27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Kutengeneza kucha: Ajira inayowaweka majaribuni vijana

kucha mojaNA RAMADHAN HASSAN, DODOMA

ENEO la Nyerere Square lililopo mkoani Dodoma ni maarufu mno kwa sababu ya kuwapo kwa sanamu ya Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere.

Mbali ya kuwa na sanamu hiyo, pia ni eneo la kibiashara ambapo kuna biashara za kila aina, kama za kuuza vocha na upigaji picha.

Pia kuna soko ambalo hufunguliwa nyakati za jioni tu ambapo hupatikana nguo, vito na viatu huku wauzaji wengi wakiwa ni vijana kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dodoma.

Biashara nyingine kubwa inayofanyika katika eneo hilo ni ile ya kupaka rangi, kubandika kucha pamoja kuosha miguu huku wateja wakiwa ni kina dada na akina mama kutoka maeneo mbalimbali.

Mwandishi wa makala haya anaamua kufunga safari mpaka katika eneo hilo na kufanya mahojiano na wafanyabiashara.

Dennis Batholomeo, anasema ameamua kujiajiri katika biashara ya kubandika kucha na kupaka rangi kutokana na ugumu wa maisha uliokuwa nyumbani kwao na kwamba kwa siku huwahudumia watu 20 mpaka 25.

“Mimi nimetoka Babati mkoani Manyara, hii biashara niliianzia Babati baadae ndio nikaja hapa Dodoma. Kwa siku huwa natengeneza watu zaidi ya 20,” anasema Batholomeo.

Anasema katika maeneo hayo biashara kubwa inayofanyika ni ya kubandika kucha, kuchora kucha pamoja na kuosha miguu kwa kina dada na kaka.

Anasema bei za kubandika kucha ni kati ya Sh 10,000 hadi 15,000 wakati kupaka rangi ni kati ya Sh 3,000 hadi 5,000 na kuosha miguu na mikono ni kati ya Sh 5,000 hadi 10,000.

“Kwa siku kipato chetu ni kuanzia Sh 80,000 na kuendelea, ila kipato huwa kinakuwa kikubwa siku za mwisho wa wiki kutokana na watu kuwa wengi,” anasema.

Naye Musa Kitoti anasema biashara ya kuchora kucha imemsaidia kujikwamua kimaisha kwa kuwa sasa anaweza kumsomesha mdogo wake aliyeko Kigoma.

“Nimetokea Kigoma, nilipokuwa shule nilikuwa na kipaji cha kuchora na leo kipaji hiki kimenisaidia naweza kubandika kucha vizuri pamoja na kupaka rangi.

“Nilikuwa na maisha magumu lakini sasa hivi nashukuru fedha ya kula haisumbui na mdogo wangu anaenda shule kutokana na kazi hii,” anasema Kitoti.

Naye Yohana Jackson, anasema ametoka mkoani Ruvuma kwa ajili ya biashara hiyo baada ya kushawishiwa na rafiki yake kuwa biashara hiyo inalipa mkoani Dodoma.

“Kuna rafiki yangu alikuja likizo mwisho wa mwaka akaniambia twende Dodoma biashara ya kubandika kucha na kupaka rangi inalipa, mimi sikujivunga niliamua kuja.

“Mwanzo nilikutana na changamoto nyingi lakini sasa hivi nimezoea, nimeoa na nina mke na watoto wawili ambao wana uhakika wa kusoma pamoja na kula kila siku kutokana na biashara hii,” anasema.

Anasema kwa siku huhudumia wateja kati ya 20 mpaka 30 kwa kupaka kucha, kuosha miguu pamoja na kubandika kucha katika mikono na miguu.

Kwa upande wake Lazaro Ikoa anasema biashara yao imekuwa kubwa kutokana na kuwapo kwa wanafunzi wengi.

Wanafunzi hao wanatoka katika vyuo vifuatavyo; Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo cha Mipango, Chuo Kikuu cha Mtakatifu John, Chuo cha Tamisemi Hombolo, Chuo cha Ualimu cha Capital na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).

“Wateja wetu wengi ni kina dada hasa wa vyuo vikuu ila wanaume wanakuja baadhi kuosha miguu,” anasema.

Anasema biashara hiyo imeweza kumsaidia kuendesha maisha tofauti na ile ya mwanzo aliyokuwa akifanya ya kupiga picha.

“Zamani nilikuwa napiga picha, maisha yalikuwa kidogo magumu kwa sababu ilikuwa mpaka nisafishe ndio nipeleke kwa mteja tofauti na biashara ya kucha ambapo ukimaliza unapewa chako hapo hapo,” anasema.

Kwa upande wake Thabit Rajabu, anasema alianza biashara hiyo miaka sita iliyopita huku kazi yake kubwa ikiwa ni kubandika kucha.

“Nabandika kucha za kila aina, kuna fupi na ndefu… wateja wangu ni wanafunzi. Hapa huwa sikai sana kutokana na kupigiwa simu niwafuate huko vyuoni.

“Simu yangu ndio ofisi wateja wangu ni wanafunzi hivyo wanapeana namba zangu,” anasema Rajabu.

Anasema kupitia kazi yake hiyo ameweza kujenga nyumba pamoja na kutatua kero mbalimbali za fedha katika familia yake.

“Nyerere Square ni eneo muhimu kwetu na maisha yetu yanakwamuka kimaisha kupitia eneo hili, wakati mwingine unasema asante Mungu kwa kipaji hiki,” anasema.

kucha tatu Changamoto        

Richard Babisha anasema changamoto kubwa wanayokutana nayo ni wanawake kuacha wazi baadhi ya maumbile yao kama vile mapaja hivyo kuwa na wakati mgumu pindi wanapowahudumia.

“Wanawake wanaokuja hapa ni wazuri nadhani na wewe unawaona, sasa wakati wa kumpaka rangi unaweza kukuta kavaa kimini halafu miguu anaiweka kwenye mapaja yako.

“Tunapata wakati mgumu lakini kwa sasa tumeshazoea unaangalia na maisha yanaendelea…hatujali kwa sababu ndiyo kazi tuliyochagua,” anasema Babisha.

Naye Idrisa Kadiri anakwenda mbali zaidi na kusema wateja wengine hufanya hivyo kama kigezo cha kupatiwa huduma bure.

“Wengine wanakuachia mapaja wazi ili umtengeneze bure, tabia hiyo mimi nilishaifahamu, nina taulo langu kubwa nikiona niaachiwa mapaja basi namfunika na taulo ili nisione.

“Lakini wengine hata ukiweka taulo wanakuwa hawataki uwafunike, wanakwambia angalia tu mimi nataka unipendezeshe ili mwenzi wangu akanisifie,” anasema Kadiri.

Anasema changamoto nyingine ni wateja hasa wanaotoka vyuoni kwenda bila ya kuwa na fedha huku wakiahidi kuwalipa pindi watakapopata.

“Unaweza kukuta dada anakuja anakwambia nitengeneze, unamtengeneza ukimaliza anakwambia njoo chuoni kwetu. Ukimwambia mimi siji anakwambia kwani hakuna ulichopenda katika mwili wangu ili nikuachie, unajikuta unacheka tu,” anasema huku akicheka.

Naye Juma Ibrahim anasema amefanya kazi hiyo kwa muda mrefu hadi kufikia kuwekwa ndani na mteja wake aliyemtaka kimapenzi.

“Ni mama mtu mzima kidogo alinipenda kutokana na hii biashara yangu ya kucha, tukaishi vizuri lakini tulikuja kushindwana kwani alikuwa na mambo mengi.

“Wanawake wengi wanaokuja hapa ni wazuri kuliko hata uzuri tunaousema hivyo nawaasa vijana wenzangu tuwe makini kuna Ukimwi.

“Mavazi wanayovaa ndiyo mtihani mkubwa na kulingana na mtindo wa kazi yetu mteja anakuwa juu kidogo halafu mimi nakuwa chini kwahiyo kila kitu kinakuwa kipo wazi (akimaanisha maumbile).

“Tukio ambalo sitalisahau katika maisha yangu kuna dada wa UDOM alinipigia simu niende nikambandike kucha pamoja na kumchora, aliniambia niende saa 4 asubuhi katika chumba chake na nilipokwenda nilimkuta yupo peke yake hivyo tukawa wawili tu.

“Nilimkuta kajifunga kanga tu lakini nilipoanza kumchora akapandisha kanga juu zaidi, kumbuka ndani alikuwa hajavaa kitu huku akiwa ananikazia macho machoni, nilipomwambia vaa nguo vizuri alikataa.

“Niligoma kuendelea kumchora nikaamua kurudi zangu kijiweni, alinitukana akaniambia mimi ni mshamba na vitu vizuri nitakuwa nikila kwa macho tu,” anasema.

Ibrahimu anaiomba serikali kuwatafutia eneo maalumu ili waweze kufanya kazi zao kwa uhuru pamoja na kupata mikopo.

“Hapa tupo juani tu tena hatuna umoja, tunaiomba serikali itusaidie tupate eneo na mikopo ambayo itatusaidia,” anasema.

Neema Richard ambaye ni mwanafunzi wa kozi wa Udaktari kutoka Chuo cha Mtakatifu John kilichoko Dodoma, anasema kila mwisho wa wiki ni lazima aende katika eneo la Nyerere Square kuchonga kucha pamoja na kuchora.

Anasema mpenzi wake anavutiwa zaidi na kucha nzuri pamoja na miguu laini hivyo huwatumia vijana wa eneo hilo kumtengeneza.

“Mimi natokea Mtwara nikienda likizo huwa sifurahi kwa sababu hakuna wenye uwezo wa kuchora na kuchonga kucha kama hapa Dodoma na mpenzi wangu huwa anavutiwa na jinsi ninavyopendeza,” anasema Neema.

Naye Shekha Shally ambaye alikutwa na Mwandishi wa makala haya akitengeneza kucha katika eneo hilo, anaiomba serikali iwatafutie eneo maalumu vijana hao ili waweze kutambulika kisheria.

Kauli ya Serikali

Kwa upande wake Ofisa Biashara wa Mkoa wa Dodoma, Prisca Dugilo, anasema nia ya serikali ni kuwasaidia watu wote walioamua kujiajiri hivyo watawasaidia vijana hao kwa kushirikiana na Manispaa ya Dodoma.

Anasema kazi yake ni kusimamia sera, taratibu, sheria na maagizo hivyo anawakumbusha vijana hao kutafuta leseni za kufanyia biashara ili waweze kutambulika kisheria.

“Tunataka Dodoma ipae kiuchumi na vijana wale wanafanya kazi nzuri, hivyo tutaendelea kuwapa ushirikiano pamoja na wajasiriamali wengine wote,” anasema Prisca.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles