33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

LEMA AANZA KUONA ‘MOSHI MWEUPE’

Na ABRAHAM GWANDU – ARUSHA


lemaMBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), ameanza kuona dalili za kutoka mahabusu anakoshikiliwa kwa siku 50 sasa, baada ya Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, kukubali maombi ya mawakili wake ya kuwasilisha notisi ya nia ya kukata rufaa dhidi ya dhamana yake.

Kutokana na hali hiyo, Jaji Dk. Modesta Opiyo, anayesikiliza shauri hilo, alitoa siku kumi kuanzia jana kwa upande wa mshtakiwa huyo, kuwasilisha maombi yake ya dhamana nje ya muda.

Awali upande wa Jamhuri uliwasilisha pingamizi mbili katika maombi hayo namba 69 ya mwaka huu, ukiiomba mahakama hiyo isisikilize maombi hayo kwani hayakufuata taratibu za kisheria.

Desemba 16 mwaka huu, Jaji Dk. Opiyo alitupilia mbali pingamizi hizo na kusema mahakama haioni sababu ya msingi ya kumnyima haki Lema kwa kuwa hoja zilizowasilishwa mahakamani hapo na upande wa wajibu maombi, hazikuwa na mashiko kisheria.

Akisoma uamuzi wake jana, Jaji Dk. Opiyo alisema busara ya mahakama iliyo na nia ya kuendelea kutoa haki, inakubali maombi na inampa mleta maombi siku 10 kuanzia jana ili awasilishe maombi yake nje ya muda.

Jaji Dk. Opiyo ambaye alianza kusoma uamuzi huo jana saa 6:26 mchana hadi saa 7:18, alisema kesi inapoondolewa mahakamani, haifungi milango ya kukata rufaa nyingine ambayo ni haki ya mtuhumiwa.

“Mahakama hii kwa kuzingatia uamuzi wa kesi mbalimbali, ni lazima izingatie na kuangalia sababu, muda na athari ambazo zitatokana na uamuzi wake.

“Mahakama haikubaliani na hoja za upande wa wajibu maombi na imeona ucheleweshwaji wa notisi ya kusudio la kukata rufaa ulikuwa na sababu za msingi, hivyo inakubali maombi haya na inampa mleta maombi siku kumi kuanzia sasa.

“Kwa kuzingatia haki, walichelewa kwa sababu za msingi, hivyo mahakama haijaona kuwa ucheleweshwaji huo ni wa makusudi na katika siku mbili au tatu walizochelewa, kulikuwa na mashauri mengine yaliyokuwa yakiendelea mahakamani,” alisema Jaji Dk. Opiyo.

Katika maombi hayo, upande wa Jamhuri ulikuwa ukiwakilishwa na mawakili, Matenus Marandu na Hashimu Ngole, huku upande wa mleta maombi ambao wanamtetea Lema, unawakilishwa na mawakili Sheck Mfinanga na Faraji Mangula.

Baada ya uamuzi huo, Lema alirudishwa mahabusu akisubiri hatima yake iwapo mahakama itampa dhamana au vinginevyo.

Wakizungumzia uamuzi huo, mawakili wa pande zote mbili walikubaliana na uamuzi wa mahakama hiyo. Wakili Ngole alisema hawana pingamizi lolote.

Naye Wakili Mfinanga alidai kuwa wameridhishwa na uamuzi wa mahakama na tayari wameanza mchakato wa kuwasilisha maombi ya rufaa ya mteja wao.

Hata hivyo, taarifa zilizopatikana wakati tunakwenda mitamboni, zinasema mawakili hao walifanikiwa kuwasilisha rufaa yao na kupewa namba 126 ingawa ilikuwa haijapangiwa jaji wa kuisikiliza.

Pamoja na hayo, leo Lema atafikishwa tena mahakamani katika kesi ya kutuma ujumbe wa matusi kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo. Katika kesi hiyo, mkewe Lema aitwaye Neema Lema, naye ni mshtakiwa.

 

MAOMBI YALIVYOWASILISHWA

Akiwasilisha hoja za maombi hayo mwishoni mwa wiki, Wakili Mfinanga aliiomba mahakama hiyo iwapatie muda mfupi usiozidi saa 1:30 kupeleka notisi hiyo, ili mahakama hiyo iweze kurekebisha makosa yaliyojitokeza mahakama ya chini.

Alidai kuwa uamuzi wanaotarajia kukatia rufaa, ni  ule uliotolewa Novemba 11, mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha na Hakimu Desderi Kamugisha, ambako Lema anakabiliwa na kesi namba 440 na 441 za uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli.

Alitaja sababu mbili za msingi za kukatia uamuzi huo rufaa, kuwa ni kuiomba mahakama hiyo ipitie makosa ya kisheria yaliyofanywa na Hakimu Kamugisha, aliyekubaliana na maombi ya mawakili na kumyima Lema dhamana.

“Kuna vitu muhimu vitasahihishwa iwapo tutaleta notisi ya nia ya kukata rufaa na rufaa yenyewe kusikilizwa na mahakama yako.

“Mahakama hii ndiyo msimamizi wa haki na sheria na inaweza kutoa ruksa ili tuweze kusikilizwa na rekodi ya mahakama ya chini iweze kurekebishwa, kwani ni muhimu mahakama kuzingatia maombi haya pasipo kuzingatia mambo mengine,” alisema Wakili Mfinanga wiki iliyopita.

Huku akirejea mashauri mbalimbali ya mahakama za juu, aliendelea kueleza mahakama hiyo kuwa mahakama ikishasema imempa mtu haki ya dhamana lazima itaje masharti yake.

Alitaja sababu ya pili kuwa ni wao kutopumzika kwani muda wote walikuwa mahakamani ili kuiomba mahakama irekebishe makosa hayo ya kisheria.

“Baada ya uamuzi huo kutolewa, muda wa kazi ulishaisha na ilikuwa ni Ijumaa, hivyo Novemba 14, mwaka huu, tulipeleka barua ya malalamiko mahakamani hapo na tulipoitwa pande zote mbili, tulikumbana na pingamizi zilizowasilishwa na mawakili wa Serikali.

“Novemba 22 mahakama ilitoa uamuzi na kutaka waleta maombi tukate rufaa na hapo mleta maombi alipata haki yake ya kukata rufaa ambayo haikuelezwa mahakama ya chini.

“Tulitoa notisi tukiamini tuko ndani ya muda na hatimaye rufaa ililetwa mbele ya Jaji Mfawidhi Fatuma Masengi.

“Katika rufaa hiyo namba 113, tulikutana tena na pingamizi la Serikali, kuwa tumetoa notisi ya rufaa hiyo nje ya muda wa siku moja, hivyo hizo ni jitihada tulizokuwa tukizifanya na siyo kwamba tulikuwa wazembe au wajinga wa sheria kama ilivyodaiwa na wakili wa Serikali,” alisema.

Kwa mujibu wa wakili huyo, hakukuwa na makosa yoyote ya kisheria kama inavyodaiwa na waleta maombi hao, kwani baada ya hakimu kusema mahakama inampa mshtakiwa dhamana, Jamhuri kwa haki yake walisimama na kuifahamisha mahakama wana nia ya kukata rufaa.

“Ni utaratibu wa kisheria, kuwa panapokuwa na notisi ya nia ya kukata rufaa, mahakama haiwezi kuendelea na jambo lolote kuhusu kesi hiyo.

“Hivyo basi, hakimu asingeweza kuendelea na kesi na inafahamika notisi inasimama badala ya rufaa,” alidai Wakili Mfinanga.

Lema alikamatwa Novemba 2, mwaka huu, nje ya viwanja vya Bunge mjini Dodoma na kusafirishwa hadi Arusha. Alifikishwa mahakamani Novemba 8, mwaka huu akikabiliwa na mashtaka ya uchochezi dhidi ya Rais Dk. Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles