Klabu ya Simba matatani sakata la Mo Dewji

0
1267

Na WAANDISHI WETU – DAR ES SALAAM

Mfanyabiashara Nilesh Suchak ni miongoni mwa watu wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi nchini akihusishwa na tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini, Afrika na duniani, Mohammed Dewji, anayetambulika pia kwa jina la Mo.

Mbali na Nilesh, wengine wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi ni baadhi ya viongozi wa timu ya Simba, akiwamo  Msemaji wake,  Haji Manara.

Mfanyabiashara huyo anayetajwa na Jarida maarufu duniani la Forbes kama bilionea kijana barani Afrika, alitekwa juzi alfajiri katika Hoteli ya Colloseum, Oysterbay Jijini Dar es Salaam, mahali ambako amekuwa akifanyia mazoezi (gym).

Taarifa za Nilesh ambaye ni mmoja wa viongozi wanaoendesha kampuni inayouza na kusambaza mafuta ya State Oil inayotajwa kumilikiwa kwa asilimia 100 na Watanzania  kukamatwa,  zilithibitishwa kupitia simu yake ya mkononi ambayo gazeti hili liliipata kupitia tovuti ya kampuni hiyo.

MTANZANIA Jumamosi lilipiga namba hiyo ya Nilesh, ambaye katika tovuti hiyo ametambulishwa kama Mwenyekiti wa Kampuni ya State Oil, na kupokewa na mtu mwingine ambaye licha ya kukataa kujitambulisha, alilithibitishia gazeti hili kuwa ni kweli amekamatwa.

Mtu huyo aliliambia gazeti hili kwamba pamoja na kwamba Nilesh amekamatwa akihusishwa na tukio hilo, anayeweza kutoa maelezo zaidi ni Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa.

Jana mara kadhaa gazeti hili liliwasiliana na Mambosasa, ambaye alithibitisha kukamatwa kwa watu kadhaa wengine, hakuwataja majina na aliyemtaja ni Manara.

Alipoulizwa kuhusu kukamatwa kwa Nilesh, Mambosasa alilieleza gazeti hili hayupo ofisini, bali kwenye kazi maalumu, mara moja alikata simu.

Watu wanaomfahamu Nilesh wanasema mbali na kujishughulisha na biashara ya mafuta, pia amekuwa karibu na Klabu ya Simba, akiwa ni miongoni mwa watu wanaounda kundi la Friends of Simba.

Juzi Kamanda Mambosasa alisema wanawashikilia watu 12 kutokana na tukio hilo.

Jana gazeti hili mbali na kufika nyumbani kwa Mo na Polisi, lilikwenda pia katika Hoteli ya Coloseum  ambako mbali na kulikuta gari la mfanyabiashara huyo  likiwa katika eneo lile lile lililokuwapo tangu siku ya tukio, pia lilipata taarifa kuwa meneja wa hoteli hiyo naye anashikiliwa na Jeshi la Polisi.

Mmoja wa wafanyakazi wa hoteli hiyo aliliambia gazeti hili kuwa, Jeshi la Polisi, ambalo limeweka kambi hapo tangu siku ya tukio, lilimchukua meneja wa hoteli hiyo kwa mahojiano na hadi jana jioni walikuwa hawajamwachia.

“Meneja wetu ni mtu kwenye asili ya Kiasia, amechukuliwa hapa na gari la polisi saa nne asubuhi leo (jana), polisi wapo wengi hapa, isipokuwa wengine wamevaa nguo za kiraia hatuwezi kuwaona,” alisema mfanyakazi huyo.

Alisema hata walinzi watano ambao walikamatwa juzi bado walikuwa wanashikiliwa na jeshi hilo.

Gazeti hili lilishuhudia shughuli za uendeshaji hoteli zikiendelea katika eneo hilo kama kawaida na miongoni mwa maeneo ambayo yanaendelea kufanya kazi ni pamoja na lile la mazoezi (gym), ambalo mara tu baada ya tukio hilo kutokea lilifungwa kwa muda.

MTANZANIA Jumamosi pia lilishuhudia ulinzi wa hali ya juu kuanzia geti la kuingilia hotelini hapo, ambako kulikuwa na askari mmoja aliyevalia sare za Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) akiwa amekaa kwenye kiti pamoja na walinzi wa Kampuni ya G1.

Gazeti hili lilionana na kuzungumza na   Msimamizi wa Hoteli ya Coloseum, Faizan Osman, ambaye katika tukio la Mo ameteuliwa kuwa msemaji wake, ambapo alisisitiza kuwa kwa sasa hawako tayari kuzungumzia suala hilo hadi Jumatatu.

“Hatuwezi kuongea kwa sasa, labda tutaongea Jumatatu,  tukiwa tayari tutawaita waandishi wa habari wote kwa pamoja na mtajua kinachoendelea,” alisema Osman.

Saa 48 za kupotea kwa Mo

Wakati Jeshi la Polisi likieleza kuendelea na operesheni maalumu ya kuhakikisha Mo anapatikana, jana kiza kinene kiliendelea kutanda juu ya mahali alipo na waliomteka, hata baada ya Kamanda Mambosasa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kudai kuwa waliotekeleza tukio hilo ni wazungu, hoja ambayo imezua maswali namna walivyofahamu uraia wao mara moja, licha ya watu hao kudaiwa kuvalia kininja.

Hadi kufikia saa 11 alfajiri ya leo, ikiwa Mo atakuwa bado hajapatikana, atakuwa ametimiza saa 48 tangu kutekwa kwake saa kama hizo juzi.

Gazeti hili lilifika nyumbani kwa Dewji, eneo la Oysterybay na kukuta gari aina ya Defender la Kampuni ya  ulinzi ya G1 likiwa limeegeshwa nje ya geti, huku ndani kukiwa na walinzi wawili.

Mwandishi wa Habari wa gazeti hili alishindwa kuingia ndani baada ya kukataliwa na mlinzi aliyekuwa getini aliyedai kuwa wasemaji wa familia hiyo hawakuwapo.

Hadi tunakwenda mitamboni jana jioni, taarifa kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zilidai kuwa bado watu waliokamatwa waliendelea kushikiliwa, huku idadi yao ikizidi kuongezeka.

Chanzo kimoja ndani ya jeshi hilo kilisema hadi mchana kulikuwa kuna vikao vya viongozi wa jeshi hilo.

Juzi baada ya tukio hilo kutokea watu walioshuhudia tukio hilo waliliambia gazeti dada la hili la MTANZANIA kuwa Mo alivyofika kwenye hoteli hiyo na gari yake alikuwa akifuatiliwa kwa nyuma na gari jingine.

Mashuhuda walieleza kuwa, baada ya kufika eneo la maegesho ya magari, Mo, ambaye ni miongoni mwa mabilionea vijana Afrika, hakukawia kutoka katika gari lake  na alipotoka tu, watekaji hao walimvamia na kumkamata na kabla hawajamwingiza katika gari lao walifyatua risasi juu na kisha kutokomea kusikojulikana.

Kabla ya utekaji huo, chanzo kilichozungumza na gazeti hili hotelini hapo kilieleza picha za kamera zinaonyesha jinsi watekaji hao walivyoingia wakiwa nyuma ya gari la Mo wakimfuatilia.

Ilielezwa kuwa, tofauti na gari lililokuwa likimfuatilia, kulikuwa na gari jingine ambalo lilitangulia na lilikuwa limeegeshwa eneo la hoteli hiyo, ambako Mo hupenda kuegesha, na hivyo alivyofika magari hayo yalikuwa sambamba naye.

Kwamba picha za kamera za usalama hotelini hapo, zinaonyesha kitendo cha kumvamia Mo na kumwingiza kwenye gari ya watekaji, kilichukua karibu sekunde tano, kwa vile hakuwa mbishi.

Hadi sasa, taarifa za kutekwa mfanyabiashara huyo mkubwa zimekuwa gumzo si tu nchini, bali hata nje ya bara la Afrika, kwani taarifa zake zimeripotiwa na vyombo vingine vya kimataifa, ikiwamo BBC, CNN na VOA.

MASAKI YAZIZIMA

Taarifa za juzi na jana usiku kutoka kwa watu wanaoishi maeneo ya Oysterbay jijini Dar es Salaam ambako ndiko nyumbani kwa Mo pamoja na eneo jirani la Masaki zinaeleza kuwa kulizizima kutokana na tukio hilo.

Inaelezwa kuwa, hali ilikuwa ya utulivu katika barabara za maeneo hayo, huku katika sehemu za starehe zikiwa na watu wachache isivyo kawaida.

Taarifa za kutekwa kwa Mo zimezua gumzo katika maeneo mbalimbali, hususan katika vyombo vya usafiri pamoja na vijiwe.

Kisomo cha Simba,

Mchungaji asema atapatikana leo

Juzi na hata jana waumini wa madhehebu mbalimbali waliendelea kuendesha maombi na visomo ambavyo wanaamini vitasaidia kumrejesha akiwa salama.

Jana wanachama wa timu ya Simba walifanya dua Makao Makuu ya klabu hiyo, kuanzia saa 8, ya kumwombea Mo, ambaye ni mlezi na mwekezaji wa timu hiyo.

Dua hiyo ilihusisha uchinjaji wa mbuzi wawili na ilihudhuriwa na baadhi ya viongozi, wanachama na mashabiki wa Simba.

MTANZANIA Jumamosi lilishuhudia mwitikio mkubwa, huku wanawake nao wakiwa hawako nyuma.

Mbali na dua hiyo, jana kulikuwa na tangazo kutoka kwa Mchungaji wa Mitume, Manabii na Maaskofu Tanzania, Komandoo Mashimo, akiomba Watanzania waondoe hofu maana Roho wa Mungu amemwambia Mo atapatikana leo.

Mchungaji Mashimo alidai kuwa, hilo linawezekana kama ambavyo alidai kuomba kwa ajili ya kupatikana kwa watoto na vijana ambao walitoweka.

Miongoni mwa watoto hao ambao alidai kuwaombea na wamepatikana ni mtoto wa Mhariri wa Habari, Elvan Stambuli, Christopher Stambuli, ambaye alipotea Septemba 23, mwaka huu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here