24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Kondomu, ARV’s kuadimika mitaani

kondomuVeronica Romwald Na Harieth Faustine -DAR ES SALAAM

HATUA ya wafadhili wa miradi ya afya nchini kufunga miradi yao kuna hatari ya kuadimika kwa mipira ya kiume (kondomu) pamoja na dawa za kufubaza makali ya virusi vya Ukimwi (ARV’s).

Kitendo hicho kinaonekana huenda kikaigharibu Serikali hasa baada ya kutangaza mapambano na baadhi ya taasisi ambazo zimekuwa zikisambaza vilainishi kwa lengo la kuzuia maambukizi ya Ukimwi hali iliyotafsiriwa kwamba inakwenda kinyume na haki za binadamu kwa kuingilia kazi za NGO.

Taarifa iliyotolewa juzi kwa umma na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Tanzania Markenting and Communications (T-Marc Tanzania),  Diana Kisaka  ilieleza kufungwa kwa mradi huo ambao ulikuwa unafadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Msaada la Marekani (USAID).

Taarifa hiyo ilieleza kuwa shirika hilo lilikuwa likifanya kazi ya kuboresha upatikanaji wa huduma za afya na maendeleo nchini ambapo kazi hiyo walikuwa wakifanya kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa lengo la kuhakikisha zinapatikana bidahaa bora za afya nchini.

“Bidhaa zinazosambazwa na T-Marc ni pamoja na miradi tunayoiendesha nchini ambayo ni kuboresha afya ya uzazi ya mama na mtoto, lishe bora, kupunguza maambukizi ya magonjwa hatari kama ukimwi na malaria.

“Mbali na hilo pia tulikuwa tunahamasisha upatikanaji wa matumizi ya maji safi na salama, saratani ya mlango wa kizazi na utoaji elimuya hedhi pamoja na vifaa vya kujisitiri wakati wa hedhi kwa wasichana,” ilieza taarifa hiyo

Mkurugenzi huyo katika taarifa yake alisema kuwa wamekuwa wakitekeleza mradi wa Tanzania Social Marketing (TSMP) kwa kushirikiana na Population Services Internation (PSI) na kufadhiliwa na Shirika la Msaada la Marekani (USAID) kwa kipindi cha miaka sita toka 2010 hadi 2016.

Novemba mwaka jana shirika hilo lilizindua aina mbili mpya za mipira ya kiume aina ya Dume Extreme na Dume kama njia ya  kupunguza utegemezi ya ruzuku kutoka kwa wafadhili katika shughuli za wasambazaji wa mipira hiyo.

“Lengo la tangazo hili ni kutoa taarifa ya kufungwa kwa mradi wa TSMP ifikapo Desemba 31, mwaka huu na T-Marc itakamilisha malipo yote yanayohusiana na mradi huu. Hivyo taasisi, watu binafsi wanaombwa kuwasilisha Ankara za madai pamoja na nyaraka muhimu kabla ya tarehe tajwa,” ilieleza taarifa hiyo.

Hatua hiyo huenda ikazidi kuitikisa sekta ya afya baada ya muda wa miradi mikubwa iliyokuwa inatekelezwa  kwa ufadhili wa Shirika la USAID kufika mwisho.

Akizungumza na MTANZANIA jana kuhusu hali hiyo Msemaji wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Nsachris Mwamwaja alisema hana taarifa za kufungwa kwa mradi huo na kuahidi kuzungumzia suala hilo hii leo.

“Sina taarifa za kufungwa kwa mradi, ndiyo kwanza unaniambia hizo taarifa, bahati mbaya umenipigia saa hizi nimeshatoka ofisini najua tarifa hizo kesho (leo) zitatoka, nipigie kesho mapema nitazungumza,” alisema.

Hivi karibuni Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubsya alisema. “Wadau hawa walikuwa katika miradi ambayo ilikuwa chini ya  USAID katika kupambana na malaria   na mfumo wa utoaji na usambazaji wa dawa za kupambana na   Ukimwi kupitia mradi wake wa SCMS.

Miradi hiyo mikubwa ni pamoja na ile ya ununuzi wa dawa, vifaa tiba na misaada ya  ufundi katika sekta hiyo, utoaji wa elimu kwa wanazuoni, usambazaji na usimamizi wa vifaa vya tiba kwa   miaka 10 iliyopita.

“Walikuwa wanatoa huduma hizo kwa kushirikiana na taasisi nyingine za afya nchini ikiwamo Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) na Bohari Kuu ya Dawa (MSD),” alisema.

Dk. Ulisubsya alisema miradi hiyo imesaidia kuongeza idadi ya watu wanaotumia dawa za kupunguza makali ya   Ukimwi (Arv’s) kutoka watu 150,000 miaka 10 iliyopita hadi kufikia watu 800,000 hivi sasa,” alisema.

Katibu mkuu huyo aliweka wazi kuwa wadau kama hao wanapoondoka nchini baada ya muda wao wa kusimamia miradi kuisha, miradi hiyo hutetereka katika uendeshaji na hata kufa.

Hatua ya kuondoka kwa wafadhili hao zinaweza kuwa pigo kubwa kwa katika sekta ya afya nchini kutokana na miradi hiyo kutegemea wafadhili wa nje kwa asilimia 90 huku   Marekani ikiwa kinara wa ufadhili huo.

Taarifa mbalimbali zinaonyesha kuwa baadhi ya miradi ambayo wafadhili waliwahi kujitoa,  imedorora au imekufa.

Miradi hiyo ni pamoja na Mpango wa Taifa wa Damu Salama ambao awali ulikuwa ukifanya vizuri, lakini hivi sasa umetetereka baada ya wadau kujitoa na kuukabidhi kwa Serikali.

Hivi karibuni, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ilisimamisha ghafla matibabu ya bure kwa wagonjwa wa seli mundu (sickle cell) ambao walikuwa wakitibiwa kwa ufadhili wa Serikali ya Uingereza kupitia Shirika la Welcome Trust.

Shirika hilo lilifadhili matibabu hayo kwa  miaka 10 na ulikuwa ukisimamiwa na Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS) tangu mwaka 2004 na  ulihitimishwa Machi, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, ofisini kwake, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alizitaka taasisi zisizo za kiserikali na asasi za kiraia kuendelea kutoa huduma za afya kwa makundi maalumu, lakini si kusambaza vilainishi.

Tamko hilo linakuja zikiwa zimepita siku chache baada Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe  kupiga marufuku vitendo vya ushoga, kwani ni kinyume na sheria za nchi.
Alisema katika utoaji wa huduma kwa makundi maalumu kwa wenye maambukizi ya virusi vya Ukimwi, maambukizi yameshuka na kufikia asilimia 5.1 ambapo awali ilikuwa asilimia 7.2 .

“Kumekuwa na baadhi ya  taasisi na asasi ambazo zinachapisha vipeperushi, matangazo na kusambaza vilainishi ili kuchochea ushoga na ndoa za jinsia moja.

“Makundi yanayoathirika zaidi na maambukizi ya VVU ni wavulana, wasichana walio katika umri wa kubalehe, yatima, wafungwa, wakimbizi, madereva wa magari makubwa na wafanyakazi wa mashambani,” alisema.

Alisema katika watu 1000 watu 51 kati yao wanaishi na maambukizi na vijana wenye miaka 15-24 wana asilimia 35 ya maambukizi.

Alisema wasichana wanaofanya ngono wanapata maambukizi kwa asilimia 26 huku wanaojidunga sindano za madawa ya kulevya ni asilimia 36.

“Wadau watakuwa wakipangiwa maeneo ya kutolea huduma za afya na mganga mkuu kulingana na maambukizi, si kuchagua wenyewe kama ilivyokuwa hapo awali ambapo mtu anatoa huduma sehemu moja tu” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles