27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Kutana na vijana walioamua kufukia elimu yao ardhini

Untitled-1NA RAYMOND MINJA, DODOMA
VIJANA wengi wanaohitimu vyuo hawapati kazi mara tu ya kuhitimu masomo yao na hii ni kutokana na kutokuwapo kwa vyanzo vya ajira vinavyokwenda sambamba na ongezeko la wahitimu.

Hali hiyo inachangia kuwapo kwa wimbi la wahitimu wasiokuwa na ajira hapa nchini.

Tatizo hili la ajira limekuwa ni mwiba kwa serikali kwani kiwango cha uzalishaji wa wataalamu hakilingani na ajira zilizopo;   si jambo la kushangaza kutangazwa ajira za watu 300 lakini katika usaili wakatokea waombaji 13,000.

Na mara nyingi vyuo vingine vimekuwa vikichangia kwa kiasi kikubwa kwani vimekuwa vikizalisha vijana ambao hawaendani na soko la ajira lililopo na hii ni kutokana na wengi wa wamiliki kuangalia fedha zaidi kuliko
bidhaa anayoizalisha.

Wasomi wengi hapa nchini wamekuwa na dhana potofu kuwa wanapomaliza elimu zao za juu ni lazima waajiriwe na Serikali ama mashirika makubwa huku wakisahau kuwa wanaweza kutumia elimu na maarifa waliyoyapata vyuoni kujiajiri na hata kutoa ajira kwa watu wengine.

Kilimo ni sekta muhimu inayogusa maisha ya watu wengi nchini kwani asilimia 75 ya watu waishio vijijini wanategemea kilimo kama ajira na njia pekee ya kuendeshea maisha yao ya kila siku.

Kwa kutambua fursa ya ajira iliyoko katika kilimo vijana wasomi wanaounda Taasisi ya Maendeleo ya Vijana Tanzania (TAYODA), wanaamua kufukia elimu yao ardhini ili iweze kumea na kuzaa matunda.

Hiyo ni baada ya kuamua kujikita katika kilimo cha vitunguu tangu mwaka 2013, muda mfupi baada ya kumaliza elimu yao ya juu.

Vijana hao wanaomiliki shamba lenye ukubwa wa heka 300 katika Kijiji cha Idodoma wilayani Mpwapwa, Dodoma, wanawataka vijana wanaolalamika kukosa ajira, kuunga mkono kauli ya hivi karibuni ya Rais Dk. John Magufuli inayowataka wafanye kazi badala ya kucheza pool toka asubuhi.

Akizungumza na mwandishi wa makala hii aliyetembelea shamba lao hilo hivi karibuni, Mkurugenzi wa TAYODA, Jackson Kangoye, anasema taasisi yao imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kukuza mitaji ya vijana walioko mitaani kwa kupitia sekta  ya kilimo.

Kanyonge anasema baada ya kuona ugumu wa upatikanaji wa ajira waliamua kujiunga pamoja na kuunda taasisi hiyo yenye lengo la kuwakwamua vijana katika wimbi la umaskini na kuwafanya vijana kujishughulisha katika kazi mbalimbali ikiwemo kilimo.

Anasema mwaka 2013 walianza na vijana 25 na walifanikiwa kulima zao la vitunguu  katika shamba lenye ukubwa wa ekari 30,  wakaendelea kupata mafanikio yaliyowazesha kupata shamba lenye ukubwa wa ekari 300 huku idadi ya vijana wanaojishughulisha na kilimo hicho ikiongezeka hadi kufikia 230 mwaka huu.
“Lengo letu katika kipindi cha miaka mitatu ijayo ni kuwaingiza katika shughuli hii vijana 2,500 walioko mitaani bila kujali viwango vyao vya elimu,” anasema Kangoye.

Kangoye anasema wakiwa shambani vijana hao hugawanywa katika makundi ya watu watano ambapo kila kundi hupewa ekari tano kwa msimu mmoja na kuzitumia kupata mitaji.

“Tangu tuanze kilimo hiki uzoefu wetu unaonesha kwa kila ekari moja, tunazalisha kati ya gunia 80 na 120 za vitunguu ambalo huuzwa kwa kati ya Sh 120,000 na Sh 170,000. Fedha hizi ni sawa na wastani wa Sh milioni 10 hadi 20 kwa ekari,” anasema.

Anasema kiasi kinachobaki baada ya kutoa asilimia 25 ya pato lote linalokwenda katika taasisi hiyo kwa ajili ya kusaidia vijana wengine na gharama za matumizi, hutolewa kwa vijana hao kama mtaji wanaoweza kuutumia kujiendeleza katika kilimo hicho katika mashamba yao wenyewe.

Kangoye anasema zaidi ya vijana 120 wamekwishanufaika kiuchumi kupitia mpango huo kwa kuanzisha miradi yao ya kilimo cha vitunguu, pilipili, tikiti na nyanya.

Mmoja wa vijana aliyenufaika na mpango huo, Kassara Mageni, anasema; “Baada ya kumaliza Chuo Kikuu cha Dodoma mwaka 2012, sikutaka kubweteka kusubiri kuajiriwa. Nimehamia shamba, nalima na ninawasimamia vijana wenzangu kupitia taasisi hii ya TAYODA.

Anasema mbali na kujipatia mapato makubwa kutoka katika mashamba anayolima, mpango wake ni kuhamishia maisha yake moja kwa moja katika kijiji hicho.

“Wasomi wengi tuna ndoto ya kupata mafanikio ya haraka tena kupitia kazi za kuajiriwa, bahati mbaya wengi wetu tunachelewa kufikia ndoto hiyo, niwajulishe wasomi wenzangu maisha yako huku, sekta ya kilimo ina fursa kubwa inayoweza kubadili maisha yetu vijijini na mijini,” anasema.

Kijana mwingine, Gapi Yohana, anasema kwa miaka miwili ambayo amefanya kazi na taasisi hiyo ameweza kuongeza ukubwa wa shamba lake kutoka ekari moja hadi tano pamoja na kujiimarisha kiuchumi.

Anasema amenunua pikipiki pamoja na kiwanja anachotarajia kukitumia kujenga nyumba yake ya kisasa.

“Nawashauri vijana wenzangu wasisubiri kazi za kuajiriwa, wawe jasiri na kuthubutu kama sisi tulivyothubutu,” anasema Yohana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles