa kumlipa Liewig mshahara wake pamoja na wachezaji baada ya Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Acacia iliyokuwa ikiidhamini timu hiyo kujitoa.

Liewig anaondoka na kuiacha Stand ikiwa katika nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa imejikusanyia pointi 16 baada ya kushuka dimbani mara nane.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles