33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Kwaheri mzee Apson

Mwandishi wetu -Dar es salaam

MKURUGENZI Mkuu mstaafu wa Usalama wa Taifa (TISS), Apson Mwang’onda (75), amefariki dunia nchini Afrika Kusini alikokuwa akitibiwa.

Akithibitisha kutokea kwa msiba huo, mtoto mkubwa wa marehemu, Thomas Mwang’onda, alisema baba yao alipatwa na mauti jana majira ya saa 5 asubuhi.

“Ni kweli mzee ametutoka na inaumiza kupoteza mzazi, ilikuwa kwenye saa tano asubuhi wakati wadogo zangu wanamsindikiza mama kwenda Airport wakapigiwa simu kuwa warudi haraka hospitali. Na walipofika walikuta tayari mzee amefariki.

“Kwa sasa msiba upo nyumbani Mbezi Beach, ila kesho ndio tutajua utaratibu wa namna ya kuuleta mwili wa mzee hapa nyumbani kwa taratibu za mazishi,” alisema.

Thomas ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, alisema kuwa wakati wa uhai wake, baba yao aliwahi kufanya kazi katika maeneo mbalimbali nchini.

“Mwenyewe baba huwa nakaa naye ambapo hupata nafasi ya kunihadithia maeneo kadhaa ambayo alifanya kazi. Nakumbuka aliniambia kuwa aliwahi kufanya kazi Shirika la Mafuta la wakati huo la TP, pia alikuwa JKT katika kambi ya Kaboya mkoani Kagera na baada ya hapo alikuwa mkuu wa kambi ya JKT Mgulani ambako hapo ndipo jicho la Serikali lilimuona zaidi na kumpa kazi nyingine hadi anastaafu,” alisema.

Septemba 5, mwaka huu Rais Dk. John Magufuli alimjulia hali Mwang’onda, ambaye alikuwa akipatiwa matibabu hospitali Dar es Salaam.

Hata hivyo hali ya mzee Apson ilibadilika na familia kwa kushirikiana na Serikali iliamua apatiwe matibabu nchini Afrika Kusini kutokana na maradhi yaliyokuwa yakimsumbua.

ALIPOKUTANA NA MAGUFULI

Desemba 6, 2018 Rais Magufuli alikutana na kufanya mazungumzo na Apson, Ikulu Dar es Salaam.

Baada ya mazungumzo hayo Apson alimshukuru Rais Magufuli kwa kukubali ombi lake la kumuona.

Pia alipongeza uongozi wa Rais Magufuli kwa kuchochea kasi ya maendeleo, hususani katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.

Apson aliitaja baadhi ya miradi mikubwa ya maendeleo kuwa ni mradi wa uzalishaji wa umeme wa Julius Nyerere katika Mto Rufiji, ujenzi wa madaraja na barabara ambazo licha ya kurahisisha usafiri zitasaidia kuondoa msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam.

“Mabadiliko ni makubwa sana ambayo yametokea, kuna miradi mikubwa mingi inafanyika sasa hivi, kwa hiyo mabadiliko ni makubwa kusema kweli na yote hayo ni kwa manufaa ya nchi. Kwa hiyo ninachoweza kusema amefanya kazi kubwa kwa maendeleo ya nchi,” hiyo ndiyo iliyokuwa kauli ya Apson hadharani katika mkutano wake na Rais Magufuli

Alistaafu Agosti 21, mwaka 2006 kwa mujibu wa sheria na nafasi yake aliteuliwa Rashid Othman, ambaye naye alistaafu rasmi Agosti 19, mwaka 2016.

Apson ni Mkurugenzi Mkuu wa nne wa Usalama wa Taifa kushika nafasi hiyo kwa muda mrefu akiwa amekaa kwa miaka kumi (1995-2005).

Hadi sasa anayeshikilia rekodi ya kukaa katika nafasi hiyo muda mrefu zaidi ni Emilio Mzena aliyetumikia miaka 15   kutoka mwaka 1961 hadi 1975.

Wa pili ni Luteni Jenerali Imrani Kombe aliyekaa miaka 12 kutoka mwaka 1983 hadi 1995 na wa tatu ni Othman Rashid aliyekaa miaka 11 kutoka mwaka 2005 hadi 2016.

WALIOWAHI KUONGOZA USALAMA

Kwa miaka kadhaa idara hiyo iliongozwa na vigogo waliobobea katika masuala la ulinzi na usalama, wakiwamo Mzena, Lawrance Gama na Hans Kitine ambaye alipoondoka nafasi hiyo ilikamatwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Augustine Mahiga.

Mbali na hao, nafasi hiyo ilishikiliwa pia na Kombe, Mwang’onda na Othman.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles