25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

KOMBE LA SHIRIKISHO LIMETUONYESHA VITU VINGI

NA AYOUB HINJO

KILA kilichotokea kwenye michuano ya Kombe la FA kimeonyesha jinsi soka la  Tanzania lilivyopiga hatua ya maendeleo.

Kwa kiasi kikubwa timu za madaraja ya chini zimekuwa katika kiwango bora ambacho kimedhihirisha kuwa nchi hii imezungukwa na vipaji vingi sana.

Hakuna aliyeamini kilichoitokea Simba dhidi ya Green Warriors. Ni bingwa mtetezi lakini alitolewa katika hatua ya awali na timu hiyo ya Daraja la Pili.

Kombe hili la FA ni msimu wa tatu tangu lilipoanzishwa. Awali hakukuwa na njia nyingine ya kuzikutanisha timu za chini na hizi za Ligi Kuu.

Tangu kuanzishwa kwa michuano hii, timu hizo zimejizatiti kuonyesha uwezo wao kupitia wachezaji wao.

Kwa ukaribu zaidi na jambo la kufurahisha timu hizo nyingi zimekuwa na sura za vijana wadogo ambao ndio msingi mzuri katika soka letu kwa miaka michache ijayo.

Kinachotokea kwenye michuano hiyo hakitofautiani na kinachotokea katika ligi za Ulaya. Timu za ligi za chini zimekuwa zikitoa changamoto kwa timu za Ligi Kuu.

Manchester United iliondoshwa katika michuano ya Carabao kwa kufungwa na Bristol City, Arsenal waliondolewa katika michuano ya FA kwa kufungwa na Nottingham Forest.

Hata Real Madrid nao walitolewa Copa Delay na timu ya daraja la kwanza nchini Hispania. Ni hatari kweli lakini ndiyo njia nzuri ya kutafuta vipaji.

Timu ya Yanga ilikuwa chupuchupu kuondoshwa katika michuano ya FA na timu ya Ihefu, lakini walishinda kwa mikwaju ya penalti. Hata Singida United wamefuzu hatua inayofuata baada ya kutolewa jasho na Green Warriors.

Ushindani unaotolewa na timu za Daraja la Kwanza, la Pili na hata timu za Ligi za Mkoa umekuwa mkubwa huku kila timu ikiamini kucheza na timu za Ligi Kuu ndiyo njia sahihi ya wao kutoka katika timu zao.

Wachezaji wengi wanaocheza hizi timu za Ligi Kuu wametoka katika timu hizo baada ya kuonyesha viwango bora dhidi yao.

Kwa muda ambao upo na utakaokuja itafika mahala ambapo itakuwa ngumu kutabiri matokeo ya kila timu pindi zinavyokutana.

Hakuna njia nyingine ya timu za chini kupata uzoefu zaidi ya hii ya kukutana na timu za Ligi Kuu ambazo zinapitia mambo mengi kwenye ligi yao.

Kingine kinachofanya michuano hii ionekane bora ni jinsi inavyoonyeshwa, ndiyo njia sahihi ambayo timu nyingi za chini huamini ndio muda sahihi wa kuonyesha uwezo wao.

Msimu uliopita Simba walicheza dhidi ya Madini FC jijini Arusha, kuna mchezaji anaitwa Awesu Awesu ambaye hivi sasa yupo Mwadui FC, alionyesha kiwango kizuri kiasi cha kuwashawishi Mwadui kumsajili wakiamini ataweza kuongeza kitu kwenye timu yao.

Kwa maana hiyo unaweza kuona jinsi michuano hii inavyosaidia wachezaji kuonekana kwa urahisi na kuvutia timu nyingine kwa viwango vyao.

Maendeleo ya mpira yanaanzia katika ligi za chini, hata timu hizo zinazocheza ligi hizo hujifunza vitu vingi kutoka katika timu za Ligi Kuu na kuzifanyia kazi kwa ufasaha.

Kwa muda mfupi tu tangu michuano hii imeanza, kuna mabadiliko mengi yametokea huku kila timu ikiamini ndiyo njia sahihi ya wachezaji wao kuuzwa na hata timu pia kujifunza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles