33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Kutekwa Mo bado utata

NORA DAMIAN Na KHAMIS SHARI-DAR es salaam/ Z’BAR


KUTEKWA kwa mfanyabiashara Mohamed Dewji, kumeendelea kuzua utata baada ya Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Godbless Lema, kudai eneo ambalo alitekwa, kuna ulinzi wa hali ya juu hivyo kushangaa kutopatikana kwake hadi sasa.

Dewji maarufu kwa jina la Mo alitekwa nyara na watu wasiojulikana alfajiri ya Alhamisi iliyopita katika Hoteli ya Colosseum iliyo Oysterbay ambako amekuwa akienda kufanya mazoezi ya mwili (Gym).

Akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Chadema Dar es Salaam jana, Lema ambaye pia ni Mbunge wa Arusha Mjini, alisema Oysterbay ni eneo ambalo wanakaa viongozi mbalimbali na kuna kamera za ulinzi (CCTV) ambazo zingewezesha kuwajua waliofanya tukio hilo.

“Ni ngumu kujua Mo ametekwa kwa sababu gani, lakini zawadi iliyotolewa na familia inadhihirisha hakuna watekaji ambao wamejitokeza kutaka fedha.

“Tunajiuliza hawa wangekuwa ni watekaji wa kawaida kazi ya kuteka ni ngumu sana kuliko kazi ya kushambulia na kuondoka. Maana yake utaanza kumtunza.

“Unajiuliza ni watekaji gani hao wanakaa na mtu zaidi ya wiki moja, na hao watu wamefanya tukio Oysterbay mahali ambako ni jirani na nyumba za viongozi na kuna ulinzi wa kutosha,” alisema Lema.

Mbunge huyo pia alitilia shaka uchunguzi wa tukio hilo na kuitaka Serikali iruhusu wachunguzi huru kutoka nje.

“Waziri Lugola (Kangi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi) aliongea na vyombo vya habari akidai utekaji si jambo linalotokea Tanzania tu na kuhoji kwanini kelele zimekuwa nyingi sana. Anapopotea mtu kama huyu unatarajia Serikali iwe ‘sensitive’ kupita kiasi.

“Wanaposema upelelezi unaendelea halafu tunaambiwa waliomteka ni raia wawili wa kizungu na ambao wanaendelea kutafutwa, unapata mashaka sana, kwanza mahali tukio lilipotokea.

“Kusema ni wazungu hapa ndio mashaka makubwa yalipo. Ukimpa dada Sh milioni moja aende saluni atakuja anaonekana kama Mzungu.

“Siku hizi kuna nywele zinaitwa Peruvian, sijui Brazilian, mpe mke wako Sh milioni moja aende saluni, atakuja na nywele tofauti, kope tofauti na mdomo tofauti kabisa, labda ni wazungu wa namna hiyo,” alisema.

Lema pia aligusia matukio ya kupotea kwa aliyekuwa Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Ben Saanane, Mwandishi wa Habari wa Mwananchi, Azory Gwanda na kushambuliwa kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na kusema matukio hayo yanazidi kuichafua nchi.

“Wakati wa tukio la Ben Saanane chama chetu kiliomba kuleta wapelelezi wa kimataifa waje wasaidiane na Serikali, lakini tulizuiwa.

“Tukio la Lissu kuna mataifa yalikuwa tayari kugharamia wachunguzi wa kimataifa, lakini walizuiwa.

“Marekani pamoja na ujuaji wake wa teknolojia kuna wakati wanapata matatizo wanaomba msaada kwa majirani zake.

“Ninaamini familia ya Mo ina uwezo wa kulipia ‘private investigators’ kutoka taifa lolote duniani kuja kusaidiana na Serikali kutafuta nani amefanya jambo hili baya.

“Kwa mazingira yanavyoonyesha wakiletwa Scotland Yard, siku tatu tu watakuambia ametekwa kwa sababu gani na kama yuko hai,” alisema.

Alisema kuruhusu wachunguzi huru hakumaanishi kwamba Serikali inahusika katika tukio hilo bali kutasaidia kuondoa mashaka miongoni mwa jamii.

“Kuhitaji msaada wa kiupelelezi si ‘weakness’, ni busara tu kwa ajili ya kutoa ‘confidence’ na kuonyesha ‘credibility’ dhidi ya utawala kwa sababu mambo haya yanaichafua nchi.

“Serikali isione aibu kuungana na taasisi za kimataifa, na ikiruhusu iruhusu pia kwa Ben Saanane, Azory Gwanda na Lissu.

“Kwanini wanataka kumuharibia rais wetu mtukufu? Wangemshauri rais tulete watu wenye uzoefu wa kiuchunguzi,” alisema.

Hata hivyo waziri huyo kivuli alishauri vyombo vya dola viruhusu picha za CCTV siku ya tukio hilo zionyeshwe kwenye vyombo mbalimbali vya habari ili iwe rahisi kuwatambua wahusika.

“Ni utamaduni duniani kote kwamba linapotokea tukio kama hili ziko kumbukumbu za kamera na hata ukiangalia FBI Marekani na Scotland (Yard) Uingereza, wanavyofanya huwa wanaruhusu ziende kwenye vyombo mbalimbali vya habari duniani ili wananchi wanaoombwa msaada wa kuwatafuta wasiojulikana waweze kumtambua mtu kirahisi,” alisema.

Alisema suala la kutekwa kwa mfanyabiashara huyo, linaweza kuathiri uchumi wa nchi kwa kile alichodai kuwa wafanyabiashara na wawekezaji wataingiwa na hofu ya kuendelea kufanya biashara nchini.

“Jambo hili lina impact kubwa kwenye uchumi, habari hizi zimeenea maeneo mbalimbali duniani.

“Uchumi utashuka kwa sababu watu wataondoka, wenye mitaji wataondoa mitaji yao na kwenda nchi nyingine, kwa sababu matukio yamekuwa ya mfululizo, mtu yeyote mwenye akili timamu ambaye ana mtaji atakwenda sehemu nyingine mbalimbali,” alisema Lema.

Alidai baadhi ya kampuni zimeanza kuwa na matawi Uganda, Msumbiji na kwingineko na kutahadharisha kuwa masuala ya utekaji yasipopatiwa suluhu watu watazidi kuingiwa hofu na kukimbia.

Katika hatua nyingine, mbunge huyo ameshauri watu wasizuiwe kujadili suala hilo.

“Badala ya wananchi kuruhusiwa kupiga kelele ipatikane ‘solution’ ya mambo haya, wanazuiwa wasijadili kwenye mitandao na hadharani.

“Viongozi wa dini, taasisi za viwanda zitoke hadharani zipige kelele kwa sauti. Watu wanapotea lakini huoni ‘seriousness’ ya hili jambo kama linachukuliwa ni jambo muhimu sana.

“Sasa kama Mo anaweza akapotea hivi ni nani ambaye yuko salama?

“Mama yangu alinipigia simu na dada yangu wakaniambia nisiongee, kama kuna miongoni mwetu binadamu atapotea halafu sisi tukaona ni busara kukaa kimya kwa sababu ya kulinda uhai wetu, tunapaswa kulinda uhai kabla ya kulinda chochote kile.

“Hata kama nisingekuwa Waziri Kivuli, niko tayari na wala siogopi najua siku moja nikitekwa mimi ama akatekwa mke wangu kuna watu watapiga kelele.

“Mimi ni mbunge nimejitwisha jukumu la kumtafuta Mo kama mwanasiasa na rafiki yake na kama chama kikuu cha upinzani, lazima tuwe na wajibu kuhakikisha haya mambo yanapotea.

“Kesho atatekwa Mbowe,  nitatekwa mimi haya mambo lazima yapigiwe kelele.

“Nimekaa bungeni miaka mitano na Mo, maombi yangu awe hai na aachiwe huru na hao watekaji kama wanasikia Kiswahili naomba sana wamwachie,” alisema Lema.

 

SERIKALI

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yusuph Masauni, alisema Serikali haiwezi kuruhusu wapelelezi binafsi kuja kuchunguza tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara huyo kwa sababu vyombo vya ndani bado viko imara.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Unguja, Zanzibar jana, alisema dhamira ya Serikali ni kuliwezesha Jeshi la Polisi kuweza kupata vifaa vya kisasa kufanya kazi zao kwa ufanisi.

“Kama kuna mtu yeyote ambaye anataka umaarufu wa kisiasa kwa kujenga propaganda kwamba vyombo vyetu haviwezi kufanya kazi tuite wapelelezi kutoka nje, hoja hiyo ni dhaifu na haiwezi kukubalika.

“Tuna jeshi imara ndiyo maana nchi yetu iko salama mpaka sasa. Usalama huu tulionao kwa zaidi ya miaka 50 sasa ni kutokana na jeshi hili hili la polisi tulilonalo,” alisema Masauni.

 

19 WAACHIWA

Watu 19 kati ya 26 waliokuwa wakishikiliwa na polisi kufuatia tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara huyo waliachiwa kwa dhamana juzi usiku akiwemo Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema wanaendelea kuwashikilia wengine saba ili kuendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

Manara alishikiliwa na Jeshi la Polisi tangu Oktoba 12 kwa kosa la kusambaza taarifa za kutekwa kwa Mo kwenye mitandao ya kijamii kwa madai ya kutumwa na familia jambo ambalo polisi ilisema si za kweli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles