Kope bandia, wanja husababisha upofu

0
559

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

WANAWAKE wanaopaka wanja chini ya macho na wale wanaobandika kope bandia, wapo hatarini kupata upofu.

Hayo yalielezwa jana jijini hapa na Kaimu Meneja wa Mpango wa Taifa wa Huduma ya macho, Dk. Bernardetha Robert, wakati akizungumza kwenye kilele cha siku ya afya ya macho duniani.

Maazimisho hayo yalienda sambamba na utoaji wa huduma ya kupima wananchi macho shughuli iliyofanyika katika viwanja vya Nyerere Square.

Dk. Bernadetha alisema wakati wa uwekaji wa kope bandia, huwa kuna maji maalum ambayo yamekuwa yakitumika kugundishia karibu na kingo ya jicho.

Alisema maji hayo yanamadhara makubwa na wanawake wengi wamekuwa wakipata madhara ikiwemo macho kuvimba na wakati mwingine kushindwa kuona.

Dk. Bernadertha alisema sababu hiyo na ile ya kupaka wanja karibia na macho, zimekuwa ni mojawapo ya sababu ambazo zimekuwa zikichangia upofu.

“Wanawake wengi wanakuja kwetu macho yakiwa yamevimba sababu ni wanja na kope za bandia, tunawashauri kuacha matumizi hayo na jicho linatakiwa muda wote liwe safi hasa sehemu za nje ya jicho,”alisema.

Dk. huyo alisema bado jamii ya kitanzania haizingatii vyema utunzaji wa afya ya macho, hivyo aliwaasa kujenga utaratibu wa kupima angalau mara moja kwa mwaka.

“Tusinunue dawa bila ya kuandikiwa na daktari. Tusipake ama kubandika vitu vigeni kwenye vifuniko vya jicho ama kingo za vifuniko vya jicho kama vile rangi. Tusivae miwani bila kupimwa na mtaalamu wa macho,” alisema Dk. Bernardetha.

Kaimu Meneja huyo wa Mpango wa Taifa wa Huduma ya macho, alisema taarifa kutoka mikoa 9,watu 5000 wamefanyiwa uchunguzi huku 200 wakifanyiwa upasuaji.

Alisema kwa Mkoa wa Dodoma, wamefanya ushauri na uchunguzi kwa magonjwa yasiyoambukiza ambapo jumla ya watu 368 walifanyiwa vipimo vya sukari, shinikizo la damu na kiwango cha unene.

“Asilimia 3 walikutwa na kiwango cha juu cha sukari,asilimia 47 walikutwa na shinikizo la juu la damu na asilimia 50 walikutwa na kiwango cha unene uliopitiliza,”alisema.

Naye,Veronika Maganza ambaye alifika katika viwanja hivyo kwa ajili ya kupatiwa huduma, alisema alikuwa na tatizo ya jicho moja kutoa machozi na kwa sasa anasubiria ili aweze kufanyiwa upasuaji wa jicho hilo.

“Nilikuwa napita nikaona watu wamejaa kwa sababu mimi nina tatizo la macho nikaja kupima, sasa nasubiria kufanyiwa upasuaji,”alisema.

Kwa upande wake, Didas Komedi, aliiomba Serikali kupeleka wataalamu katika maeneo ya vijijini kwani ndiko kwenye wagonjwa wengi.

“Niwashukuru sana hawa walioandaa hili ila niwaombe waende vijijni zaidi,”alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here