24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

KUJITOSHELEZA SUKARI,BAGAMOYO SUGAR KUFANYA UZALISHAJI  

Na Shermarx Ngahemera


KAMPUNI  ya Said Salim Bakhresa (SSB Group) imeitikia mwito wa Serikali wa kuongeza uzalishaji  wa sukari ili nchi iweze kujitegemea kwa bidhaa hiyo pendwa kwa matumizi ya nyumbani na viwandani na ziada kuuza nje.

Kampuni hiyo  imejiweka imara kuanza uzalishaji wa sukari  kwa kuanza kutengeneza vitalu vya miwa huko  wilayani Bagamoyo katika kijiji cha Makurunge   ikiashiria  kuanza  uzalishaji  wa sukari ndani ya miaka miwili.

Taarifa kutoka SSB inasema itaanza rasmi kuzalisha sukari mwezi Julai 2020 kutoka Bagamoyo baada ya kumalizika kwa kubuni, kusanifu na ujenzi wa  kiwanda  cha kutengeneza sukari  zoezi ambalo  litachukua miaka miwili  kukamilisha.

Hatua hiyo inaendana na mahitaji  ya Rais John Magufuli ambaye alitoa hekta 10,000  (ekari 25,000) za ardhi kwa  mfanya biashara huyo mashuhuri  nchini  mwenye  biashara kubwa za usafiri, ukulima, biashara na viwanda Tanzania, Said Salim Bakhresa, ili kuanzisha  kilimo cha miwa  kwa kuwa na kiwanda cha  sukari na kuimarisha uzalishaji wake.

Mwezi huu SSB ilianzisha rasmi mashamba ya miwa  ya sukari kwa kuweka vitalu  na kupanda vitalu vya miwa katika shamba la Makurunge.

“Mwanzo wa mchakato wa kupanda miwa ya kitalu ni ishara kwamba tatizo la sukari litakuja  kwisha hivi karibuni hapa nchini,” alisema msemaji wa SSB Group,  Hussein Sufian kama alivyonukuliwa na vyombo vya habari nchini.

Alisema mchakato wa upandaji wa kitalu utafikia mwisho wake ndani ya  miezi sita wakati uwekaji mitambo ya kiwanda cha usindikaji wa sukari utakwisha katika miaka miwili tangu sasa.

Mahitaji ni makubwa kuliko uzalishaji

Kutokana na uzalishaji mdogo bidhaa ya sukari huuzwa kwa bei ya juu na juhudi zote za serikali kupunguza bei zimefikwa na uchu na choyo ya wafanyabiashara ambao hawataki kuona bei inashuka na hivyo kufanya biashara ya sukari kugubikwa na mikingamo ya kila namna.

Kilimo cha miwa kama ilivyo kwa mazao mengine kinategemea zaidi hali ya hewa ya eneo husika kama vile joto, unyevu, mvua, uwepo wa vyanzo vya maji vya kudumu kwa ajili ya umwagiliaji. Kwa upande wa udongo hutegemea sanaudongo wenye uwezo mkubwa  wa  kuhifadhi maji (loamy soil).

“Muda wa ukomavu wa miwa hulingana na hali ya hewa ya eneo husika, mfano Mkoa wa Morogoro miwa huwa tayari kwa kuvunwa kati ya miezi 9-12 wakati Mkoa wa Kagera huchukuwa miezi 18. Hizi ni baadhi ya sababu zinazovutia uwekezaji kwenye eneo husika kulingana na matakwa ya mwekezaji,” anasema Mkurugenzi  Mtendaji wa Bodi ya Sukari Tanzania (SBT)  Henry Semwanza.

Anaongeza kuwa,  uwepo wa kiwanda cha sukari hautegemei mkoa husika kuomba kuwekewa kiwanda bali hutegemea zaidi  uwepo wa mazingira yanayofaa kwa kilimo cha miwa.

Pia hutegemea uwepo wa mwekezaji aliyetayari kuwekeza kwenye eneo husika, uwepo wa eneo yaani ardhi  kwa shamba linalofaa kwa uwekezaji.

Katika hatua nyingine, anakiri juu ya kuendelea kuwapo kwa upungufu wa takwimu  za mahitaji halisi ya bidhaa hiyo nchini hata katika mwaka uliopita kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo uzalishaji wa chini wa bidhaa hiyo kwa viwanda vya ndani ya nchi kuwa na mipaka na nchi 8 na hivyo kuwepo na magendo ya kusafirisha nje au kuingiza ndani katika mipaka mingi iliyopo wazi; kama inavyojulikana njia za panya.

“Mahitaji ya sukari nchini kwa mwaka 2016/17 yalikadiriwa kuwa  tani 590,000,  kati ya  hizo tani 135,000 ni kwa ajili ya matumizi ya viwandani na tani 455,000 ni za matumizi ya kawaida. Uzalishaji wa sukari wa ndani kwa matumizi ya kawaida ulikuwa tani 330,843.48 kwa mwaka 2016/17 hivyo kuwa na upungufu  wa tani 259,156.52.

“Sukari kwa ajili ya matumizi ya viwandani haizalishwi nchini hivyo watumiaji wa bidhaa hiyo  huagiza moja kwa moja toka nje ya nchi, ikiwamo SSB Group” anasema Semwanza.

Hivi basi wadau wanadai kuwa huo umekuwa ni uchochoro wa kupitisha magendo ya sukari.

Lakini hilo linapingwa  na wadau wengine  kuwa kile kinachodaiwa kuwa sukari kwa matumizi ya viwanda imeonekana kuuzwa nchini kwa mlango wa nyuma kama sukari ya majumbani  kwani mara nyingi wafanyabiashara wakubwa wamebambwa na wameonekana wakibadilisha mifuko ya sukari (rebagging)kutoka Brazil katika mabohari ya baadhi ya viwanda ili kuoneshwa kama imezalishwa hapa.

Anafafanua  Semwanza kuwa bodi ya sukari wameendelea kuisimamia bidhaa hiyo kutokana na matakwa ya sheria ya sukari ya mwaka 2001 kama ilivyorekebishwa mwaka 2009 na kanuni zake za mwaka 2010 ambazo zinaipa mamlaka Bodi ya Sukari kudhibiti uingizwaji wa sukari.

Licha ya Serikali kuweka mkazo kwa wafanyabiashara ikiwamo kuwasisitiza kuiachia bidhaa hiyo kabla ya kuchukuliwa hatua kali.  Bado vitisho hivyo havijawa mwarobaini wa kushuka kwa bei ya bidhaa hiyo muhimu nchini badala yake ndio kwanza ilizidi kupanda kutoka Sh 1,800 hadi kufikia na kugota  kwa Sh 2,500 kwa kilo moja hivi sasa.

“Ili kuongeza uzalishaji wa sukari nchini yapo maeneo ambayo yameainishwa kwa ajili ya uwekezaji Kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari. Bodi ya Sukari Tanzania kwa kushirikiana na wadau tayari  imeanzisha miradi midogo na ya kati wilayani Chamwino mkoani Dodoma na Geita vijijini katika mkoa wa Geita itakayoongeza uzalishaji wa Sukari nchini.

“Sambamba na hilo kuna mradi mpya unaoendelea wa Mkulazi  Holding chini ya mifuko ya hifadhi ya jamii (NSSF na PPF) kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza eneo la Mbigiri mkoani Morogoro, uliopangwa kuzalisha tani 250,000” anasema.

“Serikali kupitia Bodi ya Sukari kwa kushirikiana na mamlaka zingine inadhibiti uingizwaji holela wa sukari nchini ili kulinda uzalishaji wa ndani, kuongeza uzalishaji na kuvutia uwekezaji mpya kwenye sekta ya sukari.”

Mwezi  Oktoba mwaka jana wakati akiwapa ardhi SSB , Rais Magufuli alimwomba mfanyabiashara  huyo maarufu kutumia ardhi  hiyo kwa uzalishaji wa miwa ya sukari  ili nchi  iweze  kukuza  kutoa sukari yake badala ya kuagiza nje.

Alisema serikali imetoa hekta 10,000 baada ya kuamini kwamba Bakhresa alikuwa akiwekeza katika nchi kwa manufaa ya Watanzania wote katika bidhaa ambazo nchi haiwezi kufikia mahitaji  yake ya ndani.
Katika maneno yake, meneja wa mradi wa Bagamoyo Sugar Limited, Narayan Krishna alionyesha kwamba hatua ya kwanza ya mchakato wa uzalishaji kiwandani katika shamba hilo  utaanza mwaka 2020.

Wakati huohuo Kiwanda cha Sukari cha Kilombero (KSC) kinampango wa kuongeza uzalishaji sukari kutoka tani 126,000 za sasa hadi 250,000 kwa mwaka itakapofika mwaka 2021 katika shamba lake la Mang’ula. Mkurugenzi Mtendaji wa KSC ,Guy Williams amesema nia yao ni kufikia malengo ya uchumi wa viwanda kama serikali ilivyoazimia kufikia 2025 na kuwa nchi ya uchumi wakati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles