27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Kumbukizi ya Sokoine: Tunahitaji ujasiri wake kupambana na dhuluma na uonevu

“EDWARD Moringe Sokoine alikuwa Mzalendo. Kila mara aliweka utumishi kwa umma mbele. Alifanya kazi kwa bidii hata alipokuwa mgonjwa. Siku zote alikuwa mstari wa mbele katika kubuni mbinu za kujenga uchumi imara na kujikwamua kutokana na hali ngumu ya uchumi.


“Uzalendo wake ndio uliomfanya awe na nidhamu ya kujituma, ufanisi katika kazi na mtekelezaji wa dhati wa Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea… wakati wa uvamizi wa nduli Idd Amin Ndugu Sokoine alifanya kazi kwa saa nyingi kusukuma upatikanaji wa mahitaji ya jeshi letu na mara nyingi alitembelea majeshi kwenye uwanja wa mapambano.


“Wakati wa kipindi cha vita, alitumia saa chache sana kupumzika na siku nyingine hakupumzika kabisa kwa saa 24. Ndugu Sokoine ni mzalendo aliyeipenda Tanzania kwa moyo wake wote.”

Hiyo ni nukuu kutoka tamko la Waziri Mkuu Salim Ahmed Salim bungeni kuhusu maombolezo ya kifo cha Marehemu Edward Moringe Sokoine Juni 20, 1984, ambaye kesho inatimia miaka 29 tangu alipofariki kutokana na ajali ya gari Aprili 12, 1984 na kesho kutwa Ijumaa inatimia miaka 35 tangu alipoaga dunia.


Habari za kifo cha Hayati Sokoine zilikuwa ni mwiba mchungu kwa jamii na watu wenye mapenzi mema na miongoni mwa watu walioguswa na kifo hicho ni Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere ambaye kwa vyovyote vile alikuwa amemwandaa kuchukua madaraka ya uongozi wa nchi pindi aking’atuka na kweli alikuwa ni chaguo mwafaka kwake.


Sokoine na mapambano ya kiuchumi
Sokoine alisikitishwa na ulanguzi, Machi 7, 1983 alisema; “Tumeruhusu walanguzi na wahujumu uchumi kuongoza nchi, wananchi wamefikia mahali ambapo wanashindwa kutofautisha kati ya viongozi wa chama na serikali na walanguzi na wahujumu uchumi wa nchi,”


Hali hiyo aliyoiona kuwa inadhalilisha wanajamii Machi 19, 1983 alitoa Waraka wa Serikali akisema; “Walanguzi na wahujumu uchumi wote ni maadui wa taifa ni lazima kuwapiga vita na kuwatokomeza waelekezwe katika shughuli za kilimo ili waweze kuishi kwa jasho lao,”
Hali kadhalika alisema; “Tabia ya rushwa na magendo inavuruga haki za wananchi na kupunguza imani ya wananchi kwa serikali, vyombo vyake na hata chama kinachotawala.”


Alisema, “Serikali ilikuwa imeenda likizo” na akatangaza operesheni dhidi ya wahujumu uchumi kuonesha imerudi kutoka likizo na iko tayari kwa mapambano ya kuuokoa uchumi.
Hayati Sokoine kutokana na kuelekeza nguvu zake dhidi ya rushwa, aliona mazingira ambayo uadilifu wa uongozi na uwajibikaji umeporomoka.


Machi 26, 1983 alinukuliwa, “Ole wake kiongozi mzembe na asiye na nidhamu nitakayemkuta: Kiongozi wa siasa hana usalama wa aina yoyote. Usalama wake ni kudra ya Mungu na Wananchi peke yake. Viongozi wazembe na wabadhirifu wahesabu siku zao. Labda tusiwajue. Hawa hatuna sababu ya kuwapa imani, kuwa tutawalinda kama vitendo vyao viovu,”


Alitupia macho nguzo ya uchumi wa nchi, kilimo ambacho kinatumiwa na asilimia 80 kama nyenzo kuu ya uchumi.
Katika kukazia kujitosheleza kwa chakula Oktoba 4, 1983 alisema “Wajibu wa kila Mtanzania, kila familia na kila anayekula ni kujilisha mwenyewe. Si wajibu wa taifa kumlisha mtu. Unaweza ukasaidiwa unapopatikana na janga. Lakini kama hakuna janga ni wajibu wa kila mtu aweze kujitosheleza kwa chakula na atoe ziada kwa taifa,”


Kutokana na jinsi alivyotoa kipaumbele kwenye kilimo pia alikuwa anapinga kuondolewa kwa ruzuku ya kilimo ambayo ilikuwa inatolewa kwa wakulima na katika kuthamini kwake huko kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) ilikuwa ni njia mwafaka na endelevu ya kumuenzi.


Sokoine hakumbukwi kwa majigambo ndani ya Bunge au kwa kujipatia utajiri wa haraka kwa kutumia nafasi yake bali anakumbukwa kwa uadilifu wake, mapenzi kwa nchi yake na kwa familia ya Watanzania.
Watanzania walimpoteza kiongozi rafiki, mzalendo, aliyeongozwa na dhana ya kuwa kila Mtanzania anastahili, aliyepinga kabisa tabia ya watu wachache kutumia vibaya nafasi zao.


Katika kutimiza wajibu wake alijijengea maadui ambao hawakupendezwa na utendaji kazi wake na kutovumilia uzembe na uvivu.
Kama binadamu wengine alikuwa na kasoro zake, lakini kwa kuwajali wanyonge, hatuna budi kufumba macho na kumuona Sokoine alikuwa ni taa ing’aayo juu ya mlima!

Alikuwa mfano wa kuigwa katika uongozi na hatuna budi kukumbushana kuwa Tanzania bado inahitaji viongozi walio mahiri, wanaoweka maslahi ya taifa mbele, wanaojali utu bila kuogopa vyeo vyao, sifa zao, au hali zao za maisha!


Akisi ya mwangwi wa utendaji wa Sokoine inaonekana hivi sasa kwa utendaji wa serikali na hiyo ni njia endelevu ya kumuenzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles