22.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

KUBENEA AVUNJA UKIMYA

 

Na AZIZA MASOUD -DAR ES SALAAM

WAKATI Kamati Kuu ya Chadema, ikikutana na kutarajiwa kutoa uamuzi wake leo, Mbunge wa Ubungo Saed Kubenea (Chadema), amesema hana bei na hakuna fedha itakayoweza kumnunua na hana mpango wa kuhamia CCM.

Alisema siku zote hujali utu zaidi kwa sababu  heshima waliompa wapiga kura wake ni kubwa kwake.

Akizungumza na waandishi wa habari  Dar es Salaam jana, alisema taarifa zilizogaza dhidi yake kuhusishwa   kujiunga na CCM  na kujiuzulu ubunge si za kweli.

“Napenda niwahakikishie sijawahi kuzungumza na chombo chochote cha habari kwamba nina mpango wa kutoka Chadema kwenda kwingine.

“Sijawahi kuzungumza na mtu yeyote wa CCM juu ya kwenda kwenye chama hicho ama kunishawishi.

“Nimekuwa mkosoaji mkubwa   wa serikali ya CCCM kuhusu masuala mbalimbali ikiwamo ubinafsishwaji wa mashirika ya umma na uwekezaji unaofanywa na kampuni za kigeni hapa kwetu,” alisema Kubenea.

Alisema kwa   miaka 15 amekuwa akiandika habari za uchunguzi na uchambuzi kwa kukosoa  sera ya ubifsishwaji  ambayo imewaacha watanzania maskini na kujenga nyufa baina walioo nacho na wasio nacho.

“Kwa uelewa wangu sioni jipya ambalo linaweza kunishawishi kwenda CCM na mimi sijawahi kununuliwa na huwa sinunuliki.

“Nikifanya jambo lolote ujue limetoka ndani ya moyo wangu, kama vishawishi vya fedha nimevipitia vingi  lakini sijawahi kuyumba katika msimamo wangu,” alisema Kubenea.

Alisema amekuwa katika mageuzi hayo kwa miaka 15 sasa  na kujiwekea historia ya kukosoa utawala wa CCM kuanzia wa awamu tatu uliokuwa ukiongozwa na Rais Mstaafu Benjamin Mkapa.

“Kwa miaka mingi nimekuwa nikiwakosoa kwa dhamira chama hiki kijirekebishe, kifuate itikadi yake ya ujamaa na kujitegemea, kifuate misingi yake ya asili ya utu wa mtu na siyo kitu na kitimize ahadi zake 10 za TANU… wakati huo tulikuwa tukikisema sana kwenye magazeti na CCM ilikuwa inajirekesha,” alisema.

Alisema katika   miaka 10 ya utawala wa awamu ya nne ulioongozwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete,   CCM ilikuwa inakwenda inazaliwa upya lakini hakujiunga kwa kuwa aliamini  katika  kazi za utetezi wa watu nje ya kuwa na chama.

Alisema ameweza kujenga jina lake kwa miaka 15 na kupata ubunge  na sifa nzuri za Chadema na    anaamini juhudi binafsi  za kutetea wananchi pia zimemfikisha hapo alipo.

“Sasa nimepata fursa ya kutunga sheria, mimi mbunge sina bei, nikiondoka Chadema nitaondoka kwa dhamira yangu siyo kununuliwa.

“Siyo mtu aniambie nimefikia be,i mimi sina bei, utu wangu ndiyo bei yangu,” alisema Kubenea.

Alisema hawezi kufanya uamuzi huo kwa kuwa atawasaliti wananchi wa Ubungo na Watanzania kwa kuwa walijitoa kwa kumchangia  kwa hali na mali   aweze kufanikisha safari yake ya kupata kiti hicho.

“Kuna watu nimeshiriki kuwaleta Chadema watanielewaje? Miongoni mwao yumo Sumaye (Waziri Mstaafu Frederick Sumaye) na Lowassa  (Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa).

“Watanionaje? Niwaambie tu kwamba nimesikitika sana, nimefedheeshwa mno na nimeumizwa kwelikweli na habari hizi za mimi kuondoka Chadema.

“Mimi bado mwanachama na mbunge wa jimbo la Ubungo  mpaka 2020  labda nife au kitokee kitu  kingine  ambacho sikijui.

“Lakini kwa utashi wangu nitaendelea kuwa mwanachama wa ukweli ninayekipigania chama kupitia vikao, hivyo hayo maneno yapuuzwe,” alisema Kubenea.

Alisema  hakuna mtu yeyeote aliyewahi kuzungumza naye na  kama yupo aweke ushahidi mezani.

Alisema siku zote akipewa fedha huwa si za hongo wala ushawishi wa kitu fulani isipokuwa ni msaada tu lakini siyo za ushawishi… mtu anaamua tu kumpa.

Alisema lengo la kufanya propaganda hizo ni kuwatoa wanachama wa Chadema kwenye mstari wa kuwaza uchaguzi mdogo katika majimbo ya Longido na Singida Kaskazini na Songea Mjini.

“Wanataka wanachama wetu, wabunge watumiane wenyewe kwa wenyewe wao wanajiandaa ikifika baada ya wiki moja tunapigwa.

“Wanataka wanachama wahangaike kujibu mambo ya mitandaoni,” alisema Kubenea.

RUTH MOLLEL

Naye Mbunge wa Viti Maalum, Ruth Mollel (Chadema), alikanusha madai ya kukihama chama hicho akisema hana mpango wa kufanya hivyo.

Aliyasema hayo baada ya gazeti hili kunukuu   taarifa ambayo ilimletea usumbufu mbunge huyo, taarifa  iliyotolewa na   kiongozi mmoja.

MTANZANIA inamuomba radhi Mollel kwa usumbufu alioupata.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles