27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Kizimbani kwa kumkata mkono albino

NA WALTER MGULUCHUMA, KATAVI
WATU wanane wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi kujibu shitaka la kumjeruhi kwa mapanga na kisha kumkata mkono Lemi Luchumi (30) ambaye ni mlemavu wa ngozi (albino), mkazi wa Mwamachoma, Tarafa ya Mamba, Wilaya ya Mlele na kisha kutokomea nao.
Watuhumiwa hao waliopandishwa kizimbani jana mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda, Odira Amworo ni Alex Manyanza (24), Nogele Maliganya, Galula Nkuba (45), Shile Jilala (27), Masunga Kashinje (34), Maiku Punga (27) na Koga Silanga (32) wote wakazi wa Kijiji cha Majimoto.
Mwendesha mashitaka na Mwanasheria wa Serikali Mkoa wa Katavi, Hongera Mwakifimbo, alidai mahakamani hapo kuwa watuhumiwa walitenda kosa hilo Mei 14, mwaka huu saa 6 usiku nyumbani kwa wazazi wa Lemi katika Kijiji cha Mwamachoma.
Watuhumiwa hao wanadaiwa siku ya tukio walikwenda nyumbani kwa kina Lemi ambako walimkuta amelala, wakaanza kumshambulia kisha wakamjeruhi kwa mapanga sehemu ya mkono wake.
Mwakifimbo alidai baada ya kumjeruhi, walifanikiwa kumkata kiganja cha mkono wake na kutoweka nacho.
Baada ya kusomewa mashitaka, washitakiwa wote kwa pamoja walikana kutenda kosa hilo na kuiomba mahakama iwape dhamana.
Hata hivyo, ombi lao lilipingwa vikali kwa kile kilichodaiwa na mwanasheria wa Serikali kuwa endapo watapewa dhamana wanaweza kuharibu ushahidi, kwani bado kuna watuhumiwa wengine wanaendelea kutafutwa.
Hakimu Odira baada ya kusikiliza maombi ya pande zote, aliamuru washitakiwa wapelekwe rumande hadi Julai 15, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.
Tukio la Lemi kukatwa mkono limekuwa la kwanza kutokea katika Mkoa wa Katavi tangu kuibuka kwa mauaji ya albino katika mikoa ya Geita, Simiyu na Shinyanga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles