23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

KULALA CHALI HUONGEZA HATARI KWA WAJAWAZITO KUZAA WATOTO NJITI

sleeping-during-pregnancyWANAWAKE walioko katika miezi ya mwisho kabla hawajajifungua, ambao wanalala chali au kwa maneno mengine kulalia mgongo wanakaribisha hatari ya kuzaa watoto njiti, kwa mujibu wa utafiti mpya.

Watafiti wamebaini kuwa aina hii ya mlalo inawaweka zaidi watoto walio tumboni katika shinikizo, ikisababisha kupungua kwa mtiririko na hivyo matumizi ya hewa ya oxygen.

Ugunduzi huo unaweza kutoa mwanga zaidi juu ya kwanini baadhi ya watoto hutoka kabla ya wakati.

Takwimu nchini Uingereza huonesha kwamba kwa kila vizazi 227, mwanamke mmoja huishia kuzaa mtoto njiti.

Tafiti za awali zimeonesha kuwa aina za milalo wanazotumia akina mama huathiri afya ya watoto wao lakini haikufichua kwa namna gani na kwa nini.

Mtafiti kiongozi Profesa Peter Stone wa Chuo Kikuu cha Auckland nchini New Zealand, alisema: ‘utafiti wetu ulibaini kuwa kulalia mgongo kunaweza ongeza hatari ya kuzaa mtoto njiti.

Hatari inaweza kuongezeka zaidi kwa wanawake wenye wenye matatizo ya kiafya, alisema.

Katika utafiti huo mpya, wanasayansi waliwachunguza wanawake 29 wenye mimba na afya njema katika miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito wao (third trimester) na watoto wao walio tumboni.

Wanawake wote walikuwa na mimba zenye umri kati ya wiki 35 na 38 na hawakuwa katika hatari ya kukumbana na matatizo yoyote ya kiafya.

Kila mwanamke alitakiwa alale katika moja ya aina ya milalo minne; kulalia tumbo, chali lakini kwa mwinuko wa nyuzi 30 na kulalia upande wa kushoto na kulia.

Walitakiwa kubakia kwa kila mlalo wakiwa na mto mmoja kichwani kwa dakika 30 wakati watafiti wakifuatilia mapigo ya moyo na kiwango cha kujishughulisha cha watoto wao tumboni.

Watafiti walibaini kuwa wakati wanawake wanapolala chali, husababisha shinikizo la kisaikolojia kwa mtoto.

Kwamba walikuwa katika hali ya kulala ambapo walijishughulisha kwa kiwango cha chini, kitu kilichomaanisha walipata kiwango kidogo cha oxygen. Na mapigo ya moyo pia yaliathirika.

Watoto walio tumboni walikuwa mara tano na uwezekano wa kuwa katika hali hii iwapo mama zao walilalia tumbo kuliko pale walipolalia upande wa kushoto.

Kwa kadiri walivyokosa hewa ya oxygen ndivyo walivyoelekea kupata matatizo ya kiafya, mimba ya mapema au hata hatari ya kifo kwa watoto, hasa wale wenye matatizo ya kiafya.

Mwandishi wa utafiti huo alisema; “Milalo ya uzazi ina uhusiano mkubwa na hali ya kitabia ya mtoto aliye tumboni kwa kuzingatia mapigo ya moyo ya kijusi na tofauti zao.

Kulala chali kunaweza kuwa na athari mbaya sana kwa kijusi na kusababisha shinikizo kwa mimba na hata uwezekano wa kutoka kwa kijusi au kifo.

Hata hivyo, wanawake wote waliohusika katika utafiti huo walienda kuzaa watoto wenye afya kwa vile majaribio waliyofanya ikiwamo kulala katika mlalo mbaya yalikuwa ya muda mfupi.

Profesa Stone alisema; “Tuliangalia tu athari za milalo ya uzazi kwa kipindi kifupi wakati mama akiwa macho. Tafiti zaidi zinahitajika kuangalia athari za kukaa katika milalo fulani ya uzazi wakati wa usiku.

Chuo cha Wakunga cha Royal nchini Uingereza (RCM) kimesemna utafiti huo umeonesha kuwa aina za mlalo ni muhimu kwa wanawake walio katika miezi ya mwisho ya uzazi wao.

Louise Silverton, Mkurugenzi wa RCM kwa wakunga alisema; “Tumekuwa tukifahamu kwa muda mrefu kwamba shinikizo la damu hupunguzwa wakati mwanamke anapolala chali. Wanawake wengi husema kuwa hawalali chali kwa vile wanajisikia hali isiyo ya kawaida wakilala hivyo.

Utafiti umeonesha kwamba hata kwa wanawake wenye afya na kijusi kisicho na matatizo wako hatarini, ikionesha kwamba kuzingatia aina za mlalo kwa wajawazito ni muhimu sana.

Kuna somo kwa wakunga kuhakikisha wanawashauri wanawake kuhusu nafasi nzuri za kulala katika sofa.

Matokao ya utafiti huo yanaonekana kuendana na ile nyingine za siku nyingi ambazo tayari wanawake wanashauriwa juu ya aina za kulala.

Tafiti hizo za zamani hushauri wanawake wanaomaliza miezi mitatu ya kwanza, ambapo tumbo linakuwa limeongezeka ukubwa kutokana na ukuaji wa mtoto namna ya kulala.

Ukuaji wa mtoto unaendana na aina ya ulalaji wa mama,hivyo mama anashauriwa mimba ikifika miezi minne, yaani wiki 16 asilalie tumbo au mgongo.

Wanaelezwa kwamba kulalia mgongo si kuzuri kwa sababu uzito wa mtoto huzuia baadhi ya mishipa ya mgongoni  inayosafirisha damu toka kwenye uti wa mgongo kwenda kichwani, na kutoka miguuni kuja kichwani kusafirisha damu ipasavyo. Aidha hubadili mfumo wa mzunguko wa damu  unaoweza kumuathiri mama au mtoto.

Tafiti nyingi zinamshauri mama mjamzito alalie upande wa kushoto.

Ni kwa sababu damu husafirishwa kwa urahisi zaidi kutoka kwenye moyo wa mama na kwenda kwenye kondo la mtoto na kumpa virutubisho vingi zaidi.

Iwapo mama atalalia tumbo au mgongo itamfanya mtoto asijisikie vizuri na hivyo kuhangaika na kumpiga piga mama ili abadili aina ya mlalo.

Mama anapolala ni vizuri akaweka mto katikati ya miguu hatakiwi kubana miguu, humsaidia kulala vyema na damu kusafirishwa vizuri na kutopata maumivu ya mgongo.

Nyakati za usiku ni kawaida kwa watoto kupiga piga tumboni na iwapo inatokea anapiga piga sana tumboni basi mama atakuwa amelala vibaya na hivyo kutakiwa kubadili aina ya mlalo.

Mwisho

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles