30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Kwanini Afrika inamlilia Fidel Castro

Mwalimu Nyerere akisalimiana na Fedel Castro wakati wa uhai wao.
Mwalimu Nyerere akiwa na Fedel Castro wakati wa uhai wao.

Na LEAH H. MWAINYEKULE,

DESEMBA 10, 2013 wakati dunia nzima ikiwa inafuatilia matangazo ya moja kwa moja ya kumbukumbu ya kifo cha Rais Nelson Mandela, jambo la kihistoria lilifanyika:  Rais Barack Obama wa Marekani alishikana mkono na Rais Raul Castro wa Cuba.  Wakati huo huo, Seneta Ted Cruz wa Marekani, alitoka nje wakati Raul Castro aliposimama kutoa hotuba kwenye tukio hilo.

Rais Obama alikuwa Rais wa pili wa Marekani kuushika mkono wa kiongozi wa Cuba, katika kipindi cha miaka 60.  Mwaka 2000, Rais Bill Clinton alishikana mikono na kaka wa Raul ambaye alikuwa kiongozi wa Cuba wakati huo, Rais Fidel Castro.  Hilo lilitokea wakati wa mkutano wa Umoja wa Mataifa huko New York na Wamarekani wengi walitoa shutuma kutokana na mkono huo.

Tukio la Rais Obama kusalimiana kwa mkono na Raul Castro, liliripotiwa kwa kiasi kikubwa na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi.  Tukio hilo liliripotiwa kana kwamba lilikuwa jambo baya, hasa kutokana na Marekani kuishutumu Serikali ya Cuba ya tangu enzi za Fidel Castro, kwa matendo mengi yasiyofaa.  Cuba, licha ya kuwa jirani wa Marekani, ni mahasimu wakubwa wa nchi hiyo. Tangu enzi, Marekani imekuwa ikiishutumu Serikali ya Fidel Castro kwa utawala wa kimabavu na kuwafunga wapinzani wake wa kisiasa na kusababisha wengine kuikimbia nchi hiyo.

Mmoja wa watu hao ni baba wa Seneta Ted Cruz, Mhubiri Rafael Cruz.  Rafael Cruz alikuwa shabiki mkubwa wa Fidel Castro kwenye miaka ya 1950 na akiwa na miaka 17, aliongoza kundi la wapiganaji kupambana na dikteta Fulgencio Batista.  Hata hivyo, alikamatwa na kuteswa.  Alipotoka, alitamani sana kujiunga na kikundi cha waasi kilichokuwa kikiongozwa na Fidel Castro, lakini hakufanikiwa.  Baadaye aliamua kwenda Texas, nchini Marekani kusoma.  Aliporejea Cuba, alishangaa kuona kwamba Fidel Castro, ambaye wakati huo alikuwa kiongozi wa nchi hiyo, amejitangaza kuwa mkomunisti.  Hilo likasababisha awe mpinzani mkubwa wa Serikali ya Cuba na kuhamia kabisa Marekani.

Pengine hiyo ndiyo sababu ya Seneta Ted Cruz kunyanyuka na kutoka nje ya uwanja huko Pretoria, Afrika Kusini, wakati wa kumbukumbu ya Rais Nelson Mandela.  Mwenyewe alidai kwamba asingeweza kukaa pale kuisikiliza hotuba ya Rais wa sasa wa Cuba, Raul Castro, wakati kwa miaka mingi Castro amekuwa akiwafunga na kuwatesa raia wasiokuwa na hatia.

Lakini wakati Seneta Cruz akipigia kelele utawala wa Cuba katika kumbukumbu ya Rais wa Afrika Kusini, Waafrika walimshangilia kwa nguvu Rais Raul Castro alipokwenda kuhutubia na pengine wala hawakuligundua lile la Cruz, kwa sababu kwa Waafrika, Cruz si mtu wa kusimama na kutaka kujifananisha umaarufu ama heshima waliyonayo akina Castro.  Kwanza, wala hata hawajui Ted Cruz ni nani.  Kwa Waafrika, Mcuba wa kwanza wanayemfahamu ni Fidel Castro, ambaye ni rafiki wa Bara la Afrika.

Dunia inamtazama Fidel Castro kwa namna tofauti.  Wapo wanaomsifia kama kiongozi shupavu na mwenyewe ameshatunukiwa tuzo mbalimbali kutokana na ushupavu wake na kuifanikisha Cuba kuwa huru kutoka katika ‘ubeberu’ wa Marekani.  Ni kwa sababu hizo pia, Marekani na baadhi ya nchi washirika wa Marekani wanamshutumu Castro kwa utawala wa mabavu, kutozingatia haki za binadamu na kusababisha idadi kubwa ya Wacuba kuwa wahamiaji katika nchi zingine, kama ilivyo kwa akina Cruz.

Lakini kwa Bara la Afrika, Fidel Castro ni shujaa, mpiganaji, mwanamapinduzi na rafiki wa kweli.  Na hii ndiyo sababu ya Bara la Afrika kumlilia.  Kifo cha Castro kimewagusa Waafrika wengi, hasa wale wanaoijua historia ya ukombozi wa Bara la Afrika.  Msaada mkubwa alioutoa Castro kwa ajili ya ukombozi wa bara hili, hautakiwi kupuuzwa hata kidogo na wale wanaotushangaa.  Kusema kweli, sisi tunawashangaa wao kwa kutushangaa sisi tunaouenzi urafiki wa Castro katika harakati za ukombozi za bara hili.

Baada ya miaka 27 ya kifungo cha maisha, Nelson Mandela alihakikisha kwamba safari yake ya mwanzo kabisa za nje ya nchi itakuwa Cuba.  Alikwenda huko mwaka 1991 na kufurahia kukutana na Fidel Castro, na alimkumbatia na kummwagia sifa kede kede.  Mandela alimuita Castro kiini cha msukumo na tamanio kwa wapenda amani wote.

fidel-castro-welcomes-nelson-mandela-to-cuba-072791
Nelson mandela akiwa na Fidel Castro wakati wa uhai wao.

 

Pengine kauli hiyo ya Mandela ilitokana na ukweli kwamba baba huyo wa Afrika alishtakiwa kwa kuwa gaidi na kuhukumiwa kifungo cha maisha na Serikali ya kikaburu iliyokuwa ikishabikia ubaguzi mkubwa waliokuwa wakifanyiwa Waafrika.  Wakati huo, Serikali ya Marekani iliyokuwa chini ya uongozi wa Rais Ronald Reagan na Serikali ya Uingiereza iliyokuwa chini ya Waziri Mkuu Margareth Thatcher, zilikubaliana na Serikali ya kibaguzi ya Afrika Kusini.  Serikali hizo zilienda mbali zaidi na kumuita Nelson Mandela gaidi na mtu hatari sana.

Wakati huo huo, Fidel Castro aliamua kutoa majeshi kupambana na Serikali ya kikaburu, na mwaka 1988, kwa mfano, vikosi vya wanajeshi 36,000 wa Cuba vilishiriki kikamilifu kupambana na kuvishinda vikosi vya kikaburu vilivyokuwa vimejikita nchini Angola.  Mapigano hayo yalisaidia hata nchi jirani ya Namibia kupata uhuru kutoka kwa Afrika Kusini ya Kikaburu na yaliwahamasisha zaidi wapiganani waliokuwa wakipingana na utawala wa kikaburu.   Takribani askari 4,300 wa Cuba walipoteza maisha katika mapigano hayo ya Angola.  Kwa Kiswahili chepesi, askari hao wa Cuba walikufa wakipigania maisha bora na uhuru wa Waafrika.

Uhusiano wa Fidel Castro na Angola haukuishia hapo.  Licha ya vikosi vya askari, bado wataalamu mbalimbali kama vile walimu na madaktari waliendelea kubaki nchini Angola kwa miaka mingi, ili kusaidia kuijenga upya nchi hiyo na kuhakikisha kwamba haivamiwi.  Waangola wenyewe wanadai kwamba Castro alikuwa Mandela wa nchi yao.

Uhusiano wa Castro na nchi za Afrika unazungumzwa sana katika historia ya ukombozi wa bara hili katika miaka ya 1960 hadi 1980, ambapo askari waliofundishwa na Cuba walifanikiwa kuwaondoa Wareno katika nchi za Guinea-Bissau na Cape Verde, ambako walikuwa wakitawala.  Walipigana pia dhidi ya Mobutu Sese Seko, ambaye aliiongoza Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo), ambaye alimuua Waziri Mkuu wa kwanza wa nchi hiyo, Patrice Lumumba.  Vile vile, mwaka 1977, Castro alituma vikosi vya askari 17,000 kwenda kumsaidia kiongozi wa Kikomunisti wa nchi hiyo, Mengistu Haile Mariam.  Castro aliwahi kunukuliwa akisema kwamba takribani vikosi vya askari 400,000 vimetumika barani Afrika kwa kusaidiana “bega kwa bega na kaka zetu wa Afrika katika kuupata uhuru wao, ama kupinga ubepari wa Magharibi.”

Kutokana na sababu hizo na nyingine nyingi, haikuwa ajabu kwa viongozi wa Afrika kutoa matamko ya kuungana na wananchi wa Cuba katika majonzi ya kufiwa na kiongozi wao.  Haikuwa ajabu hata kwa Waafrika wengine wanaoijua vyema historia ya ukombozi wa bara hili, kumsifia Fidel Castro na kusema kwamba atakumbukwa daima.

Wakati Marekani, Uingereza na baadhi ya nchi zingine zikiwatuhumu watu kama Mandela kuwa magaidi, ni Fidel Castro pekee aliyeinuka na kulisaidia bara hili kujikomboa kutoka katika makucha ya ukoloni na ubaguzi wa kutisha.  Kwanini Waafrika tusimlilie?

Pumzika kwa amani Kamanda Fidel Alejandro Castro Ruz; alama uliyoiacha barani Afrika haitafutika kamwe!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles