24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Kuwarudisha wagombea upinzani si suluhisho, dawa ni kuondoa dosari

JANETH MUSHI-ARUSHA

WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleiman Jaffo, amewarejesha wagombea wote wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao walichukua fomu za kurejesha.

Anasema kuwa mamlaka ya uchaguzi inawatambua wagombea wa vyama vya upinzani vilivyotangaza kujitoa kwenye uchaguzi huo na kuwa hata kama chama chake kimetangaza kujitoa lazima watapigiwa kura.

Wakati Waziri huyo akitangaza uamuzi huo, baadhi ya vyama vya upinzani ikiwamo Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),

ACT-Wazalendo ni baadhi ya vyama vilivyojitoa kushiriki uchaguzi huo kwa madai ya kutokuridhika na mchakato wake.

Akitangaza uamuzi wa chama hicho kutokushiriki uchaguzi huo mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, aliwataka wagombea wake waliochezewa rafu kuacha kukata rufaa.

 Anadai  kuendelea kushiriki uchaguzi huo ni kuhalalisha ubatili na kudai asilimia 85 ya wagombea wao nchi nzima wameenguliwa.

Wakati vyama hivyo viwili vikijitoa,vyama 11 vya upinzani visivyo na uwakilishi katika Bunge la Tanzania vimetangaza kushiriki uchaguzi huo vikidai “anayesusa chakula kashiba”.

Vyama hivyo ni DP, NRA, AFP, Demokrasia Makini, UDP, ADC, Ada-Tadea, Sauti ya Umma(Sau), TLP,CCK na UMB, vikidai vinaamini Tamisemi ambayo ndiyo husimamia uchaguzi huo itatenda haki na kuwarejesha wagombea waliotenguliwa kushiriki uchaguzi huo.

Siku  moja baada ya Chadema kujitoa kwenye uchaguzi huo, kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, naye alitangaza chama hicho kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho.

Uamuzi huo ulitolewa baada ya kamati ya uongozi ya chama hicho Taifa kukutana na kujadili mwenendo wa uchaguzi huo ambapo alidai ni asilimia sita pekee ya wagombea wa chama hicho walikuwa hawajaenguliwa.

Baada ya vyama hivyo kujitoa kushiriki uchaguzi huo wa sita wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24 mwaka huu, Waziri Jaffo alidai kushangazwa na uamuzi huo na kuwa unawanyima fursa wagombea wa chama hicho waliopitishwa na waliokata rufaa kupinga kuenguliwa.

Waziri huyo alikiri kuwapo kwa baadhi ya fomu zenye makosa kiatika kujazwa ila kujiondoa kwa chama hicho wakati mchakato wa rufaa ukiendelea kunawakosesha haki wagombea wao hasa wa maeneo ya vijijini waliokata rufaa.

Kutokana na dosari zilizojitokeza katika mchakato wa uchaguzi huo ni vema sasa pande zote kukaa katika meza ya mazungumzo ili kuweza kupata suluhisho ya kudumu.

Tamisemi ambao ndiyo wasimamizi wa uchaguzi huu wanapaswa kuangalia kwa jicho la pekee changamoto zilizojitokeza katika uchaguzi huu na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu ikiwamo kuhirikiana na wadau wengine kukaa na vyama vyote vya siasa na kuangalia wapi pa kufanyia marekebisho.

Ni wazi kuwa licha ya Jaffo kutangaza kurejesha wagombea wote waliochukua na kurejesha fomu hizo ikiwamo wa vyama vya upinzani, bado kufanya hivyo siyo suluhisho la tatizo hilo bali ni kukaa meza ya pamoja, kujadiliana na kufanya mchakato huo kwa mujibu wa kanuni na taratibu.

Aidha, Tamisemi inapaswa kuangalia madai ya vyama vilivyojitoa kushiriki katika uchaguzi huo na kuyashughulikia ili changamoto zilizojitokeza na kusababisha mvutano mkali zisiweze kuathiri  mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa mwakani.

Licha ya kuwa hii siyo mara ya kwanza kwa baadhi ya vyama vya upinzani ikiwemo Chadema kujitoa katika chaguzi ikiwemo chaguzi ndogo za ubunge zilizofanyika miaka ya hivi karibuni,kutokana na umuhimu wa uchaguzi huu ni muhimu makubaliano kufikiwa.

Ni mtazamo wangu kuwa kutokana na dosari hizi zilizojitokeza katika uchaguzi huu zinaweza kupunguza hamasa ya wananchi kushiriki katika chaguzi mbalimbali ikiwemo uchaguzi huu ambao ni muhimu sana kwani unawaweka madarakani viongozi wa ngazi za jamii(vitongoji,vijiji na mitaa).

Baadhi ya changamoto ambazo zinalalamikiwa  ni pamoja na figisu zilizojitokeza wakati wa zoezi la kuchukua,kurejesha fomu za wagombea pamoja na uteuzi wa wagombea hao.

Baadhi ya sababu zinazodaiwa kuwakosesha sifa wagombea wa vyama hivyo na kuenguliwa  kuwania nafasi mbalimbali ni pamoja na kudaiwa kukosea kujaza fomu zao hivyo wengi wao kulazimika kukata rufaa.

Yapo maswali mengi unaweza kujiuliza,wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliochukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali kote nchini wameteuliwa kuwania nafasi hizo,je wao wameweza kuzingatia kanuni na miongozo yote ya jinsi ya kujaza fomu halafu wa upinzani wakashindwa kujaza?

Ni wazi kuwa hoja hiyo inaibua maswali mengi yasiyo na majibu, kwani haiwezekani chama kimoja kiweze kujaza fomu kwa usahihi kwa kuzingatia kanuni na miongozo halafu vyama vya upinzani ambavyo pia siyo mara yao ya kwanza kushiriki uchaguzi huo washindwe.

Ni mtazamo wangu kuwa wasimamizi wa uchaguzi kutekeleza majukumu yao kwa kufuata kanuni,taratibu na sheria katika uchaguzi huu ili kutokuathiri uchaguzi wa mwakani.

Awali Waziri Jaffo alieleza kuwa ameshatoa maelekezo kwa wasimamizi wa uchaguzi huo kufungua vituo kwa muda unaotakiwa ili kuwawezesha wagombea kupata haki yao ya msingi ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu hizo lililoanza Oktoba 29 na kukamilika Novemba 4 mwaka huu.

Wakati waziri huyo akisema hayo alikiri kuwapo kwa malalamiko kwa baadhi ya maeneo ikiwemo baadhi ya wasimamizi wasaidizi wamekuwa wakifunga vituo huku kwingine kukilalamikiwa kuwepo kwa vitendo vya uvunjifu na vurugu.

Kila mmoja akitimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria,watasaidia kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani,kutokuenenda kinyume na yanayotakiwa katika uchaguzi huo na kutenda haki ili kupunguza malalamiko na dosari zinazoepukika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles