27 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

KWA HERI KAMANDA MSANGI, KARIBU SHANNA

Na CLARA MATIMO



AgostiI 15, mwaka huu, Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Simon Sirro, alifanya mabadiliko ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi pamoja na mwenzie wa Mkoa wa Pwani, Jonathan Shanna.

Katika mabadiliko hayo, Msangi amekuwa Mkuu wa Kitengo cha Makosa Dhidi ya Binadamu Makao Makuu ya Upelelezi Dar es Salaam na nafasi yake ikachukuliwa  na Kamanda Shanna.

Mabadiliko haya yamefanywa wakati ambao wakazi wengi wa Mkoa wa Mwanza wakiwa wana imani na Kamanda Msangi ambaye kwa kiasi kikubwa aliweza kuwakabili watu waliokuwa wamezoea kujipatia fedha kwa njia zisizo halali hasa kujihusisha na vitendo vya uhalifu.

Kamanda Msangi wakati anaanza kutekeleza majukumu yake mkoani hapa, alipokelewa na vitendo kadhaa vya  uhalifu vilivyokuwa vikifanywa na baadhi ya watu ikiwemo  kujipatia fedha kwa kufanya uvamizi katika maduka na vibanda vya wajasiriamali na wafanyabiashara wanaotoa huduma za kibenki  kupitia mitandao mbalimbali ya simu za mkononi pamoja na  utekaji wa waendesha bodaboda.

Jambo jingine alilolifanya Kamanda Msangi ambalo binafsi nampongeza sana na daima nitamkumbuka kwa hilo, ni kupambana na majambazi ambao walikuwa wameweka ngome katika eneo la mapango ya Mlima wa Utemini, Kata ya Mkolani.

Mapambano baina ya vikosi vya usalama vilivyokuwa na bunduki za kivita dhidi ya majambazi hayo Juni 4 tangu saa 11 jioni hadi alfajiri Juni 5, mwaka 2016, ndiyo chimbuko la tashtiti ya wakazi wa Mwanza.

Nakumbuka katika mapambano hayo, bunduki aina za SMG zenye namba za usajili 307039, KH 347818 ikiwa na magazine nne zilizojaa jumla ya risasi 120 huku nyingine 24 zikiwa zimefungwa kwenye kitambaa,  zilikamatwa pamoja na vifaa vingi vilivyokutwa katika mapango  hayo yanayoonekana yalikuwa ni makazi ya muda mrefu ya majambazi hao.

Lakini Msangi aliweza kuwasambaratisha majambazi wote waliokuwa wakitumia eneo hilo kama maficho yao kwa ajili ya kufanya uhalifu  na wakazi wa  kata hiyo pamoja na mkoa huo, sasa wanaishi kwa amani hakuna tena bughudha yoyote.

Wengine walijihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya, lakini hakuna aliyeweza kukwepa mkono wa sheria  kwani nilishuhudia kila mara wakikamatwa na kufikishwa mahakamani, huku baadhi yao waliojaribu kupambana na askari polisi, walidhibitiwa na kuuawa.

Kamanda Msangi akishirikiana na watendaji wenzie wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, alitangaza kuanza kutumia kikosi cha mbwa waliopewa mafunzo maalumu ya kubaini dawa za kulevya ambazo  zimefichwa eneo lolote ili kuwakamata watu wanaojihusisha na biashara hiyo haramu.

Lengo lake lilikuwa ni kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano kwa kudhibiti uingizwaji, uuzwaji na utumiaji wa dawa hizo haramu ambazo zinapoteza nguvu kazi ya Taifa nchini.

Alipokuwa akizindua mpango huo, alisema utakuwa na tija kwa sababu mbwa hahongeki, hivyo akikamata dawa za kulevya lazima mhusika atabainika na kufikishwa mbele ya vyombo vya  sheria,  tofauti na askari polisi maana si wote waaminifu yawezekana wapo baadhi ambao huwakamata watu wanaojihusisha na biashara hizo haramu lakini huwaachia baada ya kupewa rushwa.

Haya ni baadhi ya mazuri ambayo Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Msangi aliyafanya ndani ya Mkoa wa Mwanza, naamini kiu ya wananchi wengi wa mkoa huo ni kuona jitihada kama hizo zikifanywa na aliyerithi mikoba yake, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP)  Shanna.

Binafsi sina mashaka na utendaji wa ACP Shanna ambaye akiwa na siku moja tu tangu akabidhiwe ofisi na mtangulizi wake, DCP Msangi Agosti 27, mwaka huu, Agosti 28 aliwafukuza kazi askari wawili wa jeshi hilo mkoani humo kwa kosa la kukutwa na nyara za Serikali, vipande viwili vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilogramu 20.

Kilichonifurahisha ni pale alipowataka wale wote waliokuwa wakishirikiana na askari hao kufanya biashara hiyo haramu, kujisalimisha kituo chochote cha polisi kilicho karibu yao, vinginevyo watambue kwamba watawakamata tu kwani wana mbinu zote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles