25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Kova: Hatuna jasiri wa uokoaji ajali majini

Na BENJAMIN MASESE


KAMANDA mstaafu wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,   Suleiman Kova amesema tatizo la watanzania  wengi kufariki dunia  inapotokea  ajali majini  ni  kutokuwapo   watu jasiri walioandaliwa katika uokoaji wa majanga ya namna hiyo.

Aliyasema hayo  jana wakati akikabidhi  vifaa mbalimbali vya uokoaji   kwa kamati ya maafa ya mkoa na wilaya, wavuvi, wanafunzi na wamiliki wa boti na mitumbwi  jijini Mwanza.

Kova ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya SUKOS KOVA inayojihusisha na masuala ya maafa, utoaji wa misaada ya vifaa na mafunzo ya ukoaji.

Alisema licha ya kuwapo  vikosi maalumu vya uokoaji katika majanga lakini  suluhisho la kupunguza au  kumaliza   vifo vya majini   ajali inapotokea ni kutoa vifaa na  mafunzo kwa wananchi wanaoishi au kuzunguka  Ziwa Victoria  wajue  kuvitumia  waweze kujiokoa wenyewe badala ya kusubiri kuokolewa.

Alisema miongoni mwa watu   wanaopaswa kuandaliwa kama  jasiri wa kuokoa ni wavuvi na baadhi ya watu wengine ambao maisha yao yanategemea   maji na kupewa vifaa vya aina zote za majanga.

“Baada ya kustaafu niliona niendelee kuihudumia jamii ambako nilianzisha taasisi ya SUKOS KOVA.

“Kazi yetu ni kuwatumikia wananchi wa chini   kwa kuwaongezea uelewa  namna ya kujiokoa wakati wa ajali za majini, pia kuwapatia vifaa na kutoa mafunzo ya majanga ya moto.

“Binafsi, ajali ya MV Nyerere inihuzunisha sana hasa  nilipoelezwa kwamba watu wengi walikufa   wanawake wakiwa  168.

“Kuna msemo unasema ajali haiepukiki lakini nasema  tunaweza kuepuka madhara   kwa kuandaa watu jasiri wa uokoaji na kuwapa vifaa vyote, tatizo hatuna na hatujaandaa  jasiri ambao muda wote shughuli zao majini.

Kova alisema ikiwa wavuvi watapewa mafunzo na vifaa na kutanguliza uzalendo, vifo vitokanavyo na ajali za majini vitaisha   kwa sababu  wao ni wazoefu wa shughuli za majini.

Aliziomba kamati za maafa za mkoa na wilaya kuandaa timu za uokoaji ambazo zitahusisha makundi mbalimbali ya watu wakiwamo wanafunzi wa  shule za msingi.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Dk.Philis Nyimbi   alisema kama Serikali imefarijika kuzinduliwa programu hiyo kwa mkoa huo na kuahidi kushirikiana kuhakikisha vifaa hivyo vinatumika katika maeneo husika.

Dk.Nyimbi alisema muda wote wa mafunzo kwa makundi mbalimbali Serikali itakuwa bega kwa bega kusimamia hatua hiyo.

Vifaa mbalimbali vilivyotolewa vikiwamo boya, redio za mawasiliano, nguo za uzamiaji na vifaa vya kuzimia moto vilikuwa na thamani ya Sh milioni 120 ambavyo vitagawia katika shule, wavuvi, kamati za mafia za mkoa na wilaya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles