25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

KOMBE LA DUNIA…AFRIKA KUMALIZA MKOSI WA NUSU FAINALI?

CAIRO, Misri


ZIMEBAKI wiki kadhaa kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia ambazo mwaka huu zitafanyika Urusi ikiwa ni mara ya kwanza kwa Taifa hilo la Ulaya Mashariki kuziandaa.

Hata hivyo, mbali ya mengi yanayosubiriwa, macho na masikio ya mashabiki wa soka Afrika yatakuwa kwa wawakilishi wao katika fainali hizo.

Matumaini ya soka la Afrika yatabebwa na timu tano kati ya 32 zitakazokuwa nchini humo kulifukuzia taji la mashindano hayo ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

Nigeria, Senegal, Misri, Morocco na Tunisia ndizo zitakazoliwakilisha Bara hili, ambalo tangu kuanzishwa kwa michuano hiyo, halijawahi kushuhudia mwakilishi wake akitinga nusu fainali.

Baada ya miaka mingi ya Afrika kuishia robo, Ghana walikaribia kuandika historia kwa kutinga nusu fainali mwaka 2010 lakini walizidiwa kete na Uruguay baada ya Luis Suarez kuzuia kwa mkono shuti la Stephen Appiah lililokuwa likielekea wavuni.

Huku mchezo huo ukielekea kumalizika na timu hizo zikiwa sare ya bao 1-1, mwamuzi alimlima kadi nyekundu Suarez na kuipa penalti Ghana ambayo hata hivyo Asamoah Gyan alishindwa kuiweka kimiani. Baadaye, wawakilishi hao wa Afrika wakaondoshwa kwa mikwaju ya penalti.

Je, katika fainali zijazo za majira ya kiangazi, Misri, Morocco, Nigeria, Senegal na Tunisia zitaweza kuibeba Afrika na kuipeleka nusu fainali?

Nigeria

Nigeria imezikosa mara moja pekee tangu mwaka 1994. Ilikata tiketi ya kwenda Urusi ikiwa Kundi B lililokuwa na Zambia, Cameroon na Algeria.

Walishinda mechi nne na kutoa sare mbili katika mechi sita za makundi. Licha ya safu yao ya ushambuliaji kufunga mabao nane, mabeki walikuwa hovyo, wakipitisha saba.

Wakali hao wa Afrika Magharibi wamepangwa Kundi D lenye Croatia, Island na Argentina.  Nigeria imefungwa mara zote nne dhidi ya Argetina.

Hata hivyo, ushindi wao wa mabao 4-2 katika mechi ya kirafiki iliyochezwa Novemba, mwaka jana, inaibua matumaini mapya kwa Super Eagles.

Morocco

Hizo zitakuwa ni fainali za tano kwa Morocco kushiriki lakini mara yao ya mwisho kuzigusa ilikuwa mwaka 1998.

Katika mechi sita za kufuzu, ikiwa chini ya nahodha wake anayeichezea Juventus, Mehdi Benatia, ilizipiku Ivory Coast, Gabon na Mali, ikishinda mechi tatu na kutoa sare tatu.

Itakwenda Urusi ikiwa inajivunia kocha mzoefu raia wa Ufaransa, Herve Renard, ambaye amenyakua mara mbili taji la Afcon akiwa na Zambia (2012) na Ivory Coast (2015).

Timu hiyo imepangwa Kundi B lenya vigogo wa soka la Ulaya, Hispania na Ureno, huku Iran ikionekana kuwa timu pekee dhaifu.

Misri

Misri watakwenda Urusi zikiwa ni fainali zao za tatu za Kombe la Dunia ingawa hawajashiriki tangu mwaka 1990.

Safari yao ya kufuzu haikuwa nyepesi kwani walikuwa kundi moja na Uganda, Ghana na Congo.

Huku kocha wake raia wa Argentina, Hector Cuper, akikabiliwa na ukosolewaji mkubwa, ilimaliza mechi za kufuzu ikiwa imefunga mabao manane pekee ingawa tangu ateuliwe ameshinda mechi 20 kati ya 30.

Ikijivunia makali ya staa wake, Mohamed Salah, droo ya fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu imewaweka Kundi A lenye Urusi, Saudi Arabia na Uruguay.

Tunisia

Timu hiyo inayonolewa na kocha mzawa Nabil Maaloul, haikufungwa katika mechi zake za kufuzu licha ya kuwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Libya na Guinea, ikishinda nne na kutoa sare mbili.

Katika fainali zijazo za Kombe la Dunia, mtihani wake mkubwa ni kuzipiku Ublegiji, England na Panama zilizowekewa Kundi G.

Tunisia watakwenda Urusi wakiwa na kikosi chenye wachezaji wengi wanaocheza ligi ya ndani, tofauti na mataifa mengine ya Afrika.

Senegal

Mashabiki wa soka wa Senegal wataishuhudia timu yao ikicheza fainali hizo kwa mara ya pili. Wakati timu hiyo ikishiriki michuano hiyo mwaka 2002, kocha wake wa sasa, Aliou Cisse, alikuwa nahodha.

Senegal walikata tiketi ya kwenda Urusi baada ya kuzipiku Afrika Kusini, Burkina Faso na Cape Verde iliyokuwa nazo kundi moja katika mechi za kufuzu.

Timu hiyo haikupoteza katika mechi zake zote sita za kufuzu, ikishinda nne na kutoa sare mbili. Pia, ilifuzu ikiwa imefunga mabao 10, huku safu yake ya ulinzi ikiruhusu matatu pekee.

Nchini Urusi, wakiwa na nyota wake anayefanya vizuri katika kikosi cha Liverpool, Sadio Mane, watakuwa wakiiwania hatua ya 16 wakiwa Kundi H ambalo linazijumuhisha Poland, Columbia na Japan.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles