23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

KWAHERI NA UPUMZIKE KWA AMANI SHAABAN DEDE

JIMMY CHIKA na CHRISTOPHER MSEKENA

MWIMBAJI mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Shaban Dede, amefariki dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu ya maradhi ya kisukari yaliyomsumbua kwa muda mrefu.

Mwanamuziki huyo ambaye pia alikuwa mtunzi tegemeo wa bendi ya Msondo Ngoma, alifikishwa hospitalini hapo wiki tatu zilizopita.

Akizungumza na MTANZANIA, mmoja wa watoto wa marehemu, Hamad Dede, alisema baba yake alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari uliosababisha matatizo kwenye figo, ini na mapafu yake kujaa maji.

“Amefariki majira ya saa mbili asubuhi ya leo (jana), mipango ya mazishi inafanyika nyumbani kwake Mbagala, Dar es Salaam na taratibu za kumpumzisha kwenye nyumba yake ya milele zinaendelea,” alisema Hamad.

Wimbo wa mwisho wa Shabani Dede enzi za uhai wake uliitwa ‘Suluhu Msondo’.

Mwandishi Jimmy Chika alimtembelea Jumapili ya Aprili 16, mwaka huu ambapo mvua kubwa ilikuwa ikinyesha siku hiyo katika Jiji la Dar es Salaam, lakini haikuwa kikwazo cha kufika kwa mwanamuziki huyo huko Mbagala Rangitatu, mkabala na shule ya Msingi Mbagala.

Eneo analoishi limepata umaarufu kutokana na kuwa karibu na familia ya mwanasoka maarufu Mbwana Samatta.

Siku hiyo Dede alikuwa mwenye nafuu hata kwa kumwangalia, aliamka mapema na kupata staftahi, lakini alisema chakula chake hakikuwa na ladha kwa vile alikuwa hatumii viungo kama chumvi wala sukari.

Hiyo imetokana na maagizo ya madaktari waliokuwa wakimtibu maradhi ya kisukari yaliyomsumbua kwa kipindi kirefu.

Alianza matibabu katika Hospitali ya Wakorea iliyopo eneo la Mtoni Mtongani jijini Dar es Salaam na kukosa kushiriki maonyesho mengi ya bendi yake, hakuwa akionekana jukwaani, kama ilitokea basi ni siku moja moja na hakuimba nyimbo nyingi kama ilivyo kawaida yake.

Alikuwa akiiumia sana kukosa maonyesho ya jukwaani kwani alikosa fursa ya kukutana na rafiki zake pamoja na mashabiki kwa ujumla.

Dede alidai ugonjwa wa kisukari ulikuwa ukimsumbua muda mrefu na umekuwa ukimzidi na kupungua na wakati mwingine ulimuweka chini, lakini kipindi hicho alichomtembelea alikuwa amezidiwa zaidi na ugonjwa huo.

Lakini licha ya kuwa na maumivu ya ugonjwa huo, lakini alionekana mwenye furaha na uchangamfu hasa walipozungumzia baadhi ya tungo zake, alijitahidi hata kuziimba.

Alimkumbusha kuhusu nyimbo zake na hata matamshi mbalimbali aliyofanya mbele ya Rais Jakaya Kikwete wa Awamu ya Nne na John Pombe Magufuli wa Awamu ya Tano, alivyokuwa akipiga tumba wakati yeye alipokuwa akiimba.

Hakufikiria kifo wakati wote alisema anapata ahueni. Lakini siku kadhaa alizidiwa tena na kukimbizwa Muhimbili ambapo alilazwa hadi mauti  yalipomkuta.

Ingawa madaktari walionekana kutumia kila maarifa yao kwa ajili ya kuirudisha afya yake katika siha njema, lakini hali ya ugonjwa kwa mkongwe huyo aliyeanza kuimba tangu mwaka 1974 ilionekana kuzidi kuzorota.

Siku kadhaa taarifa za uzushi zilizagaa kwamba amekufa wakati alikuwa hai. Zilikuwa taarifa za kushtusha na kulaaniwa kila kona.

Mwanamuziki huyo alipitia bendi mbalimbali kuanzia 1974 ikiwemo Tabora Jazz, Dodoma International, mwaka1980 alihamia Msondo Ngoma, mwaka 1982 alihamia Mlimani Park Sikinde.

Bendi nyingine ni Bima Lee aliyohamia mwaka 1984 ambako alianzisha mtindo wa Magnet Tingisha, mwaka 1986 alihamia Oss Ochester kwa vipindi tofauti lakini baadaye alirudi Mlimani Park na kisha miaka mitatu iliyopita alirudi tena Msondo Ngoma hadi mauti yalipomkuta.

Mtanzania tunaiombea roho yake ipate pumziko la milele, Amina.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles