25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

KUKAMATWA KWA WABUNGE KWACHAFUA HALI YA HEWA

Na MAREGESI PAUL- DODOMA

MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), amechafua hali ya hewa bungeni, baada ya kuwasilisha taarifa akihoji sababu za Jeshi la Polisi kuwakamata wabunge wa upinzani bila sababu za msingi.

Katika tukio hilo lililotokea jana jioni, wabunge wote wa upinzani walilazimika kutoka nje, baada ya kutoridhishwa na majibu ya Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, aliyoyatoa wakati akijibu taarifa hiyo ya Zitto.

Awali, Dk. Tulia alilieleza Bunge jinsi alivyopata ujumbe wa maandishi kutoka kwa Zitto, ukimwomba ampe nafasi ya kutoa taarifa katika suala alilokuwa nalo.

Baada ya kukamilisha kauli hiyo, Zitto alisimama na kulieleza Bunge kwamba utaratibu wa Jeshi la Polisi wa kuwakamata wabunge wa upinzani unakiuka taratibu na kanuni za Bunge.

“Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge letu liko katika nchi za Jumuiya ya Madola na linaongozwa na katiba, kanuni, sheria za mabunge mengine, maamuzi ya maspika wengine na sheria zingine.

“Hivi karibuni, Mbunge wa Arusha, Godbless Lema (Chadema), alikamatwa nje ya Bunge baada ya kuhudhuria vikao vya Bunge na hadi sasa Bunge halina taarifa.

“Kwa mujibu wa kanuni zetu na nchi za Jumuiya ya Madola, polisi wanapotaka kumkamata mbunge, lazima kwanza wampe taarifa Spika wa Bunge na baadaye Spika aliambie Bunge juu ya taarifa hiyo na kueleza ni kwanini mbunge amekamatwa.

“Pamoja na Lema kuwekwa ndani, Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali amefungwa jela miezi sita na hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kwa Spika wa Bunge na hata Bunge halijaelezwa juu ya tukio hilo.

“Katika hayo, Sheria ya Bunge ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge inakiukwa kwa sababu hata jana (juzi), Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), alikamatwa bila Spika kuwa na taarifa.

“Mimi binafsi nilimpigia simu Spika kumuuliza juu ya tukio hilo, Spika akasema hakuwa na taarifa, hii ni dharau kubwa sana kwa Bunge.

“Mheshimiwa Naibu Spika, mhimili wa Bunge umedharauliwa mno kwani hata mimi nimepata taarifa, kwamba polisi wananisubiri ili nikitoka nje wanikamate na siogopi kukamatwa.

“Kwa hiyo, naomba jambo hili lijadiliwe na litolewe uamuzi kwa sababu mwaka 2011, Bunge la Uingereza ililetwa hoja kama hii na Bunge likaijadili na kuitolea uamuzi,” alisema Zitto huku akitoa mfano wa wabunge waliowahi kukamatwa na polisi akiwamo Mbunge wa Nzega Vijijini, Dk. Hamisi Kigwangala (CCM).

Akitoa ufafanuzi wa taarifa hiyo, Naibu Spika alivitaja vifungu vya 6, 7, 8, 12 na 13 vya Kanuni ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge, vinavyoeleza juu ya mbunge kukamatwa.

“Kwa hiyo, kifungu cha 12 kinasema Spika atapewa taarifa pale tu mbunge atakapokuwa akitakiwa kukamatwa kwa makosa ya madai na si kwa makosa yasiyokuwa ya madai.

“Hivyo basi, taarifa ya mheshimiwa Zitto siwezi kuruhusu ijadiliwe kwa sababu makosa hayo si ya madai,” alisema Naibu Spika.

Baada ya majibu hayo, wabunge wa upinzani walianza kulalamika akiwamo Mbunge wa Serengeti, Marwa Chacha (Chadema), aliyesimama akitaka apewe ruhusa ya kuzungumza.

Hata hivyo, Naibu Spika hakumruhusu na alipomtaka akae ili Bunge liendelee, alikataa na hivyo kuagiza askari wa Bunge wamtoe nje kwa nguvu, jambo ambalo lilipingwa na wabunge wa upinzani na kuamua kutoka nje ya Bunge.

ZITTO NA WAANDISHI

Baada ya wabunge hao kutoka nje, Zitto aliwaambia waandishi wa habari kwamba wataendelea kusimamia Kanuni za Bunge ili zisivunjwe kama anavyofanya Naibu Spika.

“Lissu amekamatwa bila kujua sababu za kukamatwa kwake na inawezekana mpaka sasa hajajua. Sasa Naibu Spika atwambie ni wakati gani Spika anajua mbunge anapokamatwa, anakamatwa kwa makosa ya madai au ya jinai.

“Mabunge yote duniani utaratibu ni kwamba unapotaka kumkamata mbunge, lazima utoe notisi kwa Spika, lakini hapa kwetu huo utaratibu haufanyiki. Katika hili, Naibu Spika amekwenda kinyume na ulinzi wa hadhi ya Bunge,” alisema Zitto.

MDEE

Katika mazungumzo yake kwa waandishi wa habari, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, alisema tabia ya Dk. Tulia itawatisha wabunge kwa sababu mara zote amekuwa akiwakandamiza wabunge wa upinzani.

“Hatukubaliani na kilichofanywa na Naibu Spika pamoja na kutoka bungeni leo, kesho tutaingia na kuendelea kudai haki zetu maana hatukubali kuwa tunakamatwa kila wakati,” alisema Mdee.

KHATIBU

Naye Mbunge wa Konde kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Khatibu Said Haji, alishangaa wabunge wa upinzani kukamatwa bila taarifa wakati watuhumiwa wa dawa za kulevya wanaitwa kwa utaratibu unaojali haki za binadamu.

Kutokana na hali hiyo, alisema hawatakata tamaa katika suala la kupinga uonevu wowote unaofanywa na Dk. Tulia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles