33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

KUJIUZULU KWA HAILEMARIAM KWAHITIMISHA KIVULI CHA ZENAWI

JOSEPH HIZA NA MASHIRIKA


WAZIRI Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn Boshe (HDB) alijiuzulu bila kutarajiwa Alhamisi ya wiki iliyopita, akiwa kiongozi wa kwanza kufanya hivyo katika historia ya Taifa hilo.

Minong’ono kuwa HDB angeondoka kutoka kiti hicho moto kwa sasa ilianza kusambaa katika mji mkuu wa Addis Ababa kwa miezi kadhaa, lakini tangazo lake likaja kwa mshangao wa wengi.

Wengi wanajiuliza kilichomfanya ajiuzulu, moja ya maamuzi ya nadra kufanywa na wakuu wa nchi za Afrika.

Naam, ni nadra katika bara, ambalo viongozi kung’ang’ania madaraka licha ya madudu ya wazi wafanyayo na nachelea kulinganisha uamuzi wake huo na kilichotokea nchini Zimbabwe Novemba mwaka jana na Afrika Kusini pia Alhamisi ya wiki iliyopita.

Nchini Zimbabwe, Robert Mugabe na Afrika Kusini, Jacob Zuma wote walilazimishwa na vyama vyao achilia mbali upinzani kujiuzulu kwa sababu za msingi na zinazofahamika wazi.

Lakini HDB alijiuzulu baada ya kupata joto la kichini chini ndani ya Chama chake, muungano wa vyama vinne, Ethiopian People’s Revolutionary Democratic Front (EPRDF), ambao umegawanyika kutokana na machafuko yanayoendelea humo yakihusisha maeneo yenye uwakilishi ndani ya mwavuli huo.

Vyama vinavyounda EPRDF ni cha watu wa Oromo, Oromo Peoples’ Democratic Organization (OPDO), cha watu wa Amhara, Amhara National Democratic Movement (ANDM), cha watu wa makabila madogo madogo ya kusini mwa nchi, Southern Ethiopian People’s Democratic Movement (SEPDM) na cha watu wa jamii ndogo ya Tigray, Tigrayan People’s Liberation Front (TPLF).

Ndiyo maana licha ya HDB aliyemo humo akitokea SEPDM kama kiongozi wake, kutoa sababu za kujiuzulu, wengi hawakuonekana kuridhika nazo kutokana na historia ya taifa hilo.

Akitangaza uamuzi wake huo, ambao unasubiri baraka za Bunge, Desalegn alisema: “Kujiuzulu kwangu kuna maana sana kwa wakati huu ili tuunde mazingara mwafaka ya kuendeleza mabadiliko yatakayotufaa katika kupanua amani na demokrasia.

Uamuzi wake ulikuja kutokana na maandamano katika majimbo ya Oromia na  Amhara, ambayo yana makabila makubwa zaidi nchini humo. Maandamano hayo mizizi yake ni hali ya kiuchumi, siasa, ukiukaji wa haki za binadamu na udhibiti wa EPRDF na hasa unaofanywa na jamii ya Tigray, yaani TPLF katika siasa za Taifa hilo.

TPLF ni vuguvugu la kabila na eneo dogo la Tigray, analotoka mtangulizi wa Desalegn, marehemu Meles Zenawi aliyeongoza vita ya msituni, ambaye kwalo liliangusha utawala wa kijeshi na kidikteta wa Kanali Mengistu Hailemariam Mei 1991, ambaye anaishi uhamishoni Zimbabwe hadi sasa.

Katika hilo utawala wake unahusishwa na madai tele ya ufisadi, ubaguzi, upendeleo na udhaifu wa kijumla katika kutoa nafasi sawa za huduma kwa wote kwa taifa hilo bila kujali ukubwa au udogo wa kabila.

Kwa sababu hiyo, katika kipindi cha utawala wake baadhi walimuona kama dikteta fulani na mkandamizaji kama mtangulizi wake, lakini ukweli ni kuwa HDB hakuwa mtoa maamuzi halisi.

Bali alifanya kazi kwa kivuli chenye nguvu cha mtangulizi wake Zenawi.

Kujiuzulu kwa Hailemariam kulifuatia wiki kadhaa, ambazo zilianza kwa mgomo wa siku mbili na kufungwa kwa barabara kule Oromia na kuachililiwa kwa wapinzani maarufu zaidi kutoka jela.

Hailemariam alitangaza kuachiwa kwa wafungwa mwezi uliopita huku upinzani dhidi ya serikali ukizidi kukua kwa namna ambayo haijawahi kuonekana tangu aingie madarakani Agosti 2012 kuchukua nafasi ya Zenawi.

Hasira dhidi ya EPRDF zililipuka Desemba 2015 wakati kabila hilo kubwa kabisa nchini humo yaani Oromo, lilipoanza mandamano makubwa kisha kufuatiwa na kabila la pili kwa ukubwa la Amhara.

Hali ya tahadhari ya miezi 10 iliyotangazwa Oktoba 2016 ilisaidia kupunguza machafuko makubwa, kabla ya kuibuka vifo vya mamia ya watu na makumi elfu kukamatwa huku makundi ya haki za binadamu yakilaani.

Lakini upinzani dhidi ya Serikali ukaendelea na mapigano mengine baina ya Oromo na watu wa asili ya Somalia yakisababisha watu milioni mwishoni mwa mwaka jana kukimbia nchi.

Akiwa katikati ya shinikizo baina ya pande mbili zenye nguvu; Oromi na Amhara kwa upande mmoja na wafadhili wake Watigray kwa upande mwingine, HDB hakuwa na sauti, kazi ikamshinda na kuamua kujiuzulu si tu uwaziri mkuu bali pia uenyekiti wa EPRDF.

Ni uamuzi ambao usingeshuhudiwa iwapo Meles anayejulikana kwa udikteta, msimamo mkali na asiyefikiria mara mbili mbili kupukutisha wapinzani wake angekuwa madarakani.

Sasa je, ni kweli amejiuzulu kwa moyo mkunjufu? Licha ya namna alivyoongea mwenyewe kuonesha hilo, halioneshi kuwa karibu na ukweli.

Tuangalie namna alivyochukuliwa na Meles kuwa naibu wake, yaani kuandaliwa kuwa waziri mkuu wa baadaye wa Ethiopia.

Wakati kifo kilipomjongea Meles, vigogo wa TPLF, walianza kutafuta mtu wa kuziba pengo lake. Walifahamu fika baada ya Meles hawawezi kwa mara ya pili mfululizo kumweka m- Tigray mwenzao mwingine kuwa waziri mkuu ajaye.

Kwamba itakuwa vigumu kutetea kitendo hicho ndani ya EPRDF yenye mseto wa makabila kutoka pande nne nne za nchi.

Hata hivyo, Watigray pia hawakuwa tayari kuona wadhifa huo wenye nguvu ukienda kwa mtu kutoka jamii zenye nguvu za Oromo na Amahra.

Ili kuepukana na Tigrayan, Oromo, na Amhara wakamuona HMD kutoka jamii ndogo ya Wolaita kama chaguo lao sahihi.

Kigezo kingine muhimu kwa TPLF ni kuwa na haiba ya utiifu na kujikomba, mtu atakayetekeleza matakwa yao bila kusita. HMD alionekana kuwa na sifa hiyo.

Kwa ufupi kile walichotaka TPLF kilikuwa kibaraka, ambaye wataweza kumtawala na hivyo kuendelea udhibiti wao wa nchi.

Hivyo, waziri wa mambo ya nje huyo wa zamani alichaguliwa kuwa waziri mkuu kuendeleza utawala wa mkono wa chuma wa Meles, kweli hakuwaangusha wafadhili wake!. Katika maamuzi na matendo yake yote alionesha shukrani kwa ‘watengeneza wafalme’ wake hao.

Hata hivyo, ili kuwafurahisha kwa kumuiga Meles matendo yake, namna ya kuzungumza, na kadhalika, kukamfanya awe kichekesho, kwani haikuwa haiba yake halisi!

Baba huyo wa watoto watatu wote mabinti, akawa kikatuni cha Meles, ‘kopi’ dhaifu ya Meles au maiti ya Meles inayotembea.  Kwa kufanya hivyo, akapoteza sauti yake halisi, haiba yake na kukosa fursa ya kuacha nyuma alama.

Itakuwa ngumu kwa utawala wake wa miaka mitano na nusu kukumbukwa kama utawala wa HMD, bali wa Meles, aliyetawala kutokea kaburini!.

Iwapo atakumbukwa, historia itamkumbuka HMD kama mtawala wa kipindi ambacho mtawala halisi hajachaguliwa, kipindi cha baina ya Meles na yule atakayekuja baada ya HMD.

Kipindi cha miaka mitano ya utawala wake, HMD, ambaye mkewe ni mwajiriwa wa Umoja wa Afrika (AU) nchini humo, anahesabiwa hakubuni mpango wowote mpya, sera au mradi mpya mkubwa. Yote ameikuta, ni kama meli inayoelea bila nahodha.

Kujiuzulu kwake kunaonesha ukubwa wa mgogoro uliopo nchini humo na namna vuguvugu la Qeerron (Oromo) lilivyoilazimisha TPLF kubadili dereva. Pia linaashiria mwishowe Meles amezikwa rasmi na kuanzia kwa enzi mpya za baada ya Meles.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles