23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Kukaa muda mrefu husababisha saratani

bigstock-young-man-in-office-with-compu-29935619

VERONICA ROMWALD NA ESTHER MNYIKA – DAR ES SALAAM

WATU wanaokaa kitako zaidi ya saa nne wamo katika hatari kubwa ya kupata magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza.

Utafiti unaonyesha watu wanaokaa sehemu moja kwa zaidi ya saa nne wanakabiliwa na magonjwa ya kisukari, moyo, shinikizo la damu na saratani.

Dk. Fredirick Mashili wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS) alisema hayo  Dar es Salaam jana alipozungumzia  kampeni ya mazoezi na afya bora itakayofanyika Oktoba 8, mwaka huu.

“Ingawa teknolojia ya kisasa imerahisisha maisha lakini kadri muda unavyokwenda imefanya watu wengi kuishi maisha ya kukaa tu bila kufanya mazoezi ya kutosha na hivyo kujiweka kwenye hatari ya kupata magonjwa hayo,” alisema.

Akitoa mfano, alisema katika ripoti iliyochapishwa hivi karibuni yenye kichwa cha habari ‘International Cardiovascular Desease Statistics’ Shirika la Moyo la Marekani limeeleza kuwa kutokufanya mazoezi na kula vyakula visivyofaa ni mambo yanayochangia magonjwa ya moyo.

Alisema mabadiliko ya uchumi, watu kuhamia mijini, ustawi wa viwanda na kuenea kwa biashara za kimataifa huleta mabadiliko katika mtindo wa maisha hasa mijini  kwa kusababisha kuongezeka magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

“Watu wanakaa ofisini muda mrefu mbele ya kompyuta zao, wakitoka wanaingia kwenye gari kwenda nyumbani, wakifika wanakaa kutazama luninga, matokeo yake wanajikuta wamepata maumivu ya mgongo… hali ni mbaya,” alisema.

Alisema kukua kwa teknolojia kumechangia pia watoto kukosa muda wa kucheza badala yake hupendelea kukaa na kucheza michezo ya kwenye kompyuta na video (luninga).

Alisema watoto wasiofanya mazoezi wanaweza kukabiliwa na hatari ya kutojiheshimu, kuwa na wasiwasi mwingi na mfadhaiko mkubwa.

“Upo uwezekano mkubwa wa watoto hawa kuwa wavutaji wa sigara na kutumia dawa za kulevya wanapokuwa wakubwa kuliko watoto wanaofanya mazoezi.

“Na watu wazima wasiofanya mazoezi wanapofikia umri wa uzee hupoteza nguvu na uwezo wa kufanya shughuli za kila siku na akili zao huzorota,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles