23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

KORTI YAIDHINISHA USHINDI WA KENYATTA

Nairobi, Kenya

MAHAKAMA Kuu ya Kenya imeidhinisha ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta baada ya kutupilia mbali mapingamizi mawili ya kupinga uchaguzi wa marudio ulifanyika Oktoba 26, mwaka huu.

Katika hukumu, jopo la majaji sita walitoa uamuzi kuwa kesi hizo hazina msingi na kumtangaza Kenyatta kuwa mshindi halali wa marudio ya uchaguzi.

“Baada ya kuchunguza kwa makini masuala yaliyotajwa hapo juu, wahusika katika kila mashtaka, pamoja na katiba na sheria zinazohusika, mahakama imefanya uamuzi kwamba maombi hayana msingi,” alisema Jaji Mkuu David Maraga.

Jaji Maraga alisema majaji kwa kauli moja wameamua kwamba kesi zote mbili hazina msingi. Kesi ya Mbunge Harun Mwau na wanaharakati wawili Njonjo Mue na Khelef Khalif zimetupiliwa mbali.

“Kwa matokeo ya Uchaguzi wa Rais wa Oktoba 26, mshindi wa urais ni Uhuru Kenyataa,” alisema.

Kwa mujibu wa katiba ya Kenya, baada ya uamuzi huo, Kenyatta na mgombea mwenza William Ruto, wataapishwa Novemba 28 kwa muhula wa pili.

Katiba ya Kenya inasema Rais aliyechaguliwa anafaa kuapishwa siku ya saba baada ya kutolewa kwa uamuzi wa mahakama wa kuidhinisha uchaguzi iwapo kulikuwa na kesi iliyokuwa imewasilishwa.

Katika marudio ya uchaguzi, Kenyatta alitangazwa mshindi wa urais akiwa na kura 7,483,895 sawa na asilimia 98,  huku mpinzani wake Odinga aliyesusia uchaguzi huo, alipata kura 73,228 sawa na asilimia 0.96.

Jumla ya wapigakura 7,616,217 walishiriki uchaguzi huo kati ya jumla ya wapigakura 19.6 milioni ambao wamejiandikisha, ambayo ni asilimia 38.84. Hata hivyo, wapigakura zaidi ya milioni 12 waliojiandikisha hawakushiriki katika marudio ya uchaguzi huo.

Uamuzi wa mahakama hiyo unakuja baada ya vurugu za kisiasa kuzuka jijini Nairobi mwishoni mwa wiki iliyopita na kusababisha vifo, maandamano na uharibifu wa mali.

Novemba  17, mwaka huu, watu watano waliuawa wakati polisi wakitawanya wafuasi wa Odinga, ambao walikuwa wakimpokea akitoka nchini Marekani.

Septemba, mwaka huu, Mahakama ya Juu ilitangaza kurudia kwa uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti, mwaka huu baada ya ushindi wa Kenyatta kutenguliwa.

Baada ya uamuzi ya mahakama, mgombea mwenza wa Kenyatta, Ruto aliandika katika mtandao wa Twitter kwamba: “Halleluyah! Atukuzwe Mungu aliye mbinguni. Amelikumbuka taifa letu na kutupatia matumaini na mustakabali.”

 RAILA ODINGA

Kiongozi wa muungano wa upinzani, Odinga ambaye alisusia uchaguzi huo, amepinga uamuzi uliotolewa na mahakama wa kuidhinisha urais wa Kenyatta.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, Odinga kupitia taarifa iliyotolewa na mshauri wake, Salim Lone, amesema kuwa Serikali ya Jubilee si halali akiongezea kwamba uamuzi huo wa Mahakama ya Juu ulifanywa kupitia shinikizo.

”Sisi  Nasa, tayari tulikuwa tumeamua kabla ya uamuzi wa mahakama kwamba hatuitambui Serikali ya Uhuru Kenyatta. Ni uamuzi uliotolewa chini ya shinikizo kubwa, hatushutumu mahakama, tunaihurumia,” alisema kuelezea kuwa uamuzi huo haukumshangaza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles